Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bado Chadema hakujapoa, makada wengine wajivua uanachama

Muktasari:

  • Ndani ya siku nne, tayari zaidi ya wanachama wa Chadema 20 wakiwemo waliowahi kuwa viongozi waandamizi zaidi wametangaza kukihama chama hicho, bila kuweka wazi ni wapi mwelekeo wao mpya, huku Chaumma kikihusishwa.

Dar es Salaam. Maji na mafuta yameendelea kujitenga ndani ya Chama cha Demokarasia na Maendeleo (Chadema) baada ya makundi ya makada na viongozi waandamizi kuendelea na safari ya kutangaza kukihama chama hicho kikuu cha upinzani.

Ni maji na mafuta kwa sababu kuna uwiano wa ushawishi na nguvu ya kisiasa waliyonayo kati ya wale wanaotangaza kukihama chama hicho na wale wanaendelea kusalia.

Ingawa kivuli cha mwenyekiti mstaafu, Freeman Mbowe kinadaiwa kuhusishwa kuwa mzizi wa hatua hiyo, wenyewe wanasema wamedai kuchoshwa na yanayoendelea ikiwemo Chadema kukosa mwelekeo na kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa misingi ya kuanzishwa kwa chama hicho.

Viongozi wa kanda na mabaraza wa Chadema wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kutangaza kujivua uanachama wa chama hicho, leo Jumamosi Mei 10, 2025, Dar es Salaam. Picha na Sunday George



Ndani ya siku takriban nne, tayari zaidi ya wanachama wa Chadema 20 wakiwemo waliowahi kuwa viongozi waandamizi zaidi wametangaza kukihama chama hicho, bila kuweka wazi ni wapi mwelekeo wao mpya, huku Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kikihusishwa.

Ukiacha John Mrema aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki na Mawasiliano wa chama hicho kwa zaidi ya muongo mmoja, Chadema imewapoteza viongozi kadhaa wa ngazi mbalimbali wa kanda nane waliotangaza kuhama leo.

Waliotangaza kuhama leo Jumamosi Mei 10, 2025 ni pamoja na Jackson Jingu (aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Kanda ya Kati), Emma Kimambo (Mhazini Kanda ya Kaskazini), Basil Lema (aliyekuwa Katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro) na Gimbi Masaba (aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha Kanda ya Serengeti).

Wengine ni Esther Fulano, aliyekuwa Katibu wa Bawacha Kanda ya Victoria) Doris Mpatili, aliyekuwa Mwenyekiti Kamati ya Mafunzo Kanda ya Victoria) Hadija Said Mwago, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bawacha Jimbo la Mbagala.

Pia, wamo Hanifa Chiwili, aliyekuwa Katibu wa Kamati ya Maadili ya Kanda ya Pwani), Jackline Kimambo (aliyekuwa Katibu wa Kamati ya Mafunzo Kanda ya Kaskazini), Abuu Mrope Mhazini wa Chadema Kanda ya Kusini na Magreth Mlekwa (aliyekuwa Katibu wa Bawacha Kanda ya Nyasa).

Sambamba na hao, pia, yumo Stewart Kaking (aliyekuwa Ofisa wa Kanda ya Kusini), John Lema (aliyekuwa Ofisa Oganaizesheni, Mafunzo na Uchaguzi), viongozi hao wanaotoka kanda nane za Chadema wametangaza kujivua uanachama.

Makamu Mwenyekiti Kanda ya Kati, Jingu Emmanuel akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumamosi Mei 10, 2025, (kushoto) ni Viongozi wa kanda na mabaraza wa Chadema, baada ya kutangaza kujivua uanachama wa chama hicho, jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutangaza kujivua uanachama, Jingu ndiye amesoma tamko la viongozi 13 wenye nyadhifa mbalimbali kwenye kanda hizo waliotangaza kujiondoa ndani ya Chadema.

“Tumefanya tathimin ya kina na kujiridhisha pasipo shaka yoyote ile kuwa Chadema imepoteza mweleko kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kukiukwa kwa Katiba hasa tangu uongozi mpya kuingia madarakani,” amesema Jingu.

Jingu amedai kuwa Chadema hivi kumekosekana kwa uhuru wa mawazo, hasa ushauri wa kundi la watia ni wa ubunge G55 lililoshauri uongozi wa Chadema kushiriki uchaguzi, lakini wakaishia kuitwa wasaliti, huku wengine wakiundiwa mkakati wa kufukuzwa uanachama.

“Kumekuwa na uonevu na kubaguliwa kuanzia uongozi wa Taifa hadi ngazi ya chini hasa kwa viongozi waliokuwa wakimuunga mkono Mbowe. Baada ya kutafakari hali mbaya inayoumiza ndani ya Chadema, leo tumeamua kujivua rasmi uanachama wa Chadema tunakwenda kuunga na waliokuwa wajumbe wa sekretarieti,” amesema Jingu.

Jana, Ijumaa Mei 9, 2025, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Aman Golugwa alizungumza na Mwananchi akisema kwa sasa chama hicho hakipo tayari kujibishana na mtu wakiwemo makada wao wanaotaka kuondoka na waliondoka akiwatakia kila la kheri.

“Chadema hatuna muda wa kutafuta mchawi, hatupo tayari kugombana wala kubishana na wanaoondoka. Kwa vile wapo tayari kuondoka watumie nafasi hiyo kuondoka, walikuwa wanachama tunaheshimu mchango wao,”

“Chadema sasa hivi kinajitengeneza upya ili kuaminika kwa umma katika kupigania mambo ambayo wananchi wanayahitaji, hatupo katika kutafuta mchawi,” amesema Golugwa.

Naye Emma amesema: “ni huzuni na mambo yanayotia uchungu kuona yale tuliyoyajenga yametufikisha hapa kwa chama changu. Si uamuzi mzuri, au wa kufurahisha, lakini imetulazimu kufanya hivi, sina maisha ya kuendelea kusalia ndani ya Chadema.”

Kwa upande wake, Basil aliyekuwa katibu wa Chadema kuanzia mwaka 2009/Mei 25, amesema hivi sasa Watanzania walipaswa kusikia chama kitanyakua majimbo mangapi katika uchaguzi wa Oktoba, lakini imekuwa kinyume badala ya wanasikia wangapi wanakihama.

 “Sasa Watanzania wanasikia chama kilichopanda juu, kinashuka na kinakwenda kupotea, inawauma Watanzania. Ugonjwa uliopo Chadema unaosababisha haya yanayojitokeza ni chuki iliyokuwa kubwa ndani ya chama.

“Ukiwa karibu na Lissu upo salama, ukiwa karibu na Mbowe haupo salama, sasa hivi uhuru wa kukosoa na kujieleza ndani ya Chadema hakuna, ukimkosoa bwana mkubwa wewe ni msaliti utaitwa kila aina ya lugha na vijana ndio mstari wa mbele kutukana,” amesema Lema.