Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

G55: Kiburi cha viongozi sababu Chadema kutosaini kanuni za maadili ya uchaguzi

Msemaji wa kikundi cha G55, John Mrema akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumanne Aprili 22, 2025. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Kundi la watia nia la Chadema maarufu G55, limesema licha ya Chadema kutangazwa kutoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, limewasihi makada wa chama hicho, kutofanya uamuzi wa haraka wa kuhama chama hicho, kwa kuwa kuna juhudi za ndani ikiwemo mashauriano yanafanyika ili kupata muafaka wao.

Dar es Salaam. Umoja wa watiania wa ubunge ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanaounda G55, umedai uamuzi wa chama hicho kugomea kusaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ni matokeo ya kiburi kilichotawala kwa viongozi.

Licha ya hatua hiyo, G55 imewasihi watia nia wote wasifanye uamuzi wa haraka wa kukihama chama hicho, kwa kuwa kuna juhudi za ndani ikiwemo mashauriano yanafanyika ili kupata mwafaka wao.

Ingawa tayari makada wengine wameshaanza harakati za kukihama Chadema na kutimkia vyama vingine vya upinzani ili kutimiza ndoto zao za kuwania udiwani na ubunge.

Wiki iliyopita Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba katika mahojiano yake na gazeti hili, alisema kwa kushirikiana na wazee wenzake wanawasiliana na Chadema na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kupata mwafaka wa jambo hilo.

Wakati G55 ukitoa madai hayo, uongozi wa Chadema umesema kwa sasa hawapo kubishana na baadhi ya makada wa chama hicho, hasa kundi hilo badala yake wamejikita kusimamia ajenda ya ‘No reforms, no election’ ili kuishinikiza Serikali kufanya mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.

“Kwa niaba ya viongozi wenzangu, tusingependa kubishana na wanachama sio njia sahihi, hawa wamepotoka…Tusingetamani kubishana nao kwa njia hii, taratibu za chama chochote za siasa ni kuzungumza kwenye vikao, lakini sio staili yao…

“Hakuna kiongozi yeyote wa Chadema atakayebishana na wanachama sina lolote la kuzungumza, hatuna la kuwajibu wala kubishana nao. Tulishasema tunasimamia msimamo huu kwa kutaka mabadiliko yafanyike, kwa sababu tumeshapata uzoefu wa chaguzi zilizopita,” amesema Aman Golugwa ambaye ni Naibu Katibu Mkuu (Chadema) Bara.


Kilichosemwa na G55

Akizungumza na wanahabari leo Jumanne Aprili 22, 2025 Msemaji wa G55, John Mrema alianza kueleza masikitiko kuhusu ushauri waliotoa Aprili 3 mwaka huu wa kukitaka Chadema kusaini kanuni kutofanyiwa kazi na uongozi.

Mrema amesema hatua ya Chadema, kutosaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi Mkuu, Aprili 12, 2025 jijini Dodoma kimekosa sifa ya kushiriki mchakato huo, ambapo kitalazimika kusubiria hadi mwaka 2030.

Aprili 12, 2025 Mkurugenzi wa INEC, Ramadhan Kailima alitangaza Chadema kutoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba na chaguzi ndogo zitakazofuata kwa muda wa miaka mitano baada ya chama hicho, kususia kusaini kanuni.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala jana amewataka watendaji wa INEC wajitathimini kama wanaweza kutekeleza majukumu yao baada ya kueleza kuwa, Chadema hakitashiriki uchaguzi mkuu wa 2025 kutokana na kugomea kusaini kanuni za maadili.

Akizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa, Jacobs Mwambegele amesema kilichozungumzwa na tume hiyo ni tafsiri yao, huku akisema kama Chadema wanatafsiri tofauti basi mtafsiri wa mwisho wa mambo hayo ni Mahakama.

Katika maelezo yake Mrema amesema, “jambo hili limeua ndoto za muda mrefu wanachama wa Chadema, wapo watu wapo ndani ya chama hiki kwa sababu wanatamani kuwania udiwani ili kuwakilisha wananchi au wengine wanatamani kuwania ubunge, lakini ndoto zao zimekufa kwa chama kutosaini kanuni,”

“Watu hawa waliokuwa na ndoto za muda mrefu za kushiriki katika nafasi za uamuzi, ndoto zao zimekufa kwa kiburi cha viongozi wetu. Baadhi viongozi wa dini wanaounga mkono reforms, lakini si kuzuia uchaguzi,” amesema Mrema.

Mrema ameongeza kuwa, “kiburi chao wanasema watazuia uchaguzi, ukiwauliza utazuiaje uchaguzi, wanasema wanaingia barabarani je watu wasipojitokeza je. Siku ya uchaguzi wapo wananchi wanaenda kupiga kura sasa tunaotaka kuzuia, tunakwenda kuwazuia wananchi? Amehoji Mrema.

Amesisitiza kuwa waliposhauri Chadema kisaini kanuni walijua madhara yake kwa chama amabacho hakitatimza takwa hilo, kutokana na kundi la G55 kuundwa na makada waandamizi waliowahi kuwa wabunge kwa miaka 15.


Makada Chadema wataka kuhamia vyama vingine, G55 yawabembeleza

Mrema amesema kutokana na kinachoendelea hivi sasa kuna maelfu ya makada wa chama hicho na wengine wameanza kuondoka Chadema kutafuta vyama mbadala.

“Tumesikia kule Ruvuma madiwani wameondoka, Arumeru (Arusha), aliyekuwa mtia nia ubunge ameondoka na wengine wanauliza tufanye nini? Kwa sababu wapo WanaChadema wenye ndoto za kuwatumikia wananchi katika maeneo yao,”

“Wito wetu naomba watulie kwa sasa, wakati tukiendelea kutafakari pamoja na chama chetu, tunawasihi na kuwashauri watia nia wenzetu wa ubunge, udiwani na urais watulie wasifanye uamuzi wa haraka wenye hasira,”amesema Mrema.

Amewataka kuwa watulivu na kutokakata tamaa za kuendelea na shughuli za kisiasa kwa wakati huu, na siku si huenda wakapata ufumbuzi wa sintofahamu hiyo, kutokana na mashauriano yanayoendelea yakishirikisha makundi ya wadau wa demokrasia.


Wanaounga G55 wanashughulikiwa

Kwa mujibu wa Mrema, wanachama na watia nia waliounga mkono kuendelea kutishiwa na kushughulikiwa ndani ya chama kwa maelekezo kupelekwa ngazi ya chini kabisa ya matawi ya Chadema ili wawachukulie hatua.

“Maelekezo haya yameenda maeneo mbalimbali ni utamaduni mpya ndani ya Chadema, hatujawahi kuona hali hii. Ndani ya Chadema tumeishi tukiwa na maoni na mitizamano tofauti kwa kipindi kirefu, pasipo watu kuchukuliwa hatua,

”Ni utamaduni unaokuwa kwa kasi unashereheshwa na matusi, sasa hivi ukiwa na maoni au mtazamo tofauti, rafiki yangu? Utashughulikiwa nakishauri chama waachane na utamaduni huu hautakia Chadema salama,” amesema Mrema.