Prime
Mshikemshike uchukuaji fomu CCM

Dar es Salaam/Mikoani. Mshikemshke wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania uteuzi wa nafasi za udiwani, ubunge na uwakilishi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) umeanza rasmi leo, Juni 28, 2025, na kuvutia makada wengi kuwania nafasi hizo.
Miongoni mwa waliovutia macho ya wengi ni Ester Bulaya, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chadema, ambaye sasa amerejea CCM na kutangaza nia ya kugombea ubunge wa Bunda Mjini.
Bulaya ni miongoni mwa wabunge 19 wa Viti Maalumu kutoka Chadema, ambao hata hivyo uteuzi wao haukutambuliwa na chama hicho.

Hekaheka hizo pia zimewakutanisha wanasiasa wakongwe waliowahi kushika nyadhifa za juu serikalini, wakiwemo mawaziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Ezekiel Maige, ambao kwa sasa wanajitosa tena kwenye kinyang’anyiro cha ubunge kupitia tiketi ya CCM.
Shughuli hiyo imeanza leo baada ya jana Juni 27, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 kutoa nafasi kwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Mchakato wa uchukuaji na urejeshaji utakamilika Julai 2, kabla ya kwenda hatua nyingine za vikao vya mchujo na kura za maoni.
Katika siku ya kwanza leo imeshuhudiwa makada kutoka fani tofauti wakichukua fomu wakiwamo wafanyabiashara, waliokuwa watumishi wa Serikali, wanamichezo, waandishi wa habari na wanachama wa kawaida wa CCM, wakiwemo waliojitosa katika kinyang’anyiro hicho mwaka 2020.
Uchukuaji fomu kwa nafasi ya ubunge unafanyika kwenye ofisi za CCM za wilaya, za udiwani kwenye kata, huku za viti maalumu zikipatikana katika ofisi ya jumuiya za chama hicho. Gharama za fomu ya ubunge ni Sh500,000 na zile za udiwani ni Sh50,000.
Uchukuaji huo wa fomu umekuwa wa kimya kimya baada ya CCM kupiga marufuku mhusika kualika kundi la wapambe kumsindikiza kwenda kuchukua fomu kuomba kuteuliwa.
Vilevile chama hicho kimepiga marufuku mwanachama kuandaa msafara wa magari, pikipiki, baiskeli, ngoma na matarumbeta ya kumsindikiza kwenda kuchukua fomu, kikisema vitendo hivyo vinaleta viashiria vya makundi na mpasuko ndani ya chama na havipaswi kufanyika.
Kuhusu Bulaya
Bulaya aliwahi kuwa mbunge wa viti maalumu (CCM) mwaka 2010 hadi 2015 kabla ya mwaka 2015 kuhamia Chadema ambako aliwania ubunge wa Bunda Mjini na kumshinda mwanasiasa mkongwe Stephen Wasira.
Baada ya kumaliza miaka mitano, Novemba 2020 akiwa na wenzake 18 akiwamo Halima Mdee, aliyekuwa mbunge wa Kawe, waliingia kwenye mgogoro na Chadema baada ya kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu pasipo kuruhusiwa na chama hicho kikuu cha upinzani, lakini wametumikia ubunge huo hadi shughuli za Bunge zilipohitimishwa na Rais Samia Juni 27.
Tayari baadhi ya wabunge katika kundi hilo wametangaza kwenda vyama mbalimbali, wengi wao wakiungana naye CCM, baadhi wakiwania ubunge wa majimbo na viti maalumu.
Hata hivyo, mwenzao, Naghenjwa Kaboyoka, mbunge wa zamani wa Same Mashariki, amejiunga na ACT Wazalendo leo, akiashiria mabadiliko ya mikakati ya kisiasa kuelekea Oktoba.
Geita
Katika ofisi za CCM wilayani Geita, aliyejitosa kuwania ubunge mwaka 2020, Kulwa Biteko, pacha wa Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko amejitokeza tena safari hii akiomba utezi wa chama hicho katika jimbo jipya la Katoro.
Amekabidhiwa fomu na Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Michael Msuya. Kulwa mwaka 2020 aliomba ridhaa kugombea Jimbo la Busanda akaongoza katika kura ya maoni kwa kura 665, lakini jina lake halikurudi katika hatua za juu za uteuzi.
Mwingine ni Ester James, mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kata ya Nyanchiluluma aliyechukua fomu akiomba ridhaa ya kugombea jimbo la Katoro.
Katika Jimbo la Geita Mjini, ambalo linatajwa kuwa na ushindani mkubwa, Manjale Magambo, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Geita amechukua fomu kuwania ubunge.
Magambo aligombea jimboni humo mwaka 2020 akashika nafasi ya pili nyuma ya Costantine Kanyasu, ambaye ameongoza jimbo hilo kwa miaka 10 mfululizo.
Aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel pia amechukua fomu kuwania nafasi hiyo Geita Mjini.
Chacha Wambura maarufu Waja, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na mfanyabiashara maarufu mjini Geita amechukua fomu kuwajimbo hilo, vivyo hivyo kwa Gervas Nyororo, mkazi wa Geita, akiutaka ubunge wa Geita Mjini, ikiwa ni mara ya pili baada ya kujitosa mwaka 2020 lakini kura hazikutosha.
Jimbo la Busanda waliochukua fomu ni Mathias Sangijo na Evarist Gervas, mchimbaji wa dhahabu na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, anayeingia katika kinyang'anyiro hicho kwa mara ya kwanza.
Mtoto wa Rais wa awamu ya Tano, Hayati John Magufuli, Jesca Magufuli amechukua fomu ya kugombea ubunge viti Maalum kupitia Umoja wa Vijana wa UVCCM.

Kigoma
Mwanahabari mwandamizi, Baruan Muhuza amechukua fomu kuomba ridhaa ya CCM kugombea ubunge Kigoma Mjini.
Muhuza anawania nafasi hiyo kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo mwaka 2020 na kushindwa na Kirumbe Ng'enda, mbunge anayemaliza muda wake.
Chongolo aibukia Njombe
Mkoani Njombe, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe na Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Daniel Chongolo amechukua fomu ya ubunge jimbo la Makambako.

Chongolo alikabidhiwa fomu na Katibu wa CCM Wilaya ya Njombe, Mariam Kireti.
Mbunge wa Lupembe anayemaliza muda wake, Edwin Swale amechukua fomu kutetea nafasi hiyo.
Mwingine anayewania jimbo la Lupembe ni Alois Mwenda, ambaye ni ofisa mipango miji mwandamizi wilayani Chato. Pia wamo Beno Nyato, Gilleard Ngewe, Alatanga Nyagawa, Shauku Kihombo na Gaston Kaduma.
Kwa jimbo la Ludewa, mbunge anayemaliza muda wake, Joseph Kamonga amekabidhiwa fomu na Katibu wa CCM Wilaya ya Ludewa, Alfred Mwambeleko ili kutetea nafasi hiyo.
Wengine waliochukua fomu katika jimbo hilo ni Zephani Chaula, Markion Ndofi na Anumie Mweve.
Msigwa ajitosa Iringa
Mbio za ubunge Iringa Mjini zimezidi kupamba moto baada ya Mchungaji Peter Msigwa aliyejiengua Chadema kuungana na Fadhili Ngajilo na Edward Chengula kuchukua fomu.
Mchungaji Msigwa aliwahi kuwa Mbunge wa Iringa Mjini kwa vipindi viwili kupitia Chadema (2010- 2015 na 2015- 2020) kabla ya kujiunga na CCM. Chengula aliwahi kuwania ubunge mara mbili 2015 na 2020 lakini kura hazikutosha.
Katika hatua nyingine, Mwanahabari Tumain Msowoya yeye amechukua fomu kuwania ubunge wa Viti Maalumu kupitia Mkoa wa Iringa.
Mbeya
Mkoani Mbeya, hadi saa 9:45 alasiri ya Juni 28, makada 24 wamechukua fomu kutia nia kugombea ubunge na udiwani.
Mbeya Mjini waliochukua fomu ni Anfrey Nsomba aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya Mjini, Charles Mwakipesile ambaye ni mwandishi wa habari, mwanasheria na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa. Wengine ni Dk Mabula Mahande, Ayoub Mwanjala na Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Dk Stephen Mwakajumilo.
Jimbo jipya la Uyole waliochukua ni Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson na Emir Sanga, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Kata ya Nsalaga.

Jimbo la Mbarali waliochukua ni mbunge wa sasa, Bahati Ndingo, huku Chunya akichukua mhadhiri na mchimbaji madini, Geoffrey Mwankenja anayewania kuchuana na mbunge anayemaliza muda wake, Masache Kasaka.
Jimbo la Rungwe, waliochukua ni Raulence Mwakalibure, Mathias Kabasa, Richard Kasesela na Ezekiel Gwantegile, ambaye ni mtumishi Ofisi ya Makamu wa Rais, huku Busokelo waliochukua ni Lutengano Mwalemba, Thobias Andengenye, Gerard Mwakyonde na Lucas Mwamafupa.
Makonda rasmi Arusha
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amechukua fomu kugombea Arusha Mjini rasmi sasa kuvaana na Mrisho Gambo anayemaliza muda wake.

Vilevile, wanane wamejitokeza kuwania ubunge wa Viti Maalumu mkoa huo, wakiwamo wanaomaliza muda wao Catherine Magige na Zaytun Swai.
Manyara
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo amechukua fomu kuwania tena ubunge Babati Vijijini.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo (kulia) akikabidhiwa fomu ya kugombea ubunge wa Babati vijijini mkoani Manyara na Katibu wa CCM Wilaya hiyo Aziza Isimbula. Picha na Joseph Lyimo
Jimbo la Simanjiro wamejitokeza Lenganasa Soipey, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer, Mwajuma Ally, Prisca Msuya na Lekoko Ngitiri.
Kwa upande wa viti maalumu Mkoa wa Manyara, Regina Ndege amechukua fomu kutetea nafasi hiyo.
Mwenyekiti Wazazi Babati Mjini, Emmanuel Khambay anaomba ridhaa kugombea ubunge Babati Mjini.
Jimboni Kiteto, Sisca Seuta amejitokeza kuwania ubunge huku Peter Nyalandu akijitokeza Hanang.
Kilimanjaro
Mkoani Kilimanjaro wamejitosa Enock Koola kwa jimbo la Vunjo, ambako mwaka 2020 aliongoza katika kura ya maoni kwa kura 187 dhidi ya Dk Charles Kimei aliyeteuliwa akiwa na kura 178.
Ibrahim Shayo amechukua fomu kuwania ubunge Moshi Mjini ambako mwaka 2020 aliongoza kura ya maoni kwa kupata kura 140 dhidi ya Priscus Tarimo aliyepata kura 137.
Wengine waliochukua fomu jimbo la Vunjo ni Yuvenal Shirima, Diddas Lyamuya, Obrey Silayo na Lucy Mrema.
Waliochukua faomu kuomba jimbo la Moshi Vijijini ni Deogratius Mushi, Abdon Mallya, Nicodemus Masao na Gloria Mushi.
Jimbo la Same Mashariki waliochukua ni Miriam Mjema na mbunge anayemaliza muda wake, Anne Kilango Malecela. Same Magharibi waliochukua ni Dk David Mathayo anayetetea nafasi hiyo, Yusto Mapande na Profesa Ladslaus Mnyone.
Dodoma
Katika jimbo la Kongwa makada wanane wamejitokeza kuwania uteuzi wa CCM, akiwemo Spika wa zamani, Job Ndugai aliyehudumu tangu mwaka 2000 alipolichukua kutoka kwa Gidion Senyagwa.
Pamoja na Ndugai yupo Deus Seif, katibu mkuu wa zamani wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Philip Chiwanga, Aloyce Mbujilo, Henry Mwatwiza, Elias Mdao, Dk Simon Ngatunga na Sehewa Sabugo.
Katika Jimbo la Dodoma Mjini, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dodoma, Abdulhabib Mwanyemba amechukua fomu.
Singida
Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amejitosa kuwania ubunge Jimbo la Ilongero baada ya kukaa pembeni kwa muda, akijishughulisha na masuala mengine ya kijamii.
Nyalandu aliyewahi pia kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, alijuzulu ubunge mwaka 2017 akiitumikia nafasi hiyo tangu mwaka 2000, alijiunga na Chadema ambako aliomba kuwania urais lakini akashindwa na Tundu Lissu, kabla ya kurejea tena CCM Aprili, 2021.
Dar es Salaam
Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said amechukua fomu kuomba ridhaa ya CCM ubunge Kigamboni wakati Mwenyekiti wa Uchumi, Uwezeshaji na Fedha wa Kamati ya UVCCM, Maria Sebastian akichukua fomu kuwania ubunge Kawe.
Wengine waliochukua fomu jimboni humo ni Furaha Dominic, John Mwita, Hemedy Nkunya na Gaston Francis.
Mwanahabari, Angel Akilimali amechukua fomu kuwania ubunge jimbo jipya la Kivule huku Mbunge wa Ukonga anayemaliza muda wake, Jerry Silaa akichukua fomu kuwania muhula wa pili Ukonga.
Kadogosa aibukia Bariadi
Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amejitosa kuwania ubunge Bariadi Vijijini, ambalo ni miongoni mwa majimbo ya uchaguzi mkoani Simiyu linalotarajiwa kuwa na ushindani mkali kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.

Pwani
Kwenye Jimbo la Kibaha Mjini waliochukua fomu ni mfanyabiashara Hamza Shomari, James Deogratius na Fadhiri Hezekiah.
Shinyanga
Huko Shinyanga aliyekuwa mbunge wa Msalala kwa takribani miaka 15 kuanzia 2005 hadi 2020, ambaye pia amewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige amejitosa kuwania ubunge jimboni humo.
Katika kura ya maoni ndani ya CCM mwaka 2020 Maige alishindwa na nafasi hiyo kuchukuliwa na Idi Kassim, anayetetea kiti hicho cha ubunge. Salum Ismail alichukua fomu katika jimbo la Kahama Mjini.
Jimbo la Msalala limekuwa likikabiliwa na vurugu za kisiasa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko aliwahi kuonya hali hiyo kwenye mkutano mkuu maalumu wa CCM jimbo Februari 25, 2025, akiwataka makada kuondoa migogoro iliyopo ndani ya chama hicho ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Mwanza
Mkoani Mwanza, mbunge anayemaliza muda wake Ilemela, Dk Angeline Mabula amechukua fomu kutetea nafasi hiyo. Wengine waliochukua ni Leonard Qwihaya maarufu Manguzo, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).
Wawili hao wamekabidhiwa fomu na Katibu wa CCM Wilaya ya Ilemela, Hassan Millanga katika ofisi ya wilaya hiyo.
Kujitokeza kwa Qwihaya kunatarajiwa kuleta ushindani Ilemela, ambalo limekuwa chini ya Dk Mabula tangu mwaka 2015.
Dk Mabula amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, ikiwemo Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi baadaye akawa waziri kamili wa wizara hiyo, nafasi aliyohudumu kuanzia mwaka 2021 hadi Agosti 2023.
Watia nia wengine ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT) Taifa, Khadija Liganga 'Dida' anayewakilisha Mkoa wa Mwanza, na Halima Nassor ambaye ni kada wa CCM ambao wamechukua fomu za viti maalumu.
Aliyewahi kuwa Katibu wa Rais na Mnukulu, Ngusa Samike amechukuwa fomu kuwania ubunge Sengerema. Wengine waliochukua fomu ni Dk Omari Sukari na Mateso Tangazo ambaye anawani jimbo la Buchosa.
Kagera
Waliojitosa ni Johnston Mutasingwa ambaye amechukua fomu kuwania ubunge Bukoba Mjini, Amiry Hamza, Alex Muganyizi, Geofrey Benjamin na Almasoud Karumuna.
Zanzibar
Katika mchakato wa uchukuaji fomu kuwania uwakilishi, ubunge na udiwani sura mpya zimechomoza hasa vijana kuanzia umri wa miaka 35.
Akizungumza na Mwananchi katika ofisi za CCM Wilaya ya Mjini, Katibu wa chama hicho wilayani humo, Bilal Hussein Maulid amesema hadi saa 9:00 alasiri Juni 28, katika ngazi ya ubunge na uwakilishi makada 45 walikuwa wamechukua fomu, huku kwa nafasi ya udiwani waliochukua ni zaidi ya 60.
"Wengi kati ya hawa ni vijana, hii inaashiria nguvu kazi ya vijana inataka kufanya kazi kubwa ya kimaendeleo," amesema.
Omar Suleiman Mohammed, maarufu Mchumi amechukua fomu ya ubunge Kwahani na Ibrahim Hassan Khatib uwakilishi wa Kwahani.
Suad Shaib Ahmada anawania uwakilishi Kikwajuni, huku Waheed Muhammad Ibrahim Sanya, ambaye ni Mkurugenzi wa Hazina Zanzibar, akiwania pia nafasi hiyo Kikwajuni.