Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makada CCM waendelea kujitosa ubunge, ushindani waongezeka majimboni

Muktasari:

  • Miongoni mwa waliojitokeza ni pamoja na wabunge wanaotetea majimbo yao, wabunge wa zamani, wafanyabiashara, wasanii, watumishi wa umma, watoto wa vigogo pamoja na waliokuwa wakuu wa mikoa kabla ya kuondolewa katika nafasi zao.

Dar/Mikoani. Mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuomba ridhaa ya kugombea ubunge na udiwani katika Chama cha Mapinduzi (CCM) umeingia siku ya pili leo Juni 29, 2025 huku makada wengine wakiendelea kujitokeza kuchukua fomu.

Shughuli hiyo ilianza jana Juni 28, 2025 ambapo makada mbalimbali wa chama hicho walijitokeza kuchukua fomu katika ofisi za CCM wilaya nchi nzima, huku ushindani ukitarajiwa kuwa mkali katika hatua ya kura za maoni.

Miongoni mwa waliojitokeza jana na leo ni wabunge wanaotetea majimbo yao, wabunge wa zamani, wafanyabiashara, wasanii, watumishi wa umma, watoto wa vigogo pamoja na waliokuwa wakuu wa mikoa kabla ya kuondolewa katika nafasi zao.

Baadhi ya waliochukua fomu siku ya kwanza na majimbo wanayotaka kugombea ni pamoja na Daniel Chongolo (Makambako), Lazaro Nyalandu (Ilongero), Dk Tulia Ackson (Uyole), Paul Makonda (Arusha Mjini), Kulwa Biteko (Katoro) na Masanja Kadogosa (Bariadi Vijijini).

Kwa mujibu wa ratiba ya CCM, shughuli hiyo ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania ubunge kupitia chama hicho itafanyika kwa siku tano hadi Julai 2, 2025, baada ya hapo wajumbe watapiga kura kumchagua atakayepeperusha bendera ya chama hicho.

Leo, siku ya pili ya uchukuaji fomu, makada wengine wameendelea kuchukua fomu za kuwania ubunge katika majimbo mbalimbali nchini huku wengine wakianza kurejesha fomu zao baada ya kumaliza kuzijaza.

Masha arejea uwanjani

Mbunge wa zamani wa Nyamagana, Lawrence Masha amerejea rasmi katika kinyang’anyiro cha kisiasa kwa kuchukua fomu ya kuwania tena ubunge kupitia CCM katika jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza.

Masha amekabidhiwa fomu hiyo leo Jumapili Juni 29, 2025 na Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Deogratias Nakei.

Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM taifa kutoka Arumeru Magharibi, Ezekiel Mollel naye amejitokeza kuchukua fomu ya kuwania ubunge Jimbo la Arumeru Magharibi.

Mollel ambaye pia ni mwalimu amekabidhiwa fomu hiyo leo Jumapili Juni 29, 2025, na Katibu wa CCM Wilaya ya Arumeru, Kamila Kigosi.

 ‘Jah People’ kutetea jimbo

Siku moja baada ya Chongolo kujitosa Jimbo la Makambako, mbunge anayetetea nafasi yake katika jimbo hilo, Deo Sanga amechukua fomu leo Juni 29, 2025 kuomba ridhaa ya kuendelea kukiwakilisha chama hicho bungeni.

Sanga amekabidhiwa fomu na Katibu wa CCM Wilaya ya Njombe, Mariam Kireti.

Mbali na hao, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko leo Jumapili, Juni 29, 2025 amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kumteua tena kuwa mgombea ubunge wa Bukombe, Mkoa wa Geita.


Pia aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, John  Nchimbi ameonekana akiwa ameshikilia fomu ya kugombea ubunge Jimbo la Nyasa baada ya kuichukua katika Ofisi Kuu ya CCM wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.

Dk Biteko amechukua fomu hiyo na kuirejesha kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Bukombe, Leonard Mwakalukwa.

Mwingine aliyechukua fomu leo ni Meya wa Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, Abdallah Mtinika amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwania Jimbo la Mbagala.

Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo naye amechukua fomu kutetea jimbo hilo.  Gambo amekabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa CCM Wilaya ya Arusha, Timoth Sanga.


Mkulima ajitosa Vwawa

Mmiliki wa kiwanda cha kahawa na kuchakata zao la parachichi (LIMA) Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Tinson Nzunda amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea ubunge Jimbo la Vwawa kupitia CCM.



Nzunda amekabidhiwa fomu hiyo leo Juni 29, 2025 na Katibu wa chama hicho wilayani Mbozi, JuliusMbwiga.

Katika hatua nyingine, Bahati  Soja ambaye kitaaluma ni mwalimu wa sekondari na mtaalamu wa saikolojia, naye amjitosa kuomba ridhaa ya kugombea ubunge jimbo la Mbeya vijijini. Soja amekabidhiwa fomu yake na Katibu wa CCM Wilaya ya Mbeya Vijijini, Rehema Mpagile jana Jumamosi, Juni 28, 2025.


Mtoto wa Mashishanga yumo

Rachel Mashishanga, mtoto wa mwanasiasa mkongwe nchini, Stephen Mashishanga, amechukua fomu ya ubunge wa viti maalumu kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Morogoro.


Rachel amekabidhiwa fomu hiyo leo Juni 29,2025 na Katibu wa UWT Mkoa wa Morogoro, Mwajabu Maguluko.

Mtoto mwingine wa kiongozi aliyechukua fomu ya kugombea ubunge ni Dk Kellenrose Lwakatale ambaye ni mtoto wa marehemu Dk Getrude Lwakatakele, aliyekuwa mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Morogoro.

Dk Kellenrose amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwa mgombea wa ubunge Jimbo la Mlimba.

Pia  Dk Seria Masole amechukua fomu leo Juni 29,2025 kuwaniwa ubunge Jimbo la Uyole.

Shilole achukua fomu

Msanii na mjasiriamali, Zena Mohamed, maarufu Shilole, amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea ubunge viti maalumu Mkoa wa Tabora.

Shilole amekabidhiwa fomu leo Juni 29, 2025 na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoani humo, Rhoda Madanha.

Mbunge wa Igunga anayemaliza muda wake, Nicholaus Ngassa amechukua fomu ya kuwania tena ubunge katika jimbo hilo.

Ngassa amechukua na kuirejesha leo Jumapili Juni 29, 2025 kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Igunga, Ebeneza Mainoya.

Wakati huohuo, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Deomkrasia na Maendeleo (Chadema), Salome Makamba, amekwenda ofisi za CCM Mkoa wa Shinyanga kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya CCM ili kugombea nafasi ya ubunge wa viti maalumu kwa wanawake kupitia UWT.