Operesheni za Polisi zanasa 200 kwa tuhuma za uhalifu Tanga
Pikipiki mbalimbali zilizokamatwa ambazo watuhumiwa walikuwa wakizitumia kwenye wizi katika Mkoa wa Tanga. Picha na Mbonea Herman
Muktasari:
- Oparesheni hiyo imefanyika kati ya Juni 1 na Julai 16, 2026 katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tanga.
Tanga. Watu 200 wamekamatwa katika operesheni maalumu zilizofanywa na Jeshi la Polisi mkoani Tanga kati ya Juni 1 na Julai 16, 2026, wakihusishwa na makosa mbalimbali ikiwemo biashara ya dawa za kulevya, wizi, unyang’anyi na uharibifu wa miundombinu ya umma.
Hayo yameelezwa leo, Ijumaa Julai 17, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Muchunguzi.
Amesema watuhumiwa hao walikamatwa katika doria na operesheni zilizoendeshwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Amesema baada ya uchunguzi kukamilika, kesi 51 zilifikishwa mahakamani na baadhi ya watuhumiwa walitiwa hatiani.
Katika operesheni za kupambana na dawa za kulevya, amesema walikamata watuhumiwa 29. Kati yao, 14 walikutwa na mafungu 750 ya mirungi yenye uzito wa kilogramu 45.
Aidha, amesema watuhumiwa wengine 15 walikamatwa wakiwa na bangi, ikiwemo misokoto 114, pakiti 126, vifurushi vitano na vipande 120 vilivyobanwa.
Muchunguzi, amesema polisi pia walikamata pikipiki 20 zisizosajiliwa wakati wa operesheni hizo.
“Operesheni na doria zinazoendelea zimechangia kwa kiasi kikubwa kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa wa makosa mbalimbali pamoja na kuokoa vielelezo muhimu vya uhalifu,” amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi akizungumza na waandishi wa habari juu ya operesheni mbalimbali walizozifanya kwa ajili ya kukabiliana na uhalifu katika Mkoa wa Tanga.
Katika hatua nyingine, amesema watuhumiwa watano walikamatwa wakiwa na nyara za Serikali na vielelezo vinavyohusiana na wanyamapori.
Pia, polisi walipata vifaa vya miundombinu vinavyodhaniwa kuibwa kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na mamlaka za barabara, noti bandia za Kenya, televisheni 10, simu za mkononi 25 pamoja na mali nyingine zinazoshukiwa kuwa za wizi.
Kuhusu usalama barabarani, Kamanda huyo amesema madereva 10,028 walibainika kukiuka sheria za usalama barabarani katika kipindi hicho.
Amesema madereva tisa walifungiwa leseni zao kwa muda baada ya kufanya makosa makubwa, yakiwemo kuendesha kwa mwendo kasi na vitendo vingine vilivyohatarisha usalama wa watumiaji wa barabara.
Muchunguzi, amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu na watu wanaohatarisha usalama wa jamii.
“Tunawaomba wananchi waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za vitendo vinavyohatarisha usalama ili kuendelea kulinda amani, usalama na utulivu wa Mkoa wa Tanga,” amesema.
Operesheni hizo, amesema ni sehemu ya juhudi za Jeshi la Polisi za kuimarisha usalama na kudhibiti makosa ya jinai katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tanga.