Hivi ndivyo trilioni moja za Wizara ya Maji zitakavyotumika

Muktasari:
- Jumla ya Sh1.01 trilioni zimeombwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji katika mwaka 2025/26.
Dodoma. Bunge limeombwa kuidhinishia Sh1.01 trilioni kwa ajili ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2025/26, huku vipaumbele sita vikiainishwa, kikiwemo cha utekelezaji wa miradi ya maji 1,544 inayoendelea kutekelezwa nchini.
Ombi hilo limetolewa leo, Alhamisi Mei 8, 2025, na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Kati ya fedha hizo zilizoombwa, Sh943.11 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Katika mwaka wa fedha 2024/25, Bunge lilipitisha Sh627.78 bilioni, huku Sh558.11 bilioni zikienda kwenye miradi ya maendeleo.
Hata hivyo, kwa mwaka huu, bajeti kwa ajili ya miradi ya maji imeongezeka kwa asilimia 40.8, ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Aweso ametaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na kutekeleza miradi ya maji 1,544 inayoendelea kujengwa, ikiwemo mingine 1,318 inayotekelezwa vijijini na miradi 226 mijini, ikiwemo ile mikubwa ya kimkakati.
Miongoni mwa vipaumbele vilivyowekwa ni kukamilisha Mpango Kabambe wa Taifa wa Maji, kuimarisha uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na kuendeleza vyanzo hivyo kwa kuchimba visima na kujenga miundombinu ya kuvuna maji ya mvua.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi na udhibiti wa ubora wa maji, ili kuhakikisha yanakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa, sambamba na kuboresha utoaji wa huduma endelevu na kudhibiti upotevu wa maji.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025 / 2026 jijini Dodoma leo Mei 8, 2025
Kipaumbele kingine kilichoainishwa ni utekelezaji wa miradi ya Gridi ya Taifa ya Maji, ikiwemo mradi wa kusambaza maji kutoka Ziwa Victoria kwenda mikoa ya Dodoma na Singida, pamoja na mradi wa kutoa maji Ziwa Tanganyika kwenda mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa.
Miradi mingine ya Gridi ya Taifa ya Maji ni ule wa kutoka Mto Ruvuma kwenda mikoa ya Mtwara na Lindi, na ule wa kutoka Mto Rufiji kwenda mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Pia, maji yatachukuliwa kutoka maziwa ya Victoria na Nyasa kwenda maeneo mbalimbali, ikiwemo vijiji vilivyo jirani na maziwa hayo.
Kwa upande wa huduma za usambazaji wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini, Waziri Aweso amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, wizara imepanga kutekeleza jumla ya miradi 1,318 ya maji vijijini. Vilevile, Serikali itaendelea na jitihada za kufikisha huduma ya maji katika vijiji 1,781 ambavyo bado havijafikiwa.
“Utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji vijijini kutoka wastani wa asilimia 83 hadi zaidi ya asilimia 85,” amesema Aweso.
Kwa upande wa mijini, Aweso amesema miradi 225 ya maji itatekelezwa katika mwaka huo wa fedha, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mitandao ya kusambaza maji katika Jiji la Dar es Salaam na mradi wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji kwenda mikoa ya Dar es Salaam na Lindi.
Miradi mingine itakayotekelezwa ni pamoja na ule wa maji na usafi wa mazingira katika eneo la Vwawa–Tunduma, pamoja na upanuzi wa mtandao wa maji safi katika maeneo ya Kalenga, Mseke, Kiwele na Luhota mkoani Iringa.
Mradi mwingine ni ule wa huduma ya maji Muungano, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, utakaohudumia maeneo ya Kilimani, Mchangani, Lipande, Likangara, Nachingwea, Dodoma Kitandi na Maguja.
Pia, mradi wa kusambaza maji katika miji ya Kigoma, Mpanda na Sumbawanga, pamoja na jamii zinazozunguka Ziwa Tanganyika, utaendelea kutekelezwa.
Wizara pia itaendelea na ujenzi wa miradi ya maji safi na usafi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na mradi wa miji 28 na ule wa kutoa maji kutoka Mto Kiwira kwenda Jiji la Mbeya.
Kwa Jiji la Dodoma, Aweso amesema kuwa katika mpango wa muda wa kati, wizara itaanza ujenzi wa bwawa la Farkwa. Kwa muda mrefu, Serikali inakusudia kutekeleza mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Dodoma kupitia Singida, ambapo usanifu wa mradi huo unaendelea.
Kuhusu kudhibiti upotevu wa maji, Aweso amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, wizara imepanga kufanya ukarabati wa miradi ya maji iliyochakaa ili kupunguza upotevu huo.
Miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na kufunga mita za maji za malipo kabla ya matumizi (pre-paid water meters), kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kulinda miundombinu ya maji, pamoja na kuchukua hatua kali dhidi ya wale wanaohusika na uharibifu wa miundombinu au wizi wa maji.
Waziri Aweso amesema kuwa wizara inalenga pia kudhibiti vitendo vya wizi wa maji vinavyoathiri upatikanaji wa huduma hiyo. Ametoa takwimu zinazoonyesha kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25, wastani wa maji yanayopotea ni asilimia 33.4, kiwango ambacho kiko juu ya kiwango cha kimataifa cha upotevu wa maji, ambacho ni asilimia 20.
Msamaha kwa wadaiwa wa ankara za maji
Waziri Aweso ametangaza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha wa faini zote kwa wananchi waliokuwa wakidaiwa na mamlaka za maji nchini.
Amesema wadaiwa wafike ofisi za mamlaka husika kuanzia leo hadi Mei 31, mwaka huu, ili kupatiwa utaratibu wa kurejeshewa huduma.
Aidha, kwa wateja wote wenye madeni ya muda mrefu, Aweso amesema watapewa utaratibu wa kuyalipa kwa awamu, ili warudishiwe huduma ya maji haraka iwezekanavyo.
“Tuko kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama. Hivyo, tutawawekea utaratibu wa kulipa kidogo kidogo ili huduma isikatike,” amesema.
Pia, ameagiza mamlaka za maji kuhakikisha hazikati huduma ya maji kwa wananchi wakati wa mwisho wa wiki au siku za sikukuu, na kuhakikisha maunganisho mapya ya huduma yanafanyika ndani ya kipindi cha siku saba kwa mujibu wa mwongozo uliopo.