Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nderemo na vifijo vyatawala Samia akilifunga Bunge

Dodoma. Ni hotuba iliyosheheni utekelezaji wa sekta mbalimbali. Ndivyo unavyoweza kusema kuhusu hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 ambalo litavunjwa rasmi Agosti 3, 2025.

Hotuba ya Rais Samia ya jumla ya saa 2 na dakika 47 ndani ya ukumbi wa Bunge ilikuwa ikikatishwa mara nyingi kwa makofi ya wabunge hata wakati mwingine alilazimika kuwaomba wanyamaze.

Wabunge walipiga meza kwa nguvu kuonesha kuunga mkono, huku wengine wakiimba kwa sauti, “Tuna imani na Samia,” hasa alipokuwa akieleza kwa kina hatua zilizochukuliwa na Serikali yake katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Rais Samia alipogusa kuhusu kukua kwa uchumi kwa Tanzania kufikia uchumi wa kati wa juu ifikapo 2030, Mbunge wa Viti Maalumu, Jacqueline Ngonyani alianzisha wimbo wa 'Tunaimani na Samia huku Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka akiongoza wabunge kusimama na wengine wote wakafuatia na kuanza kupiga makofi.

Rais Samia ndani ya hotuba yake amemtaja Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalumu, George Mkuchika kuwa ndiye alitangaza kung'atuka ambapo (Mkuchika) alisimama na kuwapungia mikono wenzake kwa ishara ya kuwaaga.

Mbali na Mkuchika kutangaza kung’atuka ubunge, wabunge wengine hakuna aliyenukuliwa au kusikika akisema anang’atuka ubunge, ikiwa na maana waliosalia wote wanakwenda kugombea.


Utulivu bungeni

Hali ya utulivu ilitawala nje ya ukumbi wa Bunge, huku ulinzi ukiimarishwa kwa karibu wakati Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa akiwasilisha hotuba yake ya mwisho Ijumaa, Juni 27, 2025, kufunga rasmi Bunge la 12 kabla ya kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

Milango yote ya kuingia ndani ya Bunge, maeneo ya ndani ya ukumbi na mgahawa maalumu ambapo wabunge hupumzika, yalikuwa na utulivu kamili.

Maegesho ya magari yalihamishiwa maeneo salama yenye ulinzi mkali wa askari wenye silaha.

Ghorofa ya jengo la kitengo cha habari, lililokuwa zamani Hoteli ya Fifty Six, ilishikiliwa kwa zamu na askari waliovalia silaha.

Milango kwa wageni ilifungwa saa 8:30 mchana na eneo la waandishi lilitumiwa na walinzi wa viongozi, hivyo waandishi waliwekwa katika sehemu maalumu pamoja na wageni wengine.


Kuwasili bungeni

Rais Samia aliwasili kwenye viunga vya Bunge saa 10.50 jioni jana ambapo uliimbwa wimbo wa Taifa na Afrika Mashariki, huku akiwa amesimama kwenye jukwaa maalumu aliloandaliwa.

Baada ya wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki, Rais alikagua gwaride maalumu lililoandaliwa na Jeshi la Polisi kabla ya kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge saa 11.10 jioni akiongozwa na Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson.

Kabla ya kufika viwanja vya Bunge, msafara wa kwanza kuingia  ukumbini ulikuwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Zubeir Ali Maulid na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Joseph Ntakirutimana wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge, Nagma Giga.

Msafara wa pili ulikuwa wa Jaji Mkuu wa Tanzania,  George Masaju uliongozwa na Mwenyekiti wa Bunge, Deodatus Mwanyika na kisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla na Mwenyekiti wa Bunge Dk Joseph Mhagama.

Ulifuata msafara uliokuwa wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi aliyewasili viwanja vya Bunge saa 9.00, lakini ndani aliongozwa na Naibu Spika wa Bunge, Musa Zungu.

Ndani ya ukumbi Dk Tulia alianza kwa dua kisha akatoa utaratibu utakavyokuwa wakati wakimsubiri Rais Samia.

“Jana tulitengua kanuni zetu za Bunge kuwawezesha wageni wetu kuingia humu ndani, kwa muktadha huo nitasitisha shughuli za Bunge kwa muda ili niruhusu wageni wetu waweze kuingia bungeni,” alisema Dk Tulia.

Wakati hayo yakifanyika mpambe wa Bunge aliondoa siwa mezani na kuliweka katika droo iliyopo ndani ya meza kubwa mahali linapowekwa siku zote.

Tukio lingine lilikuwa ni taarifa ya kuwatoa hofu wabunge waliokata tiketi za treni zitakazoondoka Dodoma kuanzia saa 11.00 hadi 12.00 jioni jana.

Mtoa taarifa alisema, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Machibya Masanja ametaka tiketi za wabunge hao ili wabadilishiwe muda ambapo itakuwa ni zaidi ya saa 1.00 jioni.