Wabunge wapinga maazimio ya Bunge la Umoja wa Ulaya dhidi ya Serikali ya Tanzania

Muktasari:
- Kauli za wabunge hao zimebeba ujumbe wa umoja, uzalendo na msimamo thabiti wa kulinda uhuru wa taifa, huku wakitoa wito kwa Serikali kutumia vyombo vyake vya kidiplomasia kuwasilisha ujumbe huo kwa Umoja wa Ulaya kwa njia ya heshima, lakini yenye msimamo usiotetereka.
Dodoma. Wabunge wameonyesha kusikitishwa na kushangazwa na maazimio sita yaliyotolewa na Bunge la Umoja wa Ulaya dhidi ya Serikali ya Tanzania, wakisema hatua hiyo ni dhihaka kwa mamlaka ya kitaifa na maadili ya Kitanzania.
Maazimio hayo yalitolewa Mei 7, 2025, katika kikao cha Bunge la Umoja wa Ulaya, ambapo wanachama wa umoja huo wanatarajiwa kupiga kura Mei 8, 2025.
Miongoni mwa maudhui ya maazimio hayo yanahusu masuala ya ndani ya Tanzania, ikiwemo mwenendo wa kesi ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu, hali ya demokrasia nchini, na msimamo wa Tanzania kuhusu mapenzi ya jinsia moja.
Mbunge wa Biharamulo Magharibi (CCM), Ezra Chiwelesa, amepinga maazimio hayo, akisema yanaonyesha dharau kwa mamlaka ya Tanzania na kwenda kinyume na misingi ya kiimani na kiutamaduni ya Watanzania.
Akiwasilisha hoja yake bungeni wakati wa mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Chiwelesa amesema maazimio hayo yanaingilia uhuru wa taifa na heshima ya mahakama, hasa kwa kuzungumzia kesi ya Tundu Lissu, ambayo bado iko mahakamani.
Mbunge huyo amesisitiza kuwa mojawapo ya maazimio hayo yanataka Tanzania kutambua mapenzi ya jinsia moja, jambo ambalo alilikemea kwa kusema ni kinyume na maadili ya taifa, imani za dini, na hata misingi ya kikatiba.
“Hii ni dharau kwa nchi yetu na kwa Mungu tunayemwabudu. Tanzania ni nchi inayomtegemea Mungu, na hatuwezi kukubali kushinikizwa na mataifa ya nje katika mambo ya kimaadili,” alisema kwa msisitizo.
Akiendelea na mchango wake, Chiwelesa amesema ameyasambaza maazimio hayo kwa wabunge wenzake kupitia kundi sogozi la wabunge, waweze kuyasoma na kujua maudhui yake, huku akilitaja azimio la sita kuwa la kudhalilisha kwa kuitaka Bunge la Ulaya kuiandikia Serikali ya Tanzania barua rasmi ya kufikisha maazimio hayo.
“Tunaomba sauti yetu isikike kwa niaba ya Watanzania. Hatukubali maadili yetu kutikiswa kwa misukumo ya kigeni,” aliongeza.
Katika mchango wake, amekumbusha kuwa kabla ya shughuli za Bunge kuanza, wabunge husali pamoja, na viongozi wa dini huombwa kuombea Taifa, jambo linalothibitisha kuwa Tanzania inasimama kwenye misingi ya kidini.
Ameonya kuwa heshima ya nchi haitapaswa kutumbukizwa kwa misingi ya misaada au mashinikizo kutoka mataifa ya nje.
Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara, naye alikubaliana na hoja ya Chiwelesa kupinga vikali maazimio hayo.
Waitara amesisitiza kuwa mila na desturi za Kitanzania haziwezi kuruhusu suala la ndoa za jinsia moja, akitolea mfano wa jamii ya Wakurya, ambayo alisema haiwezi kukubali chifu kuolewa.
“Hata kama hawataleta miradi ya maji, sisi tutakunywa maji ya visima. Maendeleo ni muhimu, lakini hatutauza utu na maadili yetu,” alisema.
Waitara ameeleza kuwa Tanzania ina utawala wa sheria na Katiba inayolinda misingi ya Taifa, hivyo mashinikizo kutoka taasisi za kimataifa hayapaswi kubadilisha mwelekeo wa nchi.
Amekemea vitisho vinavyotolewa na mashirika ya kimataifa vinavyolenga kulazimisha nchi kutambua mapenzi ya jinsia moja, akisisitiza kuwa taifa linapaswa kusimama imara.
Mbunge huyo pia aliunga mkono msimamo wa baadhi ya viongozi wa dunia, kama Rais wa Marekani, Donald Trump, na Serikali ya Uganda waliopinga suala la mapenzi ya jinsia moja.
Amesema ni wakati sasa kwa Tanzania kusimama kidete kulinda watoto wa Taifa dhidi ya athari za mmomonyoko wa maadili unaoletwa kutoka nje.
Wabunge wengine wameunga mkono hoja za Chiwelesa na Waitara, wakikemea maazimio ya Bunge la Umoja wa Ulaya na kuyataja kama hatua ya kuingilia uhuru wa Tanzania.
Wamesisitiza kuwa nchi yao haitakubali kupoteza mwelekeo kwa kushinikizwa kukubali mambo yanayokiuka maadili ya kitamaduni na kidini.