Prime
Uongozi mpya wa Chadema unavyopita katika tanuri la moto

Muktasari:
- Baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa ndani, Chadema hakijasimama tena kama chama chenye mvuto kwa Watanzania, chama kikuu cha upinzani na kimbilio la wapenda demokrasia kutokana na kuwa na sera mbadala zinazolenga kuikomboa jamii. Kimekuwa kikikabiliana na migogoro ya ndani na upinzani mkali kutoka nje.
Dar es Salaam. Tangu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilipofanya uchaguzi wake wa ndani na kupata viongozi wapya, Januari 22, 2025, hali haijawa shwari ndani ya chama hicho kutokana na mwendelezo wa makundi.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Januari 21, 2025, Tundu Lissu aliibuka mshindi akimbwaga Freeman Mbowe ambaye amekuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa miaka 20, hivyo akawa mwenyekiti wa nne wa Chadema tangu kuanzishwa kwake mwaka 1992.

Baada ya uchaguzi huo, viongozi na wanachama waligawanyika katika makundi mawili; wale waliomuunga mkono Mbowe na waliomuunga mkono Lissu. Makundi haya yalikuwa na minyukano mikali inayokigharimu chama sasa.
Dalili mbaya zilianza kuonekana wakati wa kampeni za kuwania uenyekiti wa chama hicho ambapo wagombea na wafuasi wao walifanya siasa za kuchafuana, jambo ambalo lilihatarisha umoja wa chama hicho.
Baada ya kukamilika kwa uchaguzi huo, Chadema hakijasimama tena kama chama chenye mvuto kwa Watanzania, chama kikuu cha upinzani na kimbilio la wapenda demokrasia kutokana na kuwa na sera mbadala zinazolenga kuikomboa jamii.
Viongozi wa chama hicho wamekuwa wakikabiliwa na mizozo ya ndani na nje ya chama, jambo ambalo limepunguza kasi ya chama kufanya siasa zake, bali kinashughulikia mizozo na mashambulizi dhidi yake.
‘No reforms, no election’
Kaulimbiu ya Chadema ya ‘No reforms, no election’ (bila mabadiliko hakuna uchaguzi) imeibua mjadala mpana wa wanazuoni, wanachama wa Chadema na wananchi wa kawaida huku Chadema kikikabiliwa na ukosoaji mkubwa kuhusu namna kitakavyotekeleza jambo hilo.

Ajenda hiyo ya Chadema inalenga kushinikiza mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi na kama mabadiliko hayo hayatafanyika, basi chama hicho kitazuia uchaguzi na Lissu alibainisha njia watakazotumia kuwa ni pamoja na kuzungumza na makundi mbalimbali ikiwamo jumuiya ya kimataifa.
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa ni miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa kaulimbiu hiyo ya Chadema huku viongozi wake, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla wakikosoa na kubeza ajenda hiyo.
Katika mikutano yake aliyoifanya katika mikoa mbalimbali aliyotembelea, Wasira amekuwa akieleza kwamba hakuna mtu mwenye uwezo wa kuzuia uchaguzi kufanyika na anahoji mbinu watakazotumia Chadema kuzuia uchaguzi.
Makalla, katika mikutano yake, amekuwa akieleza kwamba Chadema kisiposhiriki uchaguzi kitapotea na huo utakuwa mwisho wao kama chama kikuu cha upinzani. Amekuwa akisisitiza kwamba uchaguzi ni jambo la kikatiba, hivyo hakuna mwenye uwezo wa kuzuia usifanyike.
Kutokana na ajenda hiyo ya kushinikiza mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi, chama hicho kimeingia katika mgogoro na vyombo vya dola ambapo baadhi ya mikutano yao ya hadhara imekuwa ikizuiliwa na vyombo vya dola kwa hofu ya uvunjifu wa amani.
Kuibuka kwa Mchome
Katika hali isiyo ya kawaida, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mwanga, Lembrus Mchome aliibuka na hoja ya kwamba uteuzi wa wajumbe wa kamati kuu na sekretarieti, uliofanywa na Lissu, haukuwa halali kwa kuwa akidi ya wajumbe wa halmashauri kuu haikutimia.
Kada huyo wa Chadema alitaka viongozi hao waliothibitishwa na mkutano huo wa halmashauri kuu ambao alidai haukuwa halali, wasitambuliwe, badala yake uitishwe mkutano mwingine wa halmashauri kuu utakaowathibitisha viongozi hao.
Kutokana na kutojibiwa kwa barua yake aliyomwandikia katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, Mchome alifikisha jambo hilo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kupitia barua yake ya Februari 18, 2025, akieleza ubatili wa viongozi walioteuliwa.
Aprili 8, 2025, Mchome aliandika barua nyingine kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, akishinikiza kujibiwa kwa barua yake, ndipo Msajili akakielekeza Chadema kujibu madai ya Mchome ndani ya siku. Mnyika alijitokeza na kueleza kwamba viongozi walioteuliwa ni halali kwa mujibu wa katiba ya chama.
Wakati sakata hilo likiendelea, uongozi wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro ulimwandikia barua Mchome ukimtaka ajieleza ndani ya siku 14 kwanini asichukuliwe hatua za kinidhamu ikiwamo kuondolewa kwenye nafasi yake na pia kuvuliwa uanachama.
Mvutano huo kati ya Mchome na uongozi mpya wa Chadema umekipitisha chama hicho katika nyakati ngumu za kushughulikia masuala yake ya ndani kwa kuhoji mambo yaliyofanyika kuwa ni kinyume na katiba ya chama.
Lissu ashitakiwa kwa uhaini
Katika mwendelezo wa matukio yanayokabiliana na Chadema, mwenyekiti wake, Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025 baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma na baadaye kupelekwa dar es Salaam.
Lissu alishitakiwa na makosa mawili; kuchapisha taarifa za uchochezi mtandaoni na kosa la uhaini linalomfanya akose dhamana. Kesi yake inatarajiwa kusikilizwa tena Mei 19, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Lissu ambaye alikuwa kinara katika ziara zake za kila mkoa kuwaeleza wananchi kuhusu kaulimbiu ya Chadema ya “No reforms, no election”, amewekwa rumande na hivyo kupunguza kasi ya kufikisha ajenda hiyo kwa wananchi ili kukwamisha uchaguzi ujao.
Kushikiliwa kwa mwanasiasa huyo ni pigo jingine kwa Chadema, hasa katika kipindi hiki ambacho chama hicho kinalenga kuzuia uchaguzi kufanyika, yeye akiwa ndiyo kinara katika kusukuma ajenda hiyo.
Hadi sasa hatima yake haijulikani, kesi yake iko mahakamani ikisubiri kusikilizwa tena baada ya mahakama kutupilia mbali maombi ya upande wa mashitaka kutaka kesi hiyo kusikilizwa kwa njia ya mtandao, jaribio ambalo limekwama mara mbili.
G55 waibuka, wahama
Kundi la G55, likihusisha wanachama wa Chadema wanaotaka chama hicho kiende kwenye uchaguzi, liliibuka na kumwandikia barua Katibu Mkuu kuhusu msimamo wao na kumweleza madhara endapo hawatashiriki uchaguzi.
Wanachama hao zaidi ya 200, hawakubaliani na msimamo wa chama, hivyo wanaonekana kuwa ni wasaliti kwa kwenda kinyume na msimamo wa chama. Wanasisitiza kwamba lengo la chama cha siasa ni kushika dola, hivyo hawawezi kufanikiwa katika hilo kama hawatashiriki uchaguzi.
Kundi hilo linaloongozwa na Mrema linadai kwamba mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi yanahitajika, lakini kutoshiriki au kuzuia uchaguzi siyo uamuzi mzuri, hivyo wanashauri washiriki uchaguzi huku wakishinikiza kufanyika kwa mabadiliko hayo.
Katika mwendelezo wa mpasuko ndani ya chama hicho, waliokuwa wajumbe wa sekretarieti ya Chadema; Mrema, Benson Kigaila, Salum Mwalimu, Julius Mwita na Catherine Ruge, wametangaza kukihama chama hicho.

Kuondoka kwa makada hao, kunaendeleza mpasuko ndani ya chama kulikosababishwa na makundi baada ya uchaguzi na huenda wengine wakafuata kwa kujiondoa ndani ya Chadema ikiwa ni mwendelezo wa kudhibitiana ndani ya chama.
Mchambuzi wa siasa, Buberwa Kaiza amesema Buberwa Kaiza amesema kilichopo ndani ya chama hicho sio mgororo, bali ni chama kinajisafisha kwa kuwaondoa wanaopingana na msimamo wa chama.
“Sio tatizo kwasababu wote wanaenda chama kingine (Chaumma) wakaendeleze yale ambayo waliona wangeweza kuifanya ndani ya Chadema na ikashindikana bada ya uchaguzi,” amesema Kaiza.
Amesema mgongano wa kimaslahi ambao umevurugwa ndani ya chadema ndio unaleta mvutano na wengine kuhama huku akisisitiza kuwa haoni mgogoro kwa sababu viongozi ndani ya chama hawazozani.
Kaiza amesema wanaotaka chama hicho kionekane hakijatulia ni wale waliokuwa viongozi utawala uliopita ambao sasa ni wanachama wa kawaida.
Wachambuzi washauri
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Samson Sombi amesema Chadema kina misingi ya kuanzishwa kwake na chama kina sera na kwamba chama huendeshwa kwa vikao na sio matamko.
“Mwenyekiti unapaswa kusimamia sera na misingi ya chama, kila anachofanya mwenyekiti iwe imetokana na uamuzi wa vikao, sasa ni jambo la kawaida uchaguzi wowote unapoisha kunakuwa na makundi.
“Sasa, ili wasonge mbele ni lazima hayo makundi yavunjwe, ili misingi ya chama isimamiwe na Mwenyekiti mpya,” amesema.
Mwalimu Sombi anasema Chadema inapaswa kutangaza ilani yake kwa sasa baada ya kukaa vikao na wanachama wake badala ya kugawanyika kama ilivyo sasa.
“Madai ya Katiba mpya sasa ni ngumu kwa sababu tayari maandalizi ya uchaguzi yamefanyika, kinachohitajika Chadema ni iunganishe watu wake na kufanya yanayowezekana,” amesema.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa na maendeleo, Dk Adan Msafiri amesema si lazima kila wakati chama kinakuwa salama.
Amesema kila kunapopigwa kelele hakumaanishi kwamba kuna vurugu, japo ndani ya Chadema kinachoonekana ni suala la maslahi.
“Mwenyekiti wa chama anapokuwa mwanasheria ni lazima haya yatokee, hakujatulia kwa sababu watu walikuwa na masalahi yao, sasa wanaona yameguswa, katiba ya chadema haijabadilika bali ni watu wamebadilika kutokana na mahitaji yao.
“Kimsingi, lazima tufanye uchambuzi wa kisomi kwa maana kwamba usifikiri watu wanapogombana tatizo ni kiongozi, hapana, yapo mambo mengi,” amesema Msafiri.