Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kutoka mipango, mauaji hadi askari kunyongwa-1

Muktasari:

  • Hukumu ya kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa  madini yenye kurasa 60 na maneno zaidi ya 13,000 imejengwa juu ya ushahidi wa mashahidi 28 upande wa mashtaka, vielelezo 16 vya upande wa mashtaka, utetezi wa washtakiwa saba na vielelezo vitatu walivyowasilisha

Dar es Salaam. “Kesi hii inaonesha hali ya kusikitisha na ya kushangaza, askari polisi ambao waliapa kulinda sheria na usalama wa maisha na mali za raia, sasa wameshtakiwa kwa kosa kubwa la kutisha la mauaji linaloweza kuharibu kabisa uaminifu wa kipekee uliowekwa kwao, badala ya kuwa kimbilio kwa watu wenye hofu, uwepo wao sasa unasababisha hofu.”

Hiyo ni tafsiri isiyo rasmi ya sehemu ya maelezo ya utangulizi wa hukumu ya Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mtwara kuhusu kesi ya mauaji ya kukusudia iliyokuwa ikiwakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara.

Kesi hiyo ilihusu mauaji ya mfanyabiashara wa madini kutoka Wilaya ya Nachingweya mkoani Lindi, Mussa Hamis ambayo awali mauaji yake yalifichwa na maofisa wa polisi walioyapanga na kuyatekeleza kwa nia ovu.

Hukumu hiyo yenye kurasa 60 na maneno zaidi ya 13,000 imejengwa juu ya ushahidi wa mashahidi 28 upande wa mashtaka, vielelezo 16 vya upande wa mashtaka,  utetezi wa washtakiwa saba na vielelezo vitatu walivyowasilisha.

Chanzo cha yote ni pesa. Huu ndio muhtasari wa jumla wa yaliyomo katika hukumu hiyo. Inaonesha fedha ndiyo msingi na chanzo cha kesi na hatimaye hukumu kutolewa.

Mussa alikuwa mfanyabiashara wa madini, mazao ya biashara na mavazi, akifanya shughuli zake mkoani Dar es Salaam na Wilaya ya Nachingwea, Mkoa wa Lindi.

Alijipatia fedha kwa juhudi na kazi zake kwa ajili ya maisha yake na familia yake.

Mussa  alikuwa na haki ya kutumia fedha hizo kwa njia yoyote halali bila kuvunja sheria. Vyombo vya dola vilikuwa na jukumu la kuhakikisha usalama wake wakati anatekeleza haki hiyo bila kuumizwa au kudhurika.

Hata hivyo, mambo yalikuwa tofauti. Fedha zake zikawa chanzo cha matatizo yake.

Washtakiwa, ambao ni polisi wenye dhamana ya kulinda raia na mali zao, walimkamata wakimtuhumu kujihusisha na wizi wa pikipiki kwa sababu tu walimuona akitumia fedha nyingi.

Baada ya kushindwa kupata ushahidi wa kuthibitisha tuhuma hizo, walimuachia lakini walichukua mali zake kwa nguvu na kumtishia asizidai tena.

Waliposikia anawalalamikia kwa kupora mali hizo, walipanga njama za kumuua ili kumnyamazisha.

Kwa tamaa ya pesa na mali, walitelekeza kiapo chao cha kulinda usalama wa raia na mali zao na kuishia kujipatia matatizo makubwa; hatimaye wakajikuta wakikabiliwa na kesi nzito ya mauaji ya kukusudia na kuhukumiwa.

Washtakiwa katika kesi ya mauaji namba 15 ya mwaka 2022 ni Gilbert Sostenes Kalanje, Charles Maurice Onyango, Nicholous Stanslaus Kisinza, Marco Mbuta Chigingozi, John Yesse Msuya, Shirazi Ally Mkupa na Salim Juma Mbalu.

Mshtakiwa wa kwanza, Kalanje, alikuwa na cheo cha Mrakibu wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara.

Mshtakiwa wa pili, Onyango alikuwa Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara.

Mshtakiwa wa tatu, Kisinza, alikuwa Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Ofisa wa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara. Mshtakiwa wa nne, Chigingozi, alikuwa Mkaguzi Msaidizi.

Mshtakiwa wa tano, Msuya, alikuwa Mkaguzi na Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara, mshtakiwa wa sita, Mkupa, alikuwa Mkaguzi Msaidizi na mshtakiwa wa saba, Salim Juma Mbalu, alikuwa Koplo.

Wote walikabiliwa na shtaka moja la mauaji ya kukusudia, wakidaiwa kumuua kwa makusudi Mussa, kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya 2022.

Kosa lilielezwa kuwa,  Januari 5, 2022, katika Kituo cha Polisi Mitengo, Wilaya ya Mtwara, washtakiwa walimuua Mussa.

Inadaiwa walimuua kwa kumziba mdomo na pua kwa kutumia kitambaa baada ya kumchoma sindano yenye dawa ya usingizi ili asiendelee kuwadai pesa na mali walizochukua walipompekua nyumbani kwake kwa tuhuma za wizi wa pesa na pikipiki.

Baada ya mauaji hayo, walichukua mwili wake na kwenda kuutupa Kijiji cha Majengo, Kata ya Hiari karibu na Kiwanda cha Saruji cha Dangote.

Mwanzo wa mambo yote

Ili kuelewa mazingira ya mauaji hayo ya kikatili na ya kusikitisha, ni vema kueleza historia fupi ya tukio hilo jinsi ilivyokuwa mpaka kusababisha washtakiwa (askari hao) kutiwa mbaroni na kushtakiwa kwa mauaji ya kukusudia.

Simulizi ya mauaji ya mfanyabiashara huyo na hatimaye kesi ya hukumu, inaanzia Oktoba 2021.

Katika tarehe isiyofahamika, Oktoba 2021, Mussa alikwenda nyumbani kwao Kijiji cha Luponda wilayani Nachingwea, Mkoa wa Lindi na akawaeleza wazazi wake kuwa anataka kuikarabati nyumba yao.

Pia, aliwaeleza wazazi wake alikuwa na fedha za kigeni alizotaka kuzibadilisha ili kutimiza azma yake hiyo.

Hivyo, alikwenda mkoani Mtwara akiwa na rafiki yake Said Makala kwa kusudi hilo la kubadilisha fedha hizo; walifika Mtwara na kulala nyumba ya wageni ya Sadina Lodge.

Oktoba 20, 2021, washtakiwa wote walikuwa zamu wakitekeleza majukumu yao katika nafasi zao.

Mshtakiwa wa tatu, Kisinza aliyekuwa Mrakibu Msaidizi wa Polisi  alipata taarifa za kiintelijensia kuwa, watu wawili wanaume walikutwa wakitumia fedha nyingi ndani ya Wilaya ya Mtwara na waliwashuku kuwa wezi wa pikipiki.

Hivyo, Kisinza alimwelekeza mshtakiwa wa saba, Koplo Mbalu kupeleleza taarifa hizo.

Koplo Mbalu aliwapeleleza watu hao wawili na akabaini kuwa walikuwa wakiishi katika Sadina Lodge iliyoko Wilaya ya Mtwara.

Koplo Mbalu alitoa taarifa za uchunguzi wake huo kwa Kalanje aliyekuwa  Mrakibu wa Polisi  na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara, Kisinza na kwa Onyango (Mrakibu Msaidizi wa Polisi), ambao walimwelekeza mshtakiwa wa nne, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi,  Chigingozi kuwakamata watu hao na kufanya operesheni ya upekuzi na ukamataji wa vielelezo ambavyo wangevikuta chumbani kwa watuhumiwa hao.

Chingingozi aliandaa timu ya ukamataji wa watu hao wawili humo Sadina Lodge.

Timu hiyo iliundwa na mshtakiwa wa sita, Mkaguzi Msaidizi Mkupa, mshtakiwa wa saba, Koplo Mbalu, Grayson Gatian Mahembe na Mkaguzi Msaidizi, Shadhil Simai Makame.

Chigingozi na timu yake walifika katika nyumba ya kulala wageni ya Sadina walikokutana na mmoja wa waliokuwa wakiwatuhumu, katika chumba namba sita na wakamuweka chini ya ulinzi. Mtuhumiwa huyo alijitambulisha kuwa ni Mussa.

Walifanya upekuzi chumbani kwa mtuhumiwa na wakamkamata akiwa na Sh2.3 milioni.

Ikaelezwa kuwa, askari hao walimchukua mtuhumiwa huyo na kwenda naye Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara walikomuweka mahabusu ya polisi na akafunguliwa jalada namba MTW/RB/1330/2021, likipewa namba ya usajili wa kuwekwa kizuizini 271.

Hukumu hiyo inasomeka kuwa, kesho yake (Oktoba 21, 2021), Onyango alimuamuru  Chigingozi, Mkupa na Koplo Mbalu walikwenda nyumbani kwa kina Mussa (mtuhumiwa), Kijiji cha Luponda kufanya operesheni ya ukaguzi na ukamataji.

Hivyo, Onyango alitoa hati ya amri ya kuwaruhusu askari hao kusafiri nje ya Mkoa wa Mtwara na kupatiwa kibali chenye namba 96774.

Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Chigingozi, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Mkupa na Koplo Mbalu walimchukua mtuhumiwa Mussa mahabusu ya polisi na kwenda naye nyumbani kwao.


Kijijini kwao Mussa, nini kilichojiri? Usikose sehemu ya pili ya simulizi hii, kesho