Rais Samia ataja kiwango cha fedha zilizonaswa utoaji rushwa

Muktasari:
- Amesema Tanzania ni nchi ya pili kwa Afrika Mashariki kwa mapamabano dhidi ya rushwa na ni nchi ya 14 kwa Afrika katika mapambano hayo.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema rushwa ni adui wa haki na kikwazo kikubwa cha maendeleo, hata hivyo Serikali imeimarisha mapambano dhidi ya rushwa na kufanikisha kuokolewa Sh211.9 bilioni.
Amesema juhudi hizo zimeiwezesha Tanzania kushika nafasi ya pili katika ukanda wa Afrika Mashariki na nafasi ya 14 kwa nchi za Afrika kwenye mapambano dhidi ya rushwa.
Taarifa hizo za Rais Samia kuhusu uwezo wa Tanzania kupambana na rushwa ni kwa mujibu wa taasisi ya kimataifa ya Transparency Inernational ya mwaka 2024.
Mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo leo Juni 27,2025 wakati akihutubia Bunge jijini Dodoma ikiwa ni hatua ya kulivunja Bunge hilo la 12 kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
“Katika kipindi hiki, tumefanikiwa kuokoa Sh211.9 bilioni na kurejesha serikalini kupitia operesheni mbalimbali za rushwa, mali zenye thamani ya Sh35.688 bilioni ikijumuisha nyumba viwanja na magari na fedha taslimu zimetaifishwa,” amesema.
Katika jitihada hizo, Rais Samia ametoa rai kwa Watanzania kuendelea kutoa ushirikiano katika pambano dhidi ya rushwa.
Kuhusu Serikali kutimiza wajibu wake kwa mhimili wa kutunga sheria katika Bunge la 12, Rais Samia amesema jumla ya miswada 60 imepitishwa na mazimio 922 na Serikali kutoa taarifa 15 kupitia kauli za mawaziri bungeni wakitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali bungeni.
Kiongozi huyo akizungumzia utoaji wa fedha za majimbo, amesema Serikali imeongeza fedha za jimbo kutoka Sh11 bilioni kwa mwaka 2021/2022 hadi kufikia Sh15.9 bilioni kuanzia mwaka 2020/2023.
“Lengo ni kurahisisha utendaji wenu majimboni na kuchochea maendeleo ni matumaini yangu kwamba fedha hizi mmezitumia vyema katika kuwaletea wananchi maendeleo vinginevyo wakati ni sasa,” amesema.