Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wengine wachukua fomu ubunge CCM, wamo waliokuwa wabunge wa Chadema

Muktasari:

  • Waliotia fora katika mchakato huo, wamo waliokuwa wabunge 19 wa viti maalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao baada ya kuhitimishwa kwa shughuli za Bunge, Juni 27, 2025, wameibukia CCM wakichukua fomu.

Dar/Mikoani. Makada wa CCM wamezidi kujitokeza kuchukua fomu katika majimbo mbalimbali nchini wakiomba ridhaa ya kukiwakilisha Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 utakaohusisha wagombea kutoka vyama vingine.

Ikiwa ni siku ya pili tangu kuanza kwa mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu hizo, makada wa chama hicho wamemiminika kwenye ofisi za makatibu wa wilaya kuchukua fomu hizo zinazotolewa kwa gharama ya Sh500,000 huku za udiwani zikilipiwa Sh50,000.

Miongoni mwa watia nia waliochukua fomu zao leo, wamo wanaotaka ubunge kwenye majimbo na wengine wametia nia kwenye ubunge wa viti maalumu kupitia jumuiya za chama hicho.

Waliotia fora katika mchakato huo, wamo waliokuwa wabunge 19 wa viti maalumu kupitia Chadema (waliofukuzwa uanachama) ambao baada ya kuhitimishwa kwa shughuli za Bunge, Juni 27, 2025, wameibukia CCM wakichukua fomu.

Matiko aibukia Tarime

Aliyekuwa mbunge wa viti Maalumu kupitia Chadema, Ester Matiko ametangaza kujiunga na CCM na kuchukua fomu ya kugombea ubunge Jimbo la Tarime Mjini.

Endapo atafanikiwa kupitishwa na CCM na kufanikiwa kushinda uchaguzi, hii itakuwa ni mara ya pili kwa Matiko kuongoza jimbo hilo ambapo mara ya kwanza alikuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema kuanzia mwaka 2015 – 2020.

Jimbo la Tarime mjini kwa sasa linaongozwa na Michael Kembaki (CCM) ambaye alimshinda Matiko akiwa Chadema kwenye kunyang'anywa cha uchaguzi mwaka 2020.

Hadi jana jioni, jumla ya makada wanne wa CCM, wote wakiwa ni wanaume, walikuwa wamechukua fomu kwa ajili ya mchakato wa uchaguzi wa ndani ya chama kumpata mgombea atakayewakilisha chama hicho kwenye kampeni na uchaguzi ujao.

Felista naye Moshi Vijijini

Mbunge mwingine wa viti maalumu, aliyetokea Chadema, Felista Njau, amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM kugombea ubunge katika Jimbo la Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro.

Njau amechukua fomu leo Juni 29, 2025 katika ofisi za CCM Wilaya ya Moshi Vijijini na kukabidhiwa na Kaimu Katibu wa chama hicho, Adrew Mwandu.

Felista anakuwa mwanachama wa nane kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea ubunge Jimbo la Moshi vijijini ambalo limeongozwa na Profesa Patrick Ndakidemi kati ya mwaka 2020-2025.

Salome Makamba yumo

Kwingineko mkoani Shinyanga, aliyekuwa mbunge wa viti maalumu kupitia Chadema (waliofukuzwa uanachama), Salome Makamba amejitokeza katika ofisi za CCM mkoani humo kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea tena nafasi hiyo kwa wanawake kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).

Fomu hiyo imekabidhiwa kwa Makamba leo Jumapili, Juni 29, 2025 na Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Shinyanga, Habiba Musimu, katika ofisi za chama mkoani humo.


Mahundi ataka tena

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhandisi Maryprisca Mahundi amechukua fomu kutetea nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Naibu Waziri huyo amechukua fomu hiyo leo Juni 29, 2025 katika ofisi za UWT Mkoa wa Mbeya na kukabidhiwa na Katibu wa UWT Mkoa wa Mbeya, Amina Mwilu.

Tarimo kutetea jimbo

Mbunge wa Moshi Mjini Mkoa wa Kilimanjaro, Priscus Tarimo amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM kugombea ubunge katika jimbo hilo.

Tarimo amechukua fomu leo katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi Moshi Mjini, ambapo amekabidhiwa fomu hiyo na Kaimu Katibu wa CCM wilayani humo, Hilary Kipingi.


Kilolo kumekucha

Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Justin Lazaro Nyamoga ameanza safari ya kutetea nafasi yake kwa kuchukua fomu ya ubunge kupitia CCM huku wagombea wengine pia wakijitokeza kuwania nafasi hiyo, wakiongeza ushindani ndani ya chama hicho.

‎Leo Juni 29, 2025 Mwananchi Digital imeshuhudia kuwa mbali na Nyamoga kuna wagombea wengine wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo ndani ya CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

‎Viongozi hao waliochukua fomu za kuwania ubunge Jimbo la Kilolo Bryan Kikoti, aliyewahi kushika nafasi ya pili kwenye kura za maoni mwaka 2020, amerejea tena kuwania nafasi hiyo. ‎Shamdi Nzogela ambaye ni mfanyabiashara wa Kilolo, naye amechukua fomu kuwania nafasi hiyo.

‎Vilevile Mdau wa maendeleo na kada wa CCM Mkoa wa Iringa, Aidan Mlawa amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea ubunge wa Jimbo la Kilolo. Pia, msanii maarufu wa filamu, Stanley Msungu maarufu Madevu, naye amechukua fomu.


Kivule nako moto

Wakati huohuo, Mkurugenzi wa kampuni ya Amala Florian Karugaba amekabidhiwa fomu ya kuwania ubunge katika jimbo jipya la Kivule kupitia CCM na Katibu wa chama hicho Wilaya ya Ilala, Chief Sylvester.