Prime
UCHAMBUZI WA DANIEL MJEMA: Msichafuane ili kuongoza kura za maoni wala msichukue fomu kuuza sura

Muktasari:
- Vyama vya siasa mtafanya kosa kubwa sana endapo mtawateua waliochukua fomu za ubunge kufanya mzaha na kushusha hadhi ya mhimili wa Bunge, yaani kuna watu wanachukua fomu kama vile maigizo hadi jamii inajiuliza “hata huyu”?
Kura ya turufu huwa inaweza kuzuia baadhi ya maamuzi yasitekelezwe, na hiki ndicho baadhi ya watia nia wa nafasi za ubunge na udiwani ama mawakala wao, wanatumia kuwapaka wenzao matope wakidhani ndio kete ya kuwasafishia njia.
Lakini hatuhitaji watia nia ambao wanachukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwa mbunge kwa kuongeza tu wasifu wake (CV), kuuza sura au ili aingie tu kwenye orodha ili Rais akiangalia watu wa kuwateua, basi naye jina lake lichomoze.
Vyama vya siasa mtafanya kosa kubwa sana endapo mtawateua waliochukua fomu za ubunge kufanya mzaha na kushusha hadhi ya mhimili wa Bunge, yaani kuna watu wanachukua fomu kama vile maigizo hadi jamii inajiuliza “hata huyu”?
Kwa muktadha wa uchambuzi huu, nawalenga baadhi ya makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliopo hatua za mwanzo kabisa za uchukuaji na urejeshaji wa fomu, kwamba ni ushamba kumchafua mwenzako ili uonekane wewe ni bora.
Japo wengi wanawatambulisha kama wagombea, kwangu mimi nawachukulia kama watu wanaoomba kuteuliwa na CCM kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na Madiwani 2025, bado si wagombea.
Veto au Turufu ni chombo chenye nguvu kinachotumiwa na watu fulani au mashirika fulani, mara nyingi katika nyadhifa za mamlaka, kuzuia au kukataa uamuzi fulani na hii kuna wakati unatumika katika Baraza la Umoja wa Mataifa.
Sasa kuna ndugu zetu ambao wameamua kufanya vitendo ambavyo vinalenga kuwachafua wagombea wenzao ama kupitia mitandao ya kijamii au kusambaza uongo ili kupotosha kwa makusudi, sifa za wagombea wengine anaoshindana nao.
Kanuni za Uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya Dola toleo la 2021 zinakataza matumizi ya mabango, vipeperushi, kampeni chafu, vurugu za wapiga debe, matusi na upotoshaji wa sifa za wagombea wengine wanaoshindana nao.
Ukisoma kanuni ya 25(3) ya Kanuni hizo, inasema ni mwiko kwa mgombea yeyote kufanya kampeni za kupakana matope au aina nyingine yoyote ile dhidi ya mgombea mwingine, na atakayethibitika kuyafanya hayo hatateuliwa kugombea.
Nataka niwaambie ndugu zangu hawa, wasijisahaulishe kuwa kanuni ya 18(1)(a) na (b) imeeleza kutakuwa na nyakati mbili za kuwasilisha na kushughulikia malalamiko nazo ni kabla, wakati na baada ya kura za maoni na hata uteuzi.
Lakini nawakumbusha pia Kanuni ya 14(2)(f) kuna angalizo linalosema “Katika kura hizi za maoni hakuna mshindi kwani haya ni maoni tu ili kuvisaidia vikao vya uchujaji na uteuzi wa mwisho, hivyo msitukane ukunga wakati uzazi ungalipo.
Hata katika viti maalum, kanuni inawataka walioshiriki kura za maoni kutambua kura zilizopigwa na nafasi aliyopata mgombea katika kundi lake ni mapendekezo tu ya vikao vilivyopiga kura, ili kukisaidia kikao cha uteuzi wa mwisho.
Hili mbona lina mifano halisi? Uchaguzi mkuu wa 2020 wako makada wa CCM walishinda kwa kishindo kura za maoni lakini majina yao hayakurudi. Wala msijipe matumaini kwa vile yanarudi majina matatu, hata hayo unaweza usiwemo.
Msifikiri chama hakina macho, kinaona na kusikia yanayoendelea huko majimboni na kwenye kata licha ya kwamba baadhi yenu hamjarejesha fomu, lakini yanayoendelea kwa baadhi yenu yanavifikia vyombo vya usalama na Dola.
Ninafahamu na pengine hata baadhi ya makada mnafahamu, kwamba wako baadhi ya watia nia wanaoomba kuteuliwa kugombea ubunge, ambao wameunda makundi ya vijana wanaotumia mitandao ya kijamii kutukana watia nia wenzao.
Japo inawezekana wanajiweka kando na makundi hayo ya Whatsapp yanayokashifu watia nia wenzao, lakini ukweli ni kuwa ukifuatilia walioko nyuma ya vijana hao, unaona kabisa mkono au kivuli cha makada hao watia nia.
Wapo wanaozusha tuhuma za uongo za baadhi ya watia nia kujihusisha na vitendo vya rushwa, ugawaji wa maduveti, khanga, vitenge au sare za CCM, lakini wapo ambao ni kweli wanafanya matendo hayo yanayokiuka kanuni.
Ninaowalenga ni hilo kundi linalotumia vibaya mitandao ya kijamii kuchafua wenzao kwa kuwazushia tuhuma za uongo wakidhani kwa kufanya hivyo wanawachafua na kuwashushia heshima na kukubalika kwao kwa wapiga kura.
Chama Cha Mapinduzi kinatafuta wagombea bora, wanaokubalika na waadilifu watakaowatumikia watanzania kwa kutanguliza maslahi ya taifa mbele na hakitafuti wagombea wasio na sifa na wenye dhamira ya kujinufaisha.
Waswahili wana usemi chema chajiuza na kibaya chajitembeza ikimaanisha mambo mazuri huwa yanajitangaza yenyewe, wakati mambo mabaya yanahitaji juhudi za ziada ili kutambuliwa, ninaamini wajumbe mnanielewa katika hili.
Msiache kumchagua mtia nia aliye bora kwa sababu tu ya chuki binafsi au kwa sababu ya tofauti za imani ya dini ama kabila lake, tuleteeni wagombea watakaokiheshimisha CCM ndani na nje ya Bunge na Baraza la Madiwani.
Ninawasihi sana wajumbe, chondechonde, epukeni kufananishwa na Karai la Zege, ambalo thamani yake huonekana wakati wa ujenzi tu, kazi ya ujenzi ikimalizika linawekwa nyuma ya nyumba likisubiri ujenzi mwingine ujao.
Kura yenu ina thamani kubwa sana kwa watanzania, msichague mtia nia kwa kutizama pesa yake, sura yake au wadhifa wake, bali angalieni mwenye sifa za kuwa kiongozi bora, ili awe bora pia atakaposhindanishwa na wa upinzani.
Tukipata wagombea bora kutoka CCM na vyama vya upinzani navyo vikaleta wagombea walio bora kuanzia nafasi ya urais, ubunge na udiwani, mtakuwa mmewapa watanzania wenye sifa ya kupiga kura, wigo mpana wa kuchagua.
Msituletee wagombea ambao wanaunga mkono sera ambazo zinaenda kinyume na maslahi ya wapiga kura au maslahi ya taifa au wagombea ambao watashindwa kuwasilisha au kutetea kwa dhati hoja zinazotokana na kero za wapiga kura wake.
Tunahitaji mbunge mwenye weledi na mwenye uwezo wa kuchambua hoja na kuisimamia na kuishauri Serikali, kwa hiyo kwa wale wabunge waliomaliza na wanaotetea viti vyao, wapimeni kwa ufanisi waliouonyesha bungeni.
Ni kweli Katiba yetu inasema sifa ya kuwa Mbunge au Diwani ni kujua kusoma na kuandika lugha ya Kiingereza ama Kiswahili, lakini tutumie busara na hekima tukitambua wajibu mkubwa wa Bunge letu ili kuleta wagombea wenye sifa.
Mimi ninaamini wakati Katiba hii ya mwaka 1977 ikitungwa na ikaweka sifa ya kuja kusoma na kuandika, tulikuwa na chuo kikuu kimoja au viwili, shule za sekondari zilikuwa ni za kuhesabu, lakini sidhani ni kigezo sahihi kwa zama hizi.
CCM kama chama kiongozi kina wajibu wa kuonyesha njia ya aina ya wabunge na madiwani ambao zama za sasa zinawahitaji, na sio wale ambao muswada wa sheria unapitishwa, ukileta kelele mitaani anasema hakujua anapitisha nini.
Vyombo vya mchujo tunaomba timizeni majukumu yenu kwa weledi, uadilifu na bila kumuonea au kumpendelea mtu, wale wanaofanya kampeni chafu hata kama wataongoza kura za maoni, majina yao yasirudi miongoni mwa wale watatu.
Lakini wale wanaochukua fomu kuuza sura au kuongeza CV zao basi wajumbe shughulikeni nao, tunahitaji wagombea watakaoheshimisha bunge letu au mabaraza ya madiwani, na msiimpe kazi kutafuta nani amteue kuwa waziri.
Tusichukue fomu kama bendera fuata upepo, jipime kama una sifa na natamani uchaguzi mkuu 2025 urejeshe heshima ya bunge kama lile la tisa na 10.
0656600900