Prime
Askari waliomuua muuza madini wahukumiwa kunyongwa

Muktasari:
- Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa wakati wa shauri hilo, mauaji hayo yalifanyika Januari 5, 2022 katika Kituo cha Polisi cha Mitengo mkoani Mtwara, mfanyabiashara huyo alichomwa sindano yenye sumu.
Mahakama Kuu Masjala Ndogo, Mtwara imewahukumu adhabu ya kunyongwa mpaka kufa maofisa wawili wa Jeshi la Polisi mkoani humo, akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC-CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje.
SP Kalanje na mwenzake, aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango, wamehukumiwa adhabu hiyo baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya mauaji ya muuza madini, Mussa Hamis.
Mbali na SP Kalanje na ASP Onyango, washtakiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa aliyekuwa ofisa intelijensia ya jinai Mkoa wa Mtwara, SP Nicholaus Stanslaus Kisinza, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Marco Mbuta Chigingozi.
Wengine ni Mkaguzi wa Polisi, John Yesse Msuya, aliyekuwa Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.

Picha ya askari polisi wakiwa wanafatilia kesi yao katika mahakama mkuu kanda ya Mtwara kati ya hao wawili wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa ambao na wakwanza kutoka kulia na watatu kutoka kulia.
Washtakiwa wote walikabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia dhidi ya Mussa Hamis, mfanyabiashara wa madini mkazi wa kijiji cha Ruponda, wilayani Nachingwea, mkoani Lindi.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, washtakiwa hao walidaiwa kumuua Mussa Januari 5, 2022, katika Kituo cha Polisi Mitengo, Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara na kwenda kuutupa mwili wake katika kijiji cha Majengo, Kata ya Hiari karibu na kiwanda cha saruji cha Dangote.
Walidaiwa kumuua kwa kumziba mdomo na pua kwa kutumia tambala, baada ya kumchoma sindano ya dawa ya usingizi, ili asiendelee kuwadai pesa na mali zake walizozichukua walipokwenda kumpekua nyumbani kwao, kijiji cha Ruponda, wilayani Nachingwea, Lindi, wakimtuhumu kwa wizi wa pesa na pikipiki.
Akitoa hukumu hiyo leo, Jumatatu, Juni 23, 2025, Jaji Edwin Kakolaki alisema washtakiwa waliotiwa hatiani SP Kalanje na ASP Onyango baada ya kuridhika kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka dhidi yao bila kuacha mashaka yoyote.
Wakati maofisa hao wawili wakitiwa hatiani, wenzao watano ambao ni SP Kisinza, Wakaguzi Wasaidizi wa Polisi, Chigingozi na Mkupa, Mkaguzi wa Polisi, Msuya na Koplo Mbalu wameachiwa huru baada ya mahakama kuwaona kuwa hawana hatia katika kesi hiyo.
Mkuu wa waendesha mashtaka Mkoa wa Mtwara, Wakili wa Serikali Mkuu, Neema Haule amelithibitishia Mwananchi kuhusu hukumu hiyo.
“Ni kweli hukumu hiyo imesomwa leo na hao washtakiwa wawili, SP Kalanje na ASP Onyango ndio wamepatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa, lakini washtakiwa wengine wameachiwa huru,” amesema Wakili Haule.
Ushahidi ulivyokuwa
Miongoni mwa mashahidi waliotoa ushahidi katika kesi hiyo ni mama wa marehemu, Hawa Bakari ambaye pamoja na maelezo yake aliomba akabidhiwe mifupa ya mwanaye, iliyookotwa mahali alipotupwa baada ya kuuawa, ili akaizike.
Shahidi mwingine alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Ilala, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (ACP) Yustino Mgonja ambaye wakati wa mauaji hayo alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) wa Mtwara.
Aliieleza mahakama jinsi kile alichodai kuwa mipango ya mauaji hayo ilivyofanyika na kutekelezwa hatua kwa hatua.
Alidai kuwa aliyafahamu hayo yote kutoka kwa mmoja wa askari hao ambaye pia alikuwa mmoja wa washtakiwa katika kesi hiyo, Grayson Gaitan, alipomhoji na kwamba aliwapeleka polisi mahali mwili huo ulipotupwa na ikapatikana mifupa ya miguu na mbavu zake.
Hata hivyo askari huyo alifariki dunia Januari 22, 2022, akidaiwa kujinyonga akiwa mahabusu, siku chache baada ya kutiwa mbaroni na wenzake, na kabla ya kupandishwa kizimbani.
Pia kuna Mkemia wa Serikali Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), makao makuu Dar es Salaam, Fidelis Bugoye.
Bugoye, shahidi wa tisa ndiye aliyefanya uchunguzi wa vinasaba vya mifupa hiyo iliyopatikana mahali ambako mwili wake ulitupwa baada ya kuuawa, na kulinganisha na vinasaba kwenye sampuli ya mate ya mama wa marehemu Mussa, Hawa Bakari Ally, ambavyo vilioana.