Prime
Kutoka mipango, mauaji mpaka askari kunyongwa– 2

Muktasari:
- Walitenda kosa hilo, Januari 5, 2022, katika Kituo cha Polisi Mitengo wilayani humo.
Dar es Salaam. Askari saba wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara walishtakiwa kwa kumuua makusudi, Mussa Hamis, mfanyabiashara wa madini, mazao ya biashara na mavazi kutoka Wilaya ya Nachingwea, Lindi.
Walitenda kosa hilo, Januari 5, 2022, katika Kituo cha Polisi Mitengo wilayani humo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Gilbert Sostenes Kalanje aliyekuwa Mrakibu wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara, Charles Onyango (Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara), Nicholous Kisinza (Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Ofisa wa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara), Marco Chigingozi (Mkaguzi Msaidizi), John Msuya (Mkaguzi na Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara), Shirazi Mkupa (Mkaguzi Msaidizi )na Salim Mbalu alikuwa Koplo.
Jana, tulieleza namna washtakiwa walivyomkamata Mussa katika nyumba ya kulala wageni mjini Mtwara alipokwenda kubadilisha fedha za kigeni, alizopanga kuzitumia kukarabati nyumba kijijini kwao Luponda, wilayani Nachingweya, Lindi. Sasa endelea.
Oktoba 21, 2021, siku moja baada ya kumkamata Mussa, Mrakibu wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara Onyango, aliwaamuru askari Chigingozi, Mkupa na Koplo Mbalu kwenda nyumbani kwao mtuhumiwa kijijini Luponda, kufanya operesheni ya ukaguzi na ukamataji.
Hivyo, Onyango alitoa hati ya amri ya kuwaruhusu askari hao kusafiri nje ya kituo chao cha kazi, Mkoa wa Mtwara yenye namba 96774.
Askari hao walimchukua Mussa kutoka mahabusu ya polisi na kwenda naye nyumbani kwao, ambako Mkaguzi Msaidizi Chigingozi alifanya upekuzi na ukamataji nyumbani kwa Mussa, mbele ya mama yake, Hawa Ally.
Katika upekuzi huo, alikamata Dola 13,558 za Marekani (Sh35 milioni kwa viwango vya sasa), paneli moja ya umeme wa jua (sola), betri moja ya sola na chaja ya invertor moja katika nyumba alimokuwa akiishi Mussa.
Vilevile walipata Sh1,050,000 katika nyumba ya rafiki wa Mussa, aitwaye Said Ahmad.
Hata hivyo, paneli moja ya sola waliiacha katika Kituo cha Polisi Nachingwea kwa kuwa haikuweza kuingia katika gari walilokuwa nalo, mali nyingine zilizokamatwa pamoja na Mussa, zilipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara.
Mali hizo zilikabidhiwa kwa washtakiwa wa kwanza, Kalanje na wa pili, Onyango walioshirikiana kuzichukua pamoja na washtakiwa wa tatu, nne, sita na saba kinyume cha sheria.
Oktoba 24, 2021, Onyango aliamuru askari G.401 Koplo Ikangilo kumwachia Mussa kwa dhamana bila kuwa na wadhamini.
Baada ya kuachiliwa, Onyango alimpatia Mussa Sh130,000 kama nauli na akamuonya kutojaribu kuchukua mali zake kutoka polisi.
Mussa aliondoka kituoni hapo akarudi nyumbani kwao kijijini Luponda na aliieleza familia na marafiki zake kuwa polisi walimnyang’anya mali zake.
Pia, alifikisha malalamiko hayo kwa viongozi wa Serikali wilayani Nachingwea, ambao waliyafikisha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) mkoani Lindi na NPS iliwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki.
Onyango alipata taarifa za malalamiko ya Mussa kuwa walimpora mali zake na alimjulisha Kalanje ambaye ndiye alikabidhiwa mali hizo zilizochukuliwa kwa Mussa.
Kalanje alimuelekeza Chigingozi amwite Mussa afike Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara ili akutane naye ofisini kwake.
Simu ya wito wa mauti
Januari 2, 2022, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Chigingozi alimjulisha Mussa kwa njia ya simu anatakiwa kufika Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara.
Mussa alipata hofu na akamweleza mama yake aliyemshauri asiende peke yake bila kuwataarifu mamlaka za Serikali na alimtaka awasiliane na mjomba wake, Salum Ng’ombo ili aende naye Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara.
Mussa alifuata ushauri wa mama yake, akawasilisha malalamiko na hofu yake katika ofisi ya NPS Mkoa wa Lindi, alikopewa barua na Mwanasheria wa Serikali wa Mkoa (RPO) wa Lindi, iliyomuelekeza kuwasilisha malalamiko hayo katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Mtwara.
Januari 4, 2022, Mussa alifika Ofisi ya NPS Mkoa wa Mtwara akiwa ameambatana na mjomba wake, Ng’ombo, ambako malalamiko yake yalipokewa.
Januari 5, 2022, Mussa alipokea barua ya majibu ya malalamiko yake kutoka NPS Mkoa wa Mtwara, iliyomjulisha kuwa malalamiko yake yanafanyiwa kazi.
Pia, kwa kutii wito wa Mkaguzi Msaidizi Chigingozi, Mussa na mjomba wake walifika Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, walikompigia simu Afande Chigingozi kumjulisha kuwa wamefika.
Afande Chigingozi, alimuelekeza Inspekta Msaidizi Grayson Mahembe, aliyekuwa kituoni wakati huo, amshughulikie Mussa na kumpeleka katika ofisi ya Kalanje, naye akatekeleza.
Mjomba alivyofukuzwa kituoni
Wakiwa ofisini kwa Kalanje, mjomba wake Mussa alitolewa na kwenda kumsubiria Mussa nje ya kituo.
Mussa alihojiwa kisha akafungiwa stoo akaambiwa asubiri maelekezo zaidi.
Wakati mjomba wa Mussa akimsubiria nje ya kituo atoke, Kalanje alimuamuru aondoke kituoni hapo, naye akatii na kuondoka lakini mjomba wake huyo akajaribu kumpigia simu Mussa na haikupokewa.
Baadaye mjomba wake Mussa alipokea ujumbe wa maandishi kutoka kwenye simu ya Mussa uliosema, “waliniachia” “tukutane nyumbani” na baada ya ujumbe huo, kuanzia hapo simu ya Mussa haikupatikana tena.
Mipango ya mauaji
Siku hiyo hiyo, Kalanje alimtafuta mshtakiwa wa tano, Inpekta Msuya (aliyekuwa Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara) na kumwomba msaada wa kumuua Mussa kwa kumdunga sindano ya sumu.
Kalanje alimweleza Inspekta Msuya kuwa alitaka kumuua Mussa, kwa kuwa hakuwa tayari kutoa ushirikiano, kuwataja wahalifu wenzake wanaohusika na wizi wa pikipiki katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.
Kwa mujibu wa Inspekta Msuya, hakuwa tayari kushiriki kitendo hicho badala yake, alimshauri Kalanje kuwa angemsaidia kumdunga sindano mtuhumiwa (Mussa) sindano ya dawa iitwayo “Ketamine.”
Inspekta Msuya alimweleza Kalanje kuwa dawa hiyo humfanya mtu kutokuwa na uwezo wa kujitambua na baada ya kuamka, anaweza kufichua taarifa zote kuhusu matendo yake ya uhalifu na wenzake.
Kalanje aliridhika na ushauri huo, hivyo Kalanje, Onyango na Inspekta Msaidizi Mahembe walimtoa Mussa katika chumba alichokuwa amefungiwa, wakampandisha kwenye gari la Kalanje.
Wote walipanda gari hilo na kuelekea Zahanati ya Polisi Mtwara kumchukua Inspekta Msuya kisha wakaelekea Kituo cha Polisi Mitengo.
Mussa alivyochomwa sindano
Walipofika Kituo cha Polisi Mitengo, Kalanje na Inspekta Msuya waliokuwa wamekaa mbele ya gari hiyo walishuka huku Onyango na askari Grayson wakimshusha Mussa, wote wakaingia ndani ya kituo hicho cha polisi.
Waliingia kwenye chumba cha stoo ya ofisi, kilichokuwa kimetengwa kwa ajili ya Kalanje aliyekuwa amekiomba kukitumia kumfanyia mahojiano Mussa.
Walinzi wa Kituo cha Polisi Mitengo waliagizwa wasiingilie shughuli hiyo.
Ndani ya chumba hicho, Kalanje alimwambia Inspekta Msuya amdunge sindano Mussa.
Mussa aliyekuwa amevuliwa shati, akiwa amejaa hofu na mshangao, Inspekta Msuya alimwelekeza alale chini na mara moja akamdunga sindano hiyo.
Fuatilia kesho Jumatano kujua nini kiliendelea