Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vigogo Chadema kutua Chaumma

Muktasari:

  • Uamuzi wa makada wa Chadema kutangaza kuhama chama hicho kumeibua mijadala na maswali juu ya wanakoelekea na uhai wa chama hicho. Je, wanahamia wapi SAU, ACT Wazalendo au Chaumma? Viongozi wa vyama hivyo wawazungumzia.

Dar/Moshi. Kujivua uanachama kwa waliokuwa viongozi katika sekretarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakati wa uongozi wa Freeman Mbowe, kumeibua maswali kuhusu uhai wa chama hicho kikuu cha upinzani.

Viongozi watano waliokuwa katika sekretarieti hiyo ya Chadema wakiongozwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu (Bara), Benson Kigaila na Naibu Katibu Mkuu - Zanzibar, Salum Mwalimu, wametangaza uamuzi huo leo Jumatano Mei 7, 2025.

Ingawa hawakusema watahamia chama gani, lakini minong’ono iliyopo inaeleza makada hao, na wengine ambao hawajatajwa, wana mpango wa kuhamia ama ACT-Wazalendo, Sauti ya Umma (SAU) au Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Minong’ono hiyo ambayo haijathibitishwa, inadai yamekuwepo mazungumzo baina yao na ACT Wazalendo na SAU lakini hawakuafikiana kwa baadhi ya masharti waliyokuwa nayo, na kuamua kuangalia uwezekano wa kwenda Chaumma.

Chaumma kinatajwa zaidi na hasa ikizingatiwa kimetangaza kufanyika kwa vikao vyake kuanzia kamati kuu Mei 10-11, 2025 na Mkutano Mkuu Juni 27 na 28, 2025, Dar es Salaam wenye lengo la kupata wagombea wa urais Tanzania na Zanzibar.

Chaumma inayoongozwa na Hashim Rungwe ni miongoni mwa vyama 18 vyenye sifa ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 na vigogo hao waliotangaza kuhama Chadema, wengi wana ndoto za kuwania ubunge, kinyume na msimamo wa chama walichotoka.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa siasa walisema ni vigumu kupima nguvu na ushawishi viongozi hao ndani ya Chadema kwa kuwa kina hatihati ya kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025, lakini nguvu hiyo inaweza kupimwa kule wanapohamia.

“Ni vigumu kupima ukubwa wa athari za kuondoka kwao kwa sababu Chadema inaonekana hakishiriki uchaguzi, ila unaweza kupima nguvu yao huko wanakoenda baada ya matokeo,” alidai mmoja wa wachambuzi.

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa na wachambuzi wanaona Chadema itatetereka kwa kiasi fulani hata kama haitashiriki uchaguzi, kwa kuwa makada hao ndio walikuwa kama injini kwenye uongozi wa Mbowe.

Wataalamu hao katika masuala ya siasa, wanarejea tukio la 1995 wakati Augustino Mrema alipoihama CCM kwenda NCCR-Mageuzi mwaka 1995 na baadaye kwenda TLP mwaka 1999, ambapo vyama alivyohamia vilipata nguvu.

Tukio lingine ni la Machi 2019 wakati aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamadi ana timu yake walipohamia ACT-Wazalendo, kitendo ambacho kiliidhofisha CUF.

Tukio lingine ni wakati Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa alivyokihama CCM mwaka 2015 alipoenguliwa kugombea urais na kujiunga na Chadema dakika za lala salama, na kukipa mafanikio makubwa.

Ni kutokana na historia hiyo, baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema wanaona kuondoka kwa makada hao kunaweza kukitikisa Chadema kutegemea na vyama watakavyohamia na pia namna watakavyotumika kukiidhofisha.


Chaumma, ACT-Wazalendo

Mwananchi limezungumza na viongozi wa Chaumma, SAU na ACT Wazalendo juu kuhusu kinachotajwa kama ujio wa maka hao.

Mwenyekiti wa Chauma, Hashim Rungwe amesema hao ni Watanzania na wana uhuru wao wa kujiunga na chama chochote cha siasa nchini.

Rungwe maarufu Mzee wa Ubwabwa amesema kama wana nia ya kujiunga na Chaumma wanakaribishwa lakini kwa kufuata utaratibu.

“Hata hivyo na mimi nasikia huenda wakaja kuomba kujiunga na chama chetu, ila suala hilo kwa sasa halijanifikia bado, ila kama watakuja basi tutawajadili kwenye mkutano wa wanachama kabla ya kufanya uamuzi wowote," amesema Rungwe.

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu amesema chama hicho hakijafanya mazungumzo na makada hao lakini kama chama makini chenye mlengo wa kufanya mageuzi ya kisiasa, kimeendelea kuweka mazingira bora ya kupata wanasiasa makini.

“Tunahitaji wanasiasa walioko tayari kushirikiana nasi kwenye jukwaa letu kuleta mabadiliko ya kweli kwa Watanzania na ninaamini kwa rekodi yetu hatujawai kushindwa kuwapokea wanasiasa, hata mliona ujio wa wanachama waliokuwa wa CUF,” amesema.

Amesema wapo tayari kushirikiana na mwanasiasa yeyote anayetaka kwenda kujiunga na chama hicho, lakini anahisi makada waliohama Chadema wanakujua wanakoenda na wameshafanya uamuzi.

“ACT-Wazalendo siku zote milango yetu ilikuwa wazi na watu kuhamia kuja kwetu, tunatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha wanafanikiwa, hatujashindana nao, kama ninavyosema tumeweka mazingira rafiki,” amesema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majaliwa Kyara amesema hawajawai kufanya nao mazungumzo yoyote lakini kama wanahitaji kujiunga na chama hicho milango iko wazi.

“Kama wanahitaji kujiunga tunawakaribisha kwa sababu chama chochote kinahitaji wanachama ilimradi wakubali kufuata katiba yetu na maelekezo ya viongozi wetu hayana shida, kikubwa tunahitaji wanachama,”amesema.


Walivyojiondoa Chadema

Kigaila na wenzake wametangaza uamuzi wa kujiondoa Chadema wakitaja sababu mbalimbali ikiwamo madai kuwa chama hicho kimeshindwa kufuata malengo ya kuanzishwa kwake.

Wakiwa wamevalia nguo nyeupe, walioshiriki mkutano huo ni Julius Mwita, John Mrema, Catherine Ruge, ambao wamesema kuna kundi kubwa linawafuata.

Kigaila amesema hali ya kisiasa ndani ya chama hicho imegubikwa na kile alichokiita ‘ubaguzi mkubwa’ dhidi ya wanachama wanaohusishwa na Mbowe, ambao wamekuwa wakitengwa kuanzia ngazi ya kamati kuu hadi mashinani.

Kigaila amesema licha ya Mbowe kutoa wito wa kuvunjwa kwa makundi na kuundwa kwa kamati ya maridhiano baada ya uchaguzi wa chama, ushauri huo uligonga mwamba kupitia kauli ya Mwenyekiti Tundu Lissu.

 “Lakini mwenyekiti aliyeshinda alimshutumu Mbowe palepale mbele ya wajumbe, hilo lilipeleka ujumbe kwa kundi lililokuwa likimuunga mkono Mbowe kuwa kampeni za kuchafuana hazikuwa zimeisha,” amesema.

Mbali na hilo, lakini amesema chama hicho kwa sasa kinaendeshwa bila vikao, akitolea mfano tangu Lissu akamatwe hakuna kikao cha Kamati Kuu kimefanyika wala hakuna kikao kilichopitisha uamuzi wa kutoshiriki uchaguzi.

“Tunatafuta jukwaa muafaka la kwenda kuwatumikia Watanzania kwa sababu hatujazeeka, tunaondoka leo Chadema tunaenda kutafakari tutaenda chama gani, lakini mjue CCM si mbadala wetu, ila tutawaambia ni wapi tunakwenda,” alisema.

Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Zanzibar, Salum Mwalimu amesema anaungana na Kigaila kukihama chama hicho kwa kuwa kila wakijaribu kuushauri uongozi uliopo juu ya kaulimbiu “No reforms, no election”, hawasikilizwi.

"Nimekaa Chadema miaka 17, nashauri hawanisikilizi kila nikiwafuata ni No reforms, no elections, sasa sisi ni watu wazima, tumevumilia tumechoka ndani ya Chadema hakuna kinachoendelea," amesema.

"Natangaza rasmi uanachama wangu ndani ya Chadema unakoma, hakuna cha kuogopa naenda kuendeleza talanta yangu sehemu nyingine," amwsema Mwalimu.

Akizungumza kwenye mkutano huo, aliyekuwa Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Catherine Ruge amesema "Siku zote naamini Chadema ilisajiliwa kwa ajili ya kushika dola na kutatua matatizo makubwa ya msingi.

“Lakini leo Chadema niliyoitumikia kwa jasho langu la damu ndani ya miaka 15 na hakuna anayeweza kubeza, badala ya kubuni mbinu ya kuwapa matumaini wananchi namna ya kuikabili CCM, matokeo yake wanawatia hofu Watanzania.”

“Niliwahi kushauri lakini sikuzingatiwa, mimi siwezi kuwa kwenye chama ambacho siamini kwenye ajenda na msimamo,” amesema Ruge.


Chadema yajibu mapigo

Akizungumzia uamuzi wa makada hao wa Chadema kukihama chao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, (Tanzania Bara), Amani Golugwa amesema hakuna pigo waliloliacha Chadema na kwa kufanya hivyo wamepotoka.

Kifuatia hatua hiyo, Golugwa amesema hana baya la kuwasema ijapokuwa wameamua kuondoka basi waendelee na safari zao.

"Kama wanachama tungetamani waendelee kuwepo lakini kwa kuwa wamepotoka hakuna pengo lolote. Wengine wanashuka wengine wanapanda, safari itaendelea," amesema

Golugwa amesema: “Chadema hakuna udikteta, Lissu au Heche wamedikteta wapi hata mimi Golugwa sura yangu imekaa kidikteta hii?

“Tumekaa vikao kama kule Bagamoyo, ndiyo maana Aprili 3 tuliwaita watia nia tukasemezana. Wanaosema Chadema inaua ndoto za watu, hao wamepotoka”.

Amesema Chadema inadai mabadiliko, kuponya majeraha na kama watu ambao wanataka waponye nao majeraha hawaonyeshi ushirikiano, chama hicho hakitakuwa na la kufanya na hakuna athari kwa kuondoka kwao.

“Salumu Mwalimu nilimuomba twende naye Kusini hakuonekana. Mrema si kiongozi, hivyo kusema Chadema inafukuza viongozi, ni nani? Chama kinataka watu tumejaribu kuwavuta hawavutiki. Mtu anaenda kupinga na kubagaza chama”

“Ninachoweza kusema sina baya la kuwasema ila wamepotoka, sasa safari yao haitakuwa salama wataenda kuishia kugombana na Watanzania,” amesema.

“Hakuna udikiteta, hiki ni kituo cha demokrasia… azimio la kupata mabadiliko lilianza tangu huko nyuma, hivyo kusema kuna udikiteta na watu hawasikilizwi sio kweli, kwani wanasikilizwa na wanapewa ushauri.


Mitizamo ya wadau

Kuhusu hamahama ya makada wa vyama, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus amesema wanasiasa wengi kukosa itikadi madhubuti wanazozisimamia ni sababu kubwa inayochangia hali hiyo.

“Walio wengi wanakuwa na masilahi yao mengine ya kisiasa kupitia hivi vyama, kwa mtu mwenye itikadi iliyodhibitika anaamini hizi ni nyakati za kiuongozi zitapita na mimi nitabaki na itikadi yangu,” amesema.

Kulingana na Dk Faraja amesema athari za kuhamahama ni kuwa taswira nzuri ya kuaminika kwenye jamii inaweza kupotea endapo itawahukumu kwamba wanatamaa ya uongozi na masilahi yao binafsi.

“Tumeona baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani walivyohama ushawishi wao haukuwa mkubwa, kwa mwaka 2016 hadi 2017 hamahama ilikuwa kubwa na nyuma yao waliahidiwa vyeo walikokuwa anaenda,” amesema

DK Faraja amesema wanasiasa wengi kuwa na hamu ya madaraka ni sababu inayowasukuma kuhama huku akitolea mfano Edward Lowassa aliwahi kuhama kutoka CCM kwenda Chadema baada ya kukosa madaraka.

“Augustino Mrema alihama kutoka CCM kwenda upinzani baada ya kukosa madaraka, Bernard Membe alihama baada ya kukosa madaraka CCM, lakini kuna watu wanahama vyama kwa sababu ya ufuasi wenye ndoto kubwa ya kutafuta madaraka wanakuwa na wafuasi wao,” amesema.

Dk Faraja amesema kwa kuangalia matukio hayo makada wengi kuhama utagundua si suala la itikadi, bali walio wengi wanahama baada ya kuona ndoto zao za kupata vyeo zinaenda kufa.

Amesema hata sakata la Chadema ukifuatilia wengi walikuwa wanamuunga mkono Mbowe na walikuwa wanaamini watanufaika kwa kuamini walikuwa kwenye sekretarieti.

“Wanaona ugumu zaidi kuishi kama raia nje ya misingi ya uongozi wa chama, ndiyo maana wanatafuta mazingira ya kuomba huruma ya umma lakini hoja za msingi unakuta hawana,” amesema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Revocutus Kabobe, amesema kuhama kwao kunatokana na matokeo ya uchaguzi wa ndani waliofanya baada ya kuibuka makundi mawili.

“Katika sayansi ya siasa ni jambo la kawaida mnapotaka kwenda katika chaguzi lakini baada ya chaguzi kambi zinapaswa kuvunjwa na kuleta umoja, Chadema kwa maoni yangu kimeshindwa kuponya haya majeraha na makovu ya uchaguzi,”amesema.

Amesema ukiwasikiliza kwa makini baadhi wanaonyesha kulalamika kwamba wanaonewa na wametenda dhabi kumuunga mkono Mbowe, ingawa haijulikani kigugumizi kiko wapi kwani Mbowe mwenyewe alishakubali matokeo.

“Pili naweza kuwatupia jiwe hawa waliondoka wameshindwa kutii mtazamo na msimamo wa chama kilichoamua No reforms no election.

“Nikweli kwenye siasa kila mmoja anakuwa na ndoto zake, tangu mwanzo nilitegemea wataondoka kwa kuwa lengo lao ni kushiriki uchaguzi,” amesema.

Kuhusu uimara wa Chadema, Dk Kabobe amesema hadhani kama kundi linaloondoka linaweza kuwa na wafuasi wengi nje ya viongozi wale waliojibainisha hadharani.

“Maoni yangu sioni kama kuondoka kwao Chadema kinaweza kuparaganyika, naamini wataondoka wao kama wao na chama kitabaki na kitaendelea kuwepo,” amesema.