Prime
Chadema yatoa kauli vigogo waliotangaza kuhama

Muktasari:
- Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakuna pengo lililoachwa na wanachama wake waliotangaza kujiondoa ndani ya chama hicho.
Dar es Salaam. Saa chache baada ya waliokuwa wajumbe wa sekretarieti ya Chadema katika uongozi uliomaliza muda wake kutangaza kuondoka kwenye chama hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, Amani Golugwa amewajibu akisema wamepotoka huku akisisitiza hakuna pengo waliloliacha.
Baadhi ya wajumbe hao waliotangaza kukihama chama hicho leo Jumatano, Mei 7, 2025 ni waliokuwa manaibu, Benson Kigaila (Bara), Salum Mwalimu (Zanzibar) na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema.
Wengine ni aliyekuwa Katibu wa sekretarieti, Julius Mwita na aliyewahi Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha), Catherine Ruge.
Wamesema wamechoshwa na ubaguzi, udikiteta na ukiukwaji wa katiba ya chama ulioanza tangu kumalizika kwa uchaguzi ambao ulishuhudia Tundu Lissu akiibuka mshindi wa uenyekiti huku Freeman Mbowe aliyekuwa akitetea nafasi hiyo akishindwa.
Mbele ya waandishi wa habari wamesisitiza kuhama chama hicho hakutawazuia kuendelea na mapambano ya kisiasa kwani wanatafakari kuhamia jukwaa lingine.
Kufuatia hatua hiyo, Mwananchi limemtafuta Golugwa ambaye amesema hana baya la kuwasema japokuwa wameamua kuondoka basi waendelee na safari zao.
"Wamepotoka kwenye hicho walichokifanya na waliowapotosha wanashangilia kwa kupotoka kwao," amesema.
Kuhusu kuacha pengo amesema: "Kwa sababu wamepotoka hakuna pengo lolote waliloacha. Ni wanachama tungetamani waendelee kuwepo lakini kwa kuwa wamepotoka hakuna pengo lolote. Wengine wanashuka wengine wanapanda safari itaendelea."
Amesema Chadema hakuna udikteta: “Lissu au Makamu Mwenyekiti-Bara, John Heche wamedikteta wapi hata mimi Golugwa sura yangu imekaa kidikteta hii?amesema akishangaa.
“Tumekaa vikao kama kule Bagamoyo, ndiyo maana Aprili 3, 2025 tuliwaita watia nia tukasemezana nao.”
Amesema wale wanaosema Chadema inaua ndoto za watu au mtu wamepotoka.
Suala la kugombea uchaguzi unatakiwa kuwa huru na wazi unaoaminika ndio maana tunadai mabadiliko.

Amefafanua chama kinadai mabadiliko, tunaponya majeraha sasa kama watu ambao tunataka tuponye nao majeraha hawaoneshi ushirikiano hakuna tunachoweza kuwafanya, acha waende.
“Salum Mwalimu nilimuomba twende naye Kusini lakini hakuonekana. Mrema sio kiongozi hivyo kusema Chadema inafukuza viongozi ni kina nani?
Chama hiki kinataka watu tumejaribu kuwavuta lakini hawavutiki. Mtu anaenda kupinga na kubagaza chama hadharani. “Ninachoweza kusema sina baya la kuwasema ila wamepotoka sasa safari yao haitakuwa salama wataenda kuishia kugombana na Watanzania,” amesema.
Golugwa ameema: “Ukisema Chadema inaua ndoto za watu ujue anapotoka, wapiganaji tuliowazoea wanaondoka hawako sahihi kwenye sababu zote wanazozitoa au wamejipotosha na wamechagua uelekeo wa kujiangamiza wenyewe.”
“Hakuna udikteta hiki ni kituo cha demokrasia, udikiteta unafanyikaje ni lini Lissu, Heche na mimi tumedikiteta hata sauti hii imekaa kidikiteta hii, tumefanya vikao Bagamoyo hapa Dar es Salaam.”
"Azimio la kupata mabadiliko lilianza tangu huko nyuma kusema kwamba kuna udikiteta watu hawasikilizwi hapana, mbona wanasikilizwa na wanapewa ushauri, hakuna aliyewahi kusema neno ambalo linaendana na nafasi ya chama ndiyo maana tuliwaita watia nia wote ili tuzungumze na tusemezane,” amesema.
Amesema si kwamba chama hicho hakichukui hatua kuna Baraza la Wazee tulilolipa jukumu la kuponya majeraha na lipo kwenye hatua ya kushughulikia hilo.
"Sasa watu wanaitwa waponywe kadri tunavyowatafuta, lakini hawataki kuja utafanyaje, wamepotoka," amesema