Aweso apata mtihani, afiwa siku ya hotuba yake ya bajeti

Muktasari:
- Miongoni mwao alikuwepo wakati Aweso akiwasilisha hotuba yake ya bajeti, ni Babu Ali ambaye ni mdogo wa Waziri huyo aliyeongozana na wanafamilia wengine kumsindikiza na kujionea tukio hilo.
Dodoma. Kifo ni fumbo. Hivi ndivyo unavyoweza kusema kwani kinaweza kumtokea mtu mahali na wakati wowote kama ilivyo kwa Babu Ali.
Wakati Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiwasilisha hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/26 bungeni jijini Dodoma, kwenye majukwaa ya wageni kulikuwa na ndugu na wageni mbalimbali waliokuja kumsindikiza.
Miongoni mwao alikuwepo Babu Ali, ambaye ni mdogo wa Waziri huyo aliyeongozana na wanafamilia wengine kumsindikiza na kujionea tukio hilo.
Hata hivyo, mara baada ya Aweso kuwasilisha bajeti yake na shughuli za Bunge kuahirishwa, familia walitoka nje na kupiga picha ya pamoja kabla ya kukutana kwenye tafrija ndogo kumpongeza Waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa Pangani.

Babu Ali enzi za uhai wake wakati akiwa bungeni.
Ndani ya Ukumbi wa Bunge, Spika Dk Tulia Ackson aliwatambulisha kila mtu kwa jina lake na Ali alisimama akionekana mwenye furaha kama ilivyokuwa kwa ndugu wengine.
Baada ya tukio hilo, kila mmoja alikwenda kujipumzisha akiwemo Ali aliyefikia katika moja ya hoteli jijini hapa.
Sherehe hiyo ndio kama ilikuwa ya kuagana na ndugu zake kwani Ali hakuamka na walipokwenda chumbani kwake kumuamsha ili wawahi bungeni kumsikiliza Aweso akijibu hoja za wabunge, alikuwa tayari amefariki dunia.
Hata hivyo, leo mapema Aweso alihitimisha hotuba yake bungeni baada ya wabunge kupitisha bajeti yake.

Mpaka sasa sababu za kifo chake hazijafahamika na taratibu za kwenda Pangani, Tanga kwa mazishi zinaendelea nyumbani kwa Aweso eneo la Ilazo jijini Dodoma.
Kama kifo kingeweza kusema huenda Ali asingesafiri kutoka Pangani kwenda Dodoma lakini siri hiyo imefanya aende Dodoma akiwa mzima na kurudi Pangani akiwa amelala usingizi wa milele.
Akizungumza kwa niaba ya a familia, msemaji katika msiba huo, Rashid Shangazi amesema hakuna aliyejua na anayejua hadi sasa nini chanzo cha kifo cha ndugu yao.
Shangazi ambaye ni Mbunge wa Mlalo, amesema Ali na ndugu zake, jana Alhamisi, alikuwa bungeni wakati Waziri Aweso alipokuwa akisoma bajeti yake na hadi usiku alikuwa mzima.
“Kama mlivyomuona jana akitambulishwa pale bungeni, baadaye jioni walikutana wanafamilia wakakaa pamoja katika halfa ambayo Mheshimiwa (Aweso) alikuwa amewaandalia na kisha wakaagana kila mmoja akaenda kulala alipokuwa ameandaliwa,” amesema Shangazi.
Shangazi ambaye ni Katibu wa Wabunge wa CCM, amesema leo Ijumaa Mei 9, 2025 asubuhi walianza kukumbushana ili waende bungeni na wengine kwenda kwenye majukumu yao, ndipo wakagundua kuwa simu yake haipatikani.
“Iliwastua ndugu na walipofuatilia katika chumba alicholala, walimkuta amepoteza maisha, hana historia ya ugonjwa wala tatizo lingine lolote katika maisha yake, isipokuwa tunasema Inna Lillah Wainna Illaih Rajjiun,” amesema Shangazi.

Amesema taratibu za kusafirisha mwili wa marehemu zinaendelea baada ya waombolezaji kupata chakula, safari ya kuelekea Pangani itaanza.
Kwa mujibu wa Shangazi, kesho Jumamosi baada ya swala ya adhuhuri watakwenda kuusitili mwili wa Ali katika nyumba yake ya milele mahali ambapo familia itakuwa imeandaa.
Hata hivyo, amesema suala la nini kilikuwa kinamsibu itabaki ni fumbo kati ya marehemu na Mungu wake kwani hajawahi kusema chochote kama kuna shida katika afya yake.
Kwa upande wake, Waziri Aweso amesema ni mpango wa Mungu, hakuna wa kulaumiwa.
Wabunge wengi wamefika nyumbani kwa Aweso ambapo wanafamilia waliokuwa wamekuja bungeni walikuwepo huku watumishi wa Wizara ya Maji wakionekana kwa wingi.
Wengine waliofika ni Waziri Mkuu na Makamu wa Rais mstaafu, John Malecela ambaye aliongozana na mkewe, Anne Kilango Malecela, wakiwa wamefuata na Mbunge wa Buchosa, Erick Shigongo.