Prime
Majimbo yenye ushindani CCM

Muktasari:
- Uchukuaji na urejeshaji wa fomu ndani ya chama hicho ulianza Juni 28, 2025 na utakamilika Julai 2, 2025 huku mwitikio ukiwa mkubwa kwa watu wenye hadhi tofauti
Dar es Salaam. Ikiwa imebaki siku moja kukamilika kwa mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania ubunge ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ushindani mkali unatarajiwa kwenye kura za maoni katika baadhi ya majimbo yaliyowakutanisha makada wenye nguvu.
Umaarufu, mvuto kwa wananchi na uzoefu wa muda mrefu ni miongoni mwa sifa zitakazowabeba baadhi ya watia nia huku uamuzi wa mwisho ukitarajiwa kufanywa na wajumbe kabla ya kutangazwa kwa mteule wa CCM kwenye jimbo husika.
Uchukuaji na urejeshaji wa fomu ndani ya chama hicho ulianza Juni 28, 2025 na utakamilika saa 10:00 jioni ya kesho Jumatano, Julai 2, 2025.
Katika siku nne za kwanza hadi leo, mwitikio umekuwa mkubwa watu wa hadhi tofauti wamejitokeza.
Waliojitokeza ni wabunge wanaomaliza muda wao, wa zamani, wasanii, watumishi wa umma, wafanyabiashara, waandishi wa habari, wahadhiri na wanachama wengine wakiwamo wenye nguvu kwenye maeneo yao.
Katika majimbo 272 yaliyopo nchini, baadhi ya majimbo yameonesha kutakuwa na ushindani mkali kutokana na kuwakutanisha watu wenye umaarufu na nguvu ya ushawishi kwa wananchi huku sintofahamu hiyo ikitarajiwa kuamuliwa na wajumbe kwenye kura za maoni.
Ushindani huo kwa makada hao waliojitosa kuchukua fomu, unategemea hasa vikao vya chama ngazi ya Taifa vitakavyofanya mchujo na kurejesha majina yatakayopigiwa kura na wajumbe wa mkutano mkuu wa jimbo.
Utaratibu wa mwaka huu, utakuwa tofauti na ule wa mwaka 2020 ambao mikutano ya jimbo ya CCM iliwapigia kura wale wote waliojitokeza kuchukua fomu.
Mwaka huu, inaeleza yatarejea majina matatu pekee ndiyo yatarudishwa kupigiwa kura za maoni.
Akizungumzia ushindani uliopo kwenye baadhi ya majimbo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Sabatho Nyamsenda amesema uzoefu unaonesha kunapokuwa na ushindani kwenye majimbo, chama kinawapa nafasi wajumbe kuamua.
Amesema wakati fulani huko nyuma, chama kiliwaacha watu waliokuwa na ushawishi na kuwachukua wenye nguvu ya fedha, jambo lililovipa nafasi vyama vya upinzani kushinda katika majimbo hayo.
“Ile iliibua makundi ndani ya chama na pia ilisaidia kuviimarisha vyama vya upinzani kwa sababu wagombea wa CCM, hata kama walikuwa na nguvu ya fedha, hawakuweza kuwashawishi wananchi kwenye uchaguzi,” amesema.
Nyamsenda ameishauri CCM kupitisha wagombea wanaokubalika na wananchi na kuachana na wale wanaotumia nguvu ya fedha kwa kuwa, watakwenda kukigharimu chama endapo wananchi hawakubali.
Majimbo yenye ushindani
Moja ya majimbo yanayotazamwa kwa karibu katika kinyang’anyiro cha ubunge ni Arusha Mjini kwa kuwakutanisha mbunge wake, Mrisho Gambo na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.
Wawili hao wamekuwa wakidhihirisha tofauti zao majukwaani tangu Makonda alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Machi 31, 2024 na mara kadhaa wamekuwa wakirushiana maneno majukwaani.
Jimbo jingine ni la Ilemela, uchaguzi wa ndani utawakutanisha mbunge wa jimbo hilo, Angelina Mabula na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Mnec), Leornad Qwihaya.
Angelina amekuwa mbunge wa Ilemela kwa miaka 10 na amekuwa waziri katika nyakati tofauti.
Pia, Qwihaya ni mfanyabiashara maarufu na kada wa CCM aliyeongoza katika kura za kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
Arumeru Magharibi hakutakuwa salama, kwa kuwa, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amejitosa kulitaka jimbo hilo ambalo linaongozwa na Noah Lembris.
Je, nani ataibuka mshindi, wajumbe wa mkutano mkuu wa jimbo hilo wataamua.
Mkoani Mwanza, Jimbo la Nyamagana, litakuwa na ushindani mkali kwa kuwa, wanaochuana kuwania jimbo hilo ni mbunge wa sasa, Stanslaus Mabula na mbunge wa zamani katika jimbo hilo, Lawrence Masha.
Kuanzia mwaka 2005 hadi 2010, Masha alikuwa Mbunge wa Nyamagana huku akihudumu katika nafasi ya mbalimbali serikalini ikiwamo ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini (2006), Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani (2006 - 2008) na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi (2008 - 2010).
Katika Jimbo la Namtumbo, waliotia nia ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera anayekwenda kumkabili mbunge wa jimbo hilo, Vita Kawawa, ushindani unaotarajiwa kuwa mkali.
Pia, katika Jimbo la Simanjiro, mbunge wa sasa, Christopher Ole Sendeka ambaye tayari amechukua fomu, atakabiliana na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, James Ole Millya ambaye kwa sasa ni mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala).
Ushindani wa wawili hao utakuwa mkubwa ukizingatia Ole Sendeka amekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa muda mrefu. Hata hivyo, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, alipoteza jimbo hilo kwa Millya ambaye wakati huo alikuwa Chadema, kabla ya kurejea CCM mwaka 2018.
Jimbo la Shinyanga Mjini, lina mvuto wake katika kinyang’anyiro hicho, miongoni mwa waliotia nia ya kugombea ubunge ni mbunge wa sasa, Patrobas Katambi na mbunge wa zamani, Stephen Masele.
Katika uchaguzi wa mwaka 2020, Masele aliongoza kura za maoni, hata hivyo, kamati kuu ilimpendekeza Katambi kukiwakilisha chama hicho kwenye uchaguzi ule.
Huko Busega, mbunge wa jimbo hilo, Simon Lusengekile anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa watangulizi wake, Raphael Chegeni na Dk Titus Kamani ambao wote wamechukua fomu kutia nia.
Katika kura za maoni uchaguzi wa mwaka 2015, Dk Chegeni alifanikiwa kumshinda Dk Kamani ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi. Hata hivyo, katika uchaguzi wa mwaka 2020, wawili hao waliangushwa na Lusengekile.
Jimbo la Sengerema, pia, litakuwa na ushindani wa aina yake kwa kuwa, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, William Ngeleja ametia nia akitaka kurudi kumkabili mbunge wa sasa, Tabasamu Mwagao ambaye naye amechukua fomu.
Tabasamu ambaye amekuwa mbunge kwa miaka mitano pekee, anapambana kurejea katika kiti hicho huku Ngeleja, aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini katika Serikali ya Awamu ya Nne, naye anataka kurudi katika jimbo hilo.
Mbali ya Tabasamu na Ngeleja kuna Ngussa Samike aliyekuwa Katibu wa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli ambaye naye analitaka jimbo hilo.
Katika Mkoa wa Kilimanjaro, Jimbo la Siha linakabiliwa na ushindani mkubwa kwenye hatua ya kura za maoni ndani ya CCM ambako vigogo waliochukua fomu hadi sasa ni mbunge wa sasa, Dk Godwin Mollel na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri.
Dk Mollel ambaye pia ni Naibu Waziri wa Afya, amekuwa mbunge wa Siha kwa miaka 10, sasa anatarajia kushindana na Mwanri ambaye naye alikuwa Naibu Waziri wa Nchi, Tamisemi katika Serikali ya awamu ya nne.
Kinondoni jijini Dar es Salaam, nako kunatarajiwa kuwa na mshikemshike kati ya mbunge wa sasa, Abbas Tarimba na mbunge wa zamani katika jimbo hilo, Idd Azzan.
Wawili hao wamejijengea ngome katika jimbo hilo, jambo linalofanya ushindani kuwa mkali.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo amechukua fomu kuwania ubunge Jimbo la Makambako, linaloongozwa na mbunge wa sasa, Deo Sanga maarufu Jah People, ambaye amekuwa mtetezi wa Serikali.
Mchakamchaka mwingine unatarajiwa kuonekana Jimbo la Butiama huku waliochukua fomu ni mbunge wa sasa, Jumanne Sagini ambaye ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria na aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Wilson Mahera.