Prime
Zijue amri 10 za kuwa tajiri

Utajiri mara nyingi unahusisha fedha, katika makala hii, tunachambua ‘Amri Kumi’ za Fedha zinazoongoza namna ya kupata, kuhifadhi, kutumia, na kuwekeza fedha kwa busara. Amri hizi si tu kuhusu kujikusanyia utajiri, bali kujenga uhusiano mzuri na fedha, kuhakikisha usalama wa kifedha, na kuacha urithi kwa vizazi vijavyo.
1. Utaweka bajeti ya kisasa daima
Nguzo ya mustakabali mzuri wa kifedha ni kuwa na bajeti ya kisasa. Kujua kipato chako na matumizi hukuwezesha kutenga fedha kwa ajili ya bili, akiba, na matumizi binafsi. Kwa mfano, ukiwa na kipato cha Sh1 milioni kwa mwezi, Sh500,000 (50%) itaelekezwa kwenye mahitaji ya msingi kama kodi ya nyumba, umeme, chakula, na usafiri; Sh300,000 (30%) kwa matamanio kama vile kula nje, burudani, na ununuzi wa vitu visivyo vya lazima; Sh200,000 (20%) kwa akiba, uwekezaji, au kulipa madeni.
2. Utalipa kadi yako ya mkopo
Kadi za mkopo ni rahisi kutumia lakini zina viwango vikubwa vya riba. Malengo yako ya kifedha yanapaswa kujumuisha kulipa salio lote la kadi kila mwezi ili kuepuka kulipa riba. Kama una deni kubwa, anza kwa kuongeza kiasi unacholipa zaidi ya kiwango cha chini. Lipa zaidi kwenye kadi moja hadi uimalize, kisha hamia nyingine.
3. Utajilipa kwanza
Weka malengo ya akiba kabla ya matumizi. Badala ya kuweka akiba iliyobaki, jiwekee utaratibu wa kuweka sehemu ya kipato chako mara tu unapokipokea. Fanya akiba kuwa bili ya lazima kila mwezi. Unaweza kuweka agizo la kudumu (standing order) ili fedha zitolewe kiotomatiki kwenda kwenye akaunti ya akiba.
4. Utaweka malengo ya fedha ya nadhifu
Malengo ya nadhifu ni: Maalumu, Yanayopimika, Yanayowezekana, Yanayohusiana, na Yenye Muda. Kwa mfano, kama unapenda kusafiri mwezi wa Desemba, anza kupanga Januari kwa kujua gharama na kuweka akiba kidogo kila mwezi hadi tarehe ya safari.
5. Utaanzisha akiba ya Dharura
Takwimu zinaonesha kuwa karibu 60% ya Watanzania hawana akiba ya kukabiliana na dharura. Anza kidogo hata Sh50,000 kwa mwezi na iweke katika akaunti tofauti. Ukilazimika kuitumia, hakikisha unaanza kuijaza tena haraka iwezekanavyo.
6. Utaepuka deni na kuishi kwa kipato chako
Uhuru wa kifedha huanza kwa kutumia kiasi kisichozidi kipato chako. Hakikisha matumizi ya kodi ya nyumba pamoja na gharama za huduma hayazidi 20% ya kipato chako ghafi. Kwa mfano, ukiingiza Sh2 milioni kwa mwezi, kodi isivuke Sh400,000.
7. Utawekeza kwa ajili ya baadaye yako
Anza kuwekeza mapema kwa kutumia faida ya riba juu ya riba. Chagua mifuko ya pamoja kama UTT, Timiza, Faida, au Alpha Halal Fund. Pia, fanya juhudi za kununua ardhi mapema kabla bei haijapanda.
8. Utafanya kila kitu kiwe kiotomatiki
Tumia programu za bajeti zinazounganishwa na akaunti zako au simu. Fungua akaunti maalumu kwa ajili ya akiba na dharura, kisha weka maagizo ya kuhamisha fedha kila mwezi. Utaratibu huu utasaidia fedha kuongezeka bila jitihada nyingi.
9. Utajielimisha kuhusu fedha
Kusoma makala hii ni mwanzo mzuri. Endelea kujielimisha kupitia YouTube, blogu, podikasti, na semina za kifedha. Fuata akaunti za mitandao ya kijamii zinazofundisha kuhusu fedha na wafuasi wa elimu ya kifedha hapa Tanzania.
10. Utaomba msaada unapouhitaji
Ukiona hali ya kifedha imekushinda, usisite kuomba msaada. Wasiliana na mshauri wa kifedha aliyeidhinishwa ili kupata ushauri juu ya bajeti, mipango ya usimamizi wa madeni, na uwekezaji.
Hakuna sababu ya kuhisi peke yako au kusongwa msaada upo.