Prime
Urais 2030 unavyoanza ‘kuitesa’ CCM
Muktasari:
- Viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali, wameshuhudiwa wakikemea kelele kuhusu vikumbo vya urais 2030.
Dar es Salaam. Imepita miezi saba tu, tangu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 ufanyike. Tayari joto la urais mwaka 2030 ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) limeanza kupanda na kufanya ajenda hiyo iwe midomoni mwa viongozi wa chama hicho na Serikali.
Wachambuzi wa siasa wanasema hali hiyo inaonyesha wazi, baadhi ya viongozi hawatumikii nafasi zao inavyopaswa, badala yake wamejikita kuandaa mazingira ya kushinda urais katika uchaguzi wa 2030.
Wadau wa siasa wamekuwa na mitazamo tofauti, wapo wanaoona suala hilo litarudisha nyuma jitihada za viongozi kuwaumikia wananchi na wengine wakikishauri chama hicho kutumia katiba na kanuni zake kuwachukulia hatua wanaoanza mipango hiyo nje ya muda.
Mmoja wa makada waandamizi wa CCM ambaye ameomba hifadhi ya jina lake anasema vuguvugu hilo si jepesi: “Mvutano upo chini kwa chini, wanaoutaka wanajipanga na tutaendelea kushuhudia hili hasa kuelekea uchaguzi wetu wa ndani mwakani.”
Anasema uchaguzi wa mwakani ndiyo utaanza kuchora ramani ya urais mwaka 2030 kwani wanaoutaka watajipanga kuanzia chini kwa kuhakikisha wanaweka watu wanaowaunga mkono ili iwe njia nyepesi ikifika 2030 ndani ya Bunge na hata urais.
Kigogo huyo amesema mbio hizo za urais si ndani ya chama tu hata serikalini, akidokeza wanaoonekana kuunga mkono upande fulani wanakutana na vibano vya kimyakimya: “Na hata huku chamani, kwa hiyo urais kwa kweli hauwezi kupita hivihivi bila kuacha kivumbi.”
Mei 23, mwaka huu, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, akiwa mkoani Iringa katika ziara ya kikazi, alionya wanaodai mwaka 2030 mfumo umepanga kumweka Rais anayetokana na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
“Leo hii hatujamaliza hata mwaka tangu tutoke kwenye uchaguzi, kila siku ajenda uchaguzi mambo ya ubinafsi. Taifa linalopaswa kupiga hatua miezi sita baada ya uchaguzi linajadili uchaguzi,” alisema Dk Mwigulu ambaye kiimani ni muumini wa KKKT.
Hali kama hiyo inajitokeza pia visiwani Zanzibar. Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wameibuka na ajenda ya mabadiliko ya Katiba ili Rais Hussein Mwinyi aongezewe muda wa kugombea 2030 baada ya kumaliza vipindi viwili.
Si mara moja pendekezo hilo limeibuka katika baraza hilo. Liliwahi kuibuka mwaka 2024 pia, hata hivyo, Dk Mwinyi alipinga hilo, akisema anaheshimu Katiba ya nchi.
Dk Mwinyi aliuzima mjadala huo akisema anaiheshimu Katiba ya Zanzibar na haoni sababu yoyote ya kufanya marekebisho kuongeza muda wa uongozi baada ya kumaliza miaka 10 inayotambuliwa kikatiba.
Katika hotuba yake, wakati wa kufungua Jukwaa la Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma na Binafsi, Mei 23, 2026, alisema ameapa kuilinda Katiba ya Zanzibar, haoni sababu ya kuanzisha mjadala wa kuongeza muda.
“Miaka minne na nusu iliyobaki ni mingi katika kuleta maendeleo, baada ya hapo tutapokezana kijiti. Ningependa kusema kuwa mjadala huu si wakati wake na hauna nafasi,” alisema.
Machi 27, 2026 Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira akiweka jiwe la Msingi ujenzi wa ofisi za CCM Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara aliwasisitiza wanachama wa chama hicho kuacha kuzungumzia urais 2030.
Alieleza Taifa bado lina kazi kubwa ya maendeleo inayohitaji umoja na mshikamano wa kisiasa.
"Unazungumziaje urais wa 2030 leo, wakati hata hujui kama utakuwepo? Hiyo ni kama kumjaribu Mungu. Wakati huu tunapaswa kujikita kwenye kazi za kujenga chama na nchi," alisisitiza.
Kauli kuhusu kuwepo vikumbo vya urais 2030, ilitolewa pia hata na Rais Samia Suluhu Hassan, alipozungumza na wazee wa Dar es Salaam, Desemba 2, mwaka jana.
Aliwatahadharisha wateule wake wenye nia ya urais 2030, waachie nafasi alizowapa, ili wafanye harakati hizo wakiwa nje ya Serikali.
“Nilizungumza na mawaziri wangu, nikawaambia namuangalia mmoja mmoja, una masilahi na huko, kaa nje kafanye huko usifanye ndani ya Serikali yangu. Nimekuweka hapo ukatumikie wananchi masilahi yako utayakuta mbele, Mungu ndio anajua nani kiongozi,” alisema
Hata hivyo, Uchaguzi Mkuu wa 2030, unatarajiwa kuja na marais wapya kwa pande zote kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, kwa kuwa waliopo sasa kutoka katika chama hicho watamaliza vipindi vyote vya kikatiba vya uongozi.
Kauli za kuwakemea wanaousaka urais 2030 ziliwahi kukemewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda akiwa mkoani Arusha, Machi 25 kwenye mkutano na wadau wa elimu aliwaambia wanaojipanga kwa urais mwaka 2030, hawatafanikiwa katika mbio hizo.
"Ukiona hao viongozi wanataka kujitenganisha, hii ni Serikali yeye akae pembeni awe sehemu ya wakosoaji wanaoikosoa Serikali. Watu wote wanaojipanga hawawezi kushika hata urais, 2030 hawapati,” alisema.
Hii ina maana gani
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Magabilo Masambu anasema kelele za 2030 zinatoa picha halisi, viongozi waliopo madarakani sasa hawatumikii nafasi zao vyema bali wanaangalia fursa zingine.
“Wanaoangalia 2030 na kujipanga ni watu ambao tayari wamekuwa viongozi au bado wana nafasi ya uongozi, hii inatoa ishara mbaya kwamba nafasi walizonazo sasa hawazitumikii kwa manufaa ya wananchi,”anasema.
Anasema mbio za urais za mapema, zina athari kwa wananchi kwani hawatapata maendeleo yaliyotarajiwa kutokana na viongozi waliopo kujikita kupanga safu zao kwa ajili ya uchaguzi ujao.
Masambu anasema viongozi kuonyesha nia mapema wakati wapo viongozi waliopo madarakani ni kutoridhishwa na uongozi uliopo.
Mjadala huo unachangiwa na Profesa Ali Makame ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa, akisema kitendo cha viongozi wakuu kukemea kunaonyesha kinachoendelea sio msimamo wa chama.
Harakati hizi kupingwa hadharani na viongozi wakuu kunaonyesha kinachofanyika hakiko sawa, hii maana yake ni nini kuna maandalizi yanafanyika kwa siri ambayo yanakwenda kinyume na msimamo wa chama,”anasema
Profesa Makame anasema ni mapema kuanza mbio za urais wakati hata ahadi zilizoahidiwa na viongozi waliochaguliwa hivi karibuni hazijaanza kutekelezwa.
Anasema kinachoendelea ni hatari kwani kunatengeneza makundi ndani ya jamii na kuibua mgawanyiko utakaochelewesha maendeleo ya wananchi.
“Tutumie muda huu kutekeleza yale ambayo wananchi wameahidiwa, kujipanga kwa uchaguzi 2030 ni mapema na ni hatari kwa maendeleo yetu,”anasema.
Mtazamo mwingine unatolewa na Wakili na mchambuzi wa masuala ya siasa, Ibrahim Bendera akisema CCM ina katiba yake, inapowaona watu wanashindwa kuifuata wachukue hatua na sio kukemea mara kwa mara.
“CCM ina katiba kama imebaini mtu anakwenda kinyume, wachukue hatua lakini lazima tukubali kuwa kwenye siasa uchaguzi maandalizi yake yanaanza sasa hata kama ni 2030,”anasema na kuongeza.
“Mtu anapaswa kujipanga muda huu, sasa kama kuna watu wanakemewa hao wanaokemea kuna jambo limejificha,”anasema.