Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Heche awashukia G55, adai wamefika bei, Mrema ajibu mapigo

Muktasari:

  • Waliokuwa viongozi na makada wa Chadema waliokuwa wakishauri chama hicho kishiriki uchaguzi mkuu ujao maarufu kama G55 walitangaza kujivua uanachama Mei 7, 2025.

Karagwe. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche amewashukia waliokuwa makada wa chama hicho waliotangaza kujivua uanachama akidai wamefika bei.

Akihutubia mikutano ya hadhara ya kampeni ya No reforms, no elections kwa nyakati tofauti katika Wilaya za Kyerwa na Karagwe leo Alhamisi, Mei 8, 2025 Heche amesema baadhi ya makada hao wamefika bei baada ya kupokea ahadi ya nafasi za uongozi, fedha na vifaa vya kampeni katika uchaguzi mkuu ujao.

Mbunge huyo wa zamani wa Tarime Vijijini ametaja sababu nyingine iliyowakimbiza baadhi ya waliokuwa makada hao kuwa ni hasira ya kukosa nafasi za ujumbe kwenye Sekretarieti mpya ya Chadema.

"Baadhi ya waliotangaza kujiondoa Chadema wamedumu kwenye Sekretarieti kwa miaka kati ya 17 hadi 22; sasa uongozi mpya umewateua wana Chadema wengine kushika nafasi hizo imekuwa nongwa," amesema Heche.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche akisalimiana na wananchi wa Omurushaka Wilaya ya Karagwe waliomzuia njiani akiwa njiani kwenda mjini Kayanga yaliyo Makao Makuu ya Wilaya ya Karagwe. Heche na msafara wake alikuwa anatoka Nkwenda wilayani Kyerwa. Picha na Peter Saramba

Amewataka Watanzania kutokatishwa tamaa na wanaofika bei na kusaliti imani ya kupigania  mabadiliko ya kimfumo kwenye uongozi wa nchi kwa sababu viongozi na makada wa Chadema waliosalia wataendeleza mapambano bila kuchoka wala kurudi nyuma.

Amesema tayari wanazo taarifa kuwa viongozi na makada kadhaa wa Chadema wanashawishiwa kujivua uanachama kwa ahadi mbalimbali ikiwemo fedha na vyeo. Sisi hatutatetereka wala kurudi nyuma katika mapambano ya kudai haki, usawa kwa wote na ustawi wa Watanzania," amesema Heche

Amesema milango iko wazi kwa wote wanaosukumwa na tamaa ya nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao waondoke kwa sababu fursa hiyo hawataipata kupitia Chadema iwapo hakutafanyika mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi unaotoa fursa sawa kwa vyama na wagombea wote.

"Tuna taarifa baadhi ya walioondoka wamepata ahadi ya kusaidiwa kufedha na vifaa yakiwemo magari na pikipiki ili wagombee ubunge; sasa wajiulize iwapo kweli watashinda baada ya kuhamia vyama vingine kwa sheria na mfumo huu huu kama hawakuweza wakiwa ndani ya Chadema inaungwa mkono na Watanzania wengi," amesema Heche

Amesema licha ya mbinu zinazofanyika kuwadhoofisha, viongozi wa Chadema hawatarudi nyumba katika kampeni ya no reforms, no elections hadi mabadiliko yatakapofanyika.

"Sisi hatutaki upendeleo, bali tunachohitaji ni haki na usawa katika uwanja wa siasa kutoa fursa kwa Watanzani siyo tu kuwachagua viongozi wanaowataka, bali pia nguvu ya kuwawajibisha wasipotimiza wajibu na ahadi zao za uchaguzi," amesema Heche


Mrema ajibu mapigo akimjibu Heche

Akizungumzia madai ya wao kufika bei, Msemaji wa kundi la makada waliojivua uanachama wa Chadema maarufu kama G55, John Mrema amesema tuhuma hizo haziwatendei haki kwa sababu wameeleza wazi kilichowatoa Chadema.

"Makama Mwenyekiti wa Chadema anatukosea sana kusema tumefika bei kusaliti imani yetu katika haki na usawa; ni vema viongozi wa Chadema wakubali matatizo yaliyopo ndani ya chama chao na kuyatafutia majawabu," amesema Mrema

Huku akionyesha msisitizo, Mrema amesema, "Sisi tulikuwa tunadai haki ya kuingia kwenye uchaguzi ili tushinde na kuleta mabadiliko kwa sababu hatuwezi kuleta mabadiliko tukiwa nje ya uongozi wa dola. Tumeondoka kwa sababu Chadema imejigeuza kuwa chama cha harakati kisichoshiriki uchaguzi," amesema.

Msemaji huyo wa zamani wa Chadema ametaja sababu nyingine iliyowafanya wajivue uanachama wa chama hicho kuwa ni chuki na ubaguzi dhidi ya makada waliomuunga mkono Mwenyekiti wa zamani, Freeman Mbowe wakati wa uchaguzi mkuu wa chama Januari 21, 2025.

"Sisi hatujapewa ahadi yoyote kutoka kwa mtu yeyote, tumeondoka Chadema kwa sababu ya chuki na ubaguzi dhidi ya tuliomuunga mkono Mbowe," amesema Mrema.

Amesema uchaguzi wowote lazima uwe na makundi ya wagombea, hivyo walioshinda walipaswa kuyaunganisha makundi yote kujenga na kurejesha umoja, kazi ambayo anadai uongozi mpya chini ya Tundu Lissu haujafanya.

"Badala ya kukiunganisha chama, hivi sasa yeyote aliyemuunga mkono Mbowe anaonekana adui na msaliti," ameongeza.

Kuhusu madai ya kuwarubuni makada wengine kuondoka Chadema, Mrema amesema; "Wao (viongozi wa Chadema) wana hofu ya watu kuondoka kutafuta fursa za kugombea katika uchaguzi ujao. Chadema ina madiwani 85 ambao walioshinda uchaguzi mwaka 2020; hawa bado wanapendwa na wapigakura wao, watakwenda vyama vingine kutafuta fursa ya kuendelea kuwawakilisha wananchi," amesema.


Nongwa ya kuondoka Sekretarieti

Akizungumzia madai ya kuchukizwa na uamuzi wa kuondolewa kwenye sekretarieti, Mrema amesema kati ya kundi la zaidi ya wanachama 55 waliojiondoa, ni watu wasiofika 10 ndio walikuwa wajumbe wa sekretarieti.

"Kama ni kuondoka Chadema kwa kukosa mapato, basi tungeondoka miaka ya 2021 au 2022 ambapo tulifanya kazi kwa miaka miwili bila malipo baada ya chama kususia ruzuku," amesema Mrema