Tanzania yajibu mapigo azimio la Bunge la Ulaya

Muktasari:
- Kutokana na maazimio ya Bunge la Ulaya, yaliyochapishwa katika tovuti yao, Serikali ya Tanzania imeeleza kusikitishwa na uamuzi huo kufikiwa kwa kufuata taarifa za upande mmoja, huku ikifafanua mageuzi yaliyofanyika nchini.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeeleza kusikitishwa na azimio la Bunge la Umoja wa Ulaya ikidai kwamba uamuzi uliofikiwa kwa kuzingatia taarifa zisizo kamili au za upande mmoja bila kuwasiliana na Serikali kwa njia za kidiplomasia.
Serikali imeeleza hayo katika taarifa iliyotolewa Mei 8, 2025 na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikiwa ni siku moja tangu Bunge la Umoja wa Ulaya lilipojadili suala la kushikiliwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu na kulaani kitendo hicho.
Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025 akiwa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wake wa hadhara na baadaye aliletwa Dar es Salaam ambako alifunguliwa mashtaka mawili; kuchapisha taarifa za uongo na uhaini.
Kutokana na mwenendo wa kesi hiyo, Bunge la Umoja wa Ulaya lilijadili na kutoa maazimio kuhusu kukamatwa kwa Lissu na kufunguliwa kesi ya uhaini ikilaani kitendo hicho kwa madai kwamba mashtaka hayo ni ya kisiasa.
Bunge hilo limezitaka Mamlaka za Tanzania kusitisha mara moja ukandamizaji unaozidi kuongezeka, ukamataji holela, ukatili, mashambulizi na unyanyasaji dhidi ya wanachama wa upinzani, watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari na mashirika ya kiraia.
Pia, imezitaka Mamlaka za Tanzania kuirejesha Chadema kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 na kuvishirikisha vyama vyote vya siasa katika majadiliano ya wazi kuhusu mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi.
Bunge hilo limeazimia kwamba Umoja wa Ulaya (EU) na nchi wanachama kushauriana na mamlaka za Tanzania kuhusu kesi ya Lissu na kufuatilia kwa karibu mwenendo mzima wa kesi hiyo. Pia, limeitaka Tanzania kukomesha adhabu ya kifo.
Kadhalika, Bunge hilo limeitaka EU kuhakikisha kwamba ushirikiano wa maendeleo kati yake na Tanzania unafuata misingi ya kulinda haki za binadamu, uhuru wa kujieleza na viwango katika mashitaka ya haki.
Jana, Mei 8, 2025, bungeni jijini Dodoma, wabunge walionyesha kushangazwa na maazimio hayo dhidi ya Serikali ya Tanzania, wakisema hatua hiyo ni dhihaka kwa Mamlaka ya kitaifa na maadili ya Kitanzania.
Kauli ya Serikali
Kutokana na maazimio hayo ya Bunge la Ulaya, yaliyochapishwa katika tovuti yao, Serikali ya Tanzania imeeleza kusikitishwa na uamuzi huo kufikiwa kwa kufuata taarifa za upande mmoja huku ikifafanua mageuzi yaliyofanyika nchini.
Taarifa hiyo inaeleza kwamba wakati Tanzania ikiheshimu uhuru wa kitaasisi wa Bunge la Ulaya na kuthamini ushirikiano wake na Umoja wa Ulaya, inaona ni muhimu kufafanua baadhi ya mambo na kusisitiza dhamira yake ya muda mrefu ya maadili ya kidemokrasia, utawala bora na utawala wa sheria.
Wizara, katika taarifa hiyo, imefafanua kwamba tangu Machi 2021, Tanzania imefanya mageuzi mapana ya kisiasa na kisheria chini ya falsafa ya 4Rs (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya).
Inaeleza kwamba marekebisho hayo yameleta matokeo yanayoonekana, ikiwa ni pamoja na kurejeshwa kwa uhuru wa kisiasa, upanuzi wa uhuru wa kiraia, kuimarishwa kwa uhuru wa vyombo vya habari, na kupitishwa kwa sheria mpya za uchaguzi Machi 2024, ambayo ilisababisha kuanzishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasikitishwa zaidi na mwenendo unaoendelea kama inavyoonekana katika azimio la Bunge la Ulaya la baadhi ya watendaji wa kimataifa kutoa uamuzi kwa kuzingatia taarifa zisizo kamili au za upande mmoja, bila ya kwanza kuwasiliana kupitia njia za kidiplomasia. Hali hii inatafsiri vibaya na kupotosha hali halisi,” Serikali imebainisha.
Pia, Serikali imesikitishwa na kesi moja kutumika kuihukumu Tanzania wakati kuna maendeleo makubwa yaliyopatikana katika maeneo kama vile uhuru wa vyombo vya habari, ushirikishwaji wa kisiasa, mageuzi katika mifumo ya uchaguzi na ujenzi wa amani ya kikanda, lakini hayajatambuliwa.
Taarifa hiyo ya wizara imeweka bayana kwamba Tanzania ni nchi huru yenye katiba yake na inaongozwa na utawala wa sheria. Masuala yote ya kisheria yanashughulikiwa kwa uhuru na Mahakama ikiwa ni moja ya mihimili ya nchi.
“Kwa hiyo, kauli zinazoashiria au kuhimiza uingiliaji kati wa watendaji katika kesi zinazoendelea si tu kwamba hazifai, bali pia ni kinyume na kanuni ya uhuru wa kimahakama kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Tanzania na inavyotetewa na Umoja wa Ulaya,” Serikali imesema.
Tanzania inasisitiza kwamba ushirikiano wowote lazima uzingatie kuheshimiana kwa maadili, ikiwa ni pamoja na kuheshimu mamlaka, Katiba, mifumo ya sheria na utambulisho na ushirikiano wa baadaye unaozingatia vipaumbele vya pamoja katika maendeleo, utawala, ukuaji wa uchumi, ustawi wa watu na ustawi wa kimsingi.
“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuthamini ushirikiano wake na Umoja wa Ulaya na iko tayari kwa mazungumzo ya wazi, yenye heshima na yenye msingi wa ushahidi kuhusu masuala yenye maslahi na kujali.
“Hata hivyo, mazungumzo haya lazima yakingwe katika uwazi, haki, kuheshimiana, na kuthamini kikamilifu mamlaka ya kila taasisi ya nchi, na katiba, pamoja na muktadha wa kisheria na kiutamaduni,” inaeleza taarifa hiyo ya Serikali.
Pia, imebainisha kwamba wakati Tanzania ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025, Serikali inasisitiza dhamira yake thabiti ya kudumisha amani, kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki na kulinda haki za msingi na uhuru wa raia wote kwa mujibu wa Katiba yake.
Maoni ya wadau
Akizungumzia azimio la Bunge la EU, mchambuzi wa masuala ya uchumi Oscar Mkude amesema endapo Serikali ya Tanzania haitatekeleza waliyosema, itawekewa vikwazo ingawa haamini kama hatua hiyo itakuwa ya haraka.
“Ikifikia huko itaongeza changamoto japo Tanzania hatufanyi biashara kubwa na nchi za Ulaya, bali Asia, lakini kwenye masuala ya utandawazi kuna thamani huhitajiki kupoteza, kama itatokea matokeo yake hayatakuwa makubwa,” amesema.
Mkude amesema athari nyingine ambayo inaweza kutokea ni usitishwaji kwa misaada au kuzuia taasisi zao kutoa ithibati kwa nchi ya Tanzania, japo nao wananufaika, amesisitiza uamuzi wa kutekeleza hayo utakuwa mgumu.
Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa, Buberwa Kaiza amesema Bunge la Umoja wa Ulaya linachangia bajeti ya Tanzania kwa kiwango kikubwa, hivyo ikiweka azimio ambalo litahitaji kutekelezwa na kutotelezwa kutakuwa na athari kwenye bajeti ya nchi.
“Kwa sababu azimio linachagiza masuala ya demokrasia, kama Serikali haitatekeleza wataweka vikwazo ambavyo vitaathiri huduma za afya, elimu na barabara. Pia, mataifa ya EU yanawasiliana, kwa hiyo hata Marekani nayo itajadiliana kuhusu suala hili,” amesema.
Buberwa amesema hata biashara nayo itakuwa kwenye matatizo kutokana na vikwazo na Tanzania itatengwa kidiplomasia.