Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pinda anatafuta utajiri kwa kuuza embe, wewe unafanya nini? – (1)

Muktasari:

Imani ya wengi ni kwamba itokee muujiza ambao kwa lugha ya mitaani huita ‘zari’ ambalo ni la fedha nyingi ambayo itabadilisha maisha yake kwa sekunde moja.

Siku hizi vijana wengi ambao wako tu mitaani bila shughuli wakidai kuwa hawana ajira.Hawa utawaona vijiweni ama wakizurura tu mitaani kuanzia asubuhi hadi jioni.

Imani ya wengi ni kwamba itokee muujiza ambao kwa lugha ya mitaani huita ‘zari’ ambalo ni la fedha nyingi ambayo itabadilisha maisha yake kwa sekunde moja.

Zari hilo laweza kuwa ni kupata fedha nyingi ya ghafla kwa mpango au au wenyewe huuita ‘dili’, ambayo hata ukimuuliza hajui ni ya namna gani.

Ukichunguza kwa makini utakuta vijana wa namna hiyo ni wale wavivu na wenye matarajio makubwa kuliko uwezo wao.

Hubaki wakitamani kufikia maisha ya watu fulani wenye mafanikio kimaisha tena kwa njia za mkato.

Hata ukimpa wazo la kufanya bishara ndogondogo kwa malengo ya kufikia ndoto hiyo hatafanya kwa kuwa anahitaji mafanikio ya haraka.

Malengo yake ni apate utajiri wa maramoja, ndoto ambayo vijana hubaki wakizifikiria vijiweni na mitaani na inapokuwa hawafanikiwi, hujiingiza kwenye uhalifu wa aina mbalimbali kama vile wizi, utumiaji na uuzaji wa dawa za kulevya.

Hayo yote hutokea kutokana na kutokuwa na mipango ambayo itawafikisha kwenye ndoto zao. Vijana kama hao wanapaswa kujifunza kwamba hata watu walioajiriwa huwa na mtazamo wa kustaafu, huku wakiwa na miradi ya ujasirimali ambayo itawasaidia baadaye.

Kumbe mipango mizuri ya ujasirimali, hata kama ukiwa ni wa kuuza karanga au genge, kwa kuanzia Sh50,000, unaweza kumfanya mtu kuwa tajiri anayemiliki mamilioni, miaka michache baadaye.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ni mmoja wa waajiriwa ambaye katika jamii aweza kuonekana hata baada ya kustaafu kazi ataishi maisha bila wasiwasi.

Hata hivyo, pamoja na hali hiyo, yeye binafsi anaona ni vyema akijiwekea mkakati wa kuaminika ambao utampatia kipato.Hakuanza na biashara kubwa bali ujasirimali katika kilimo cha embe.

Pinda anasema alijifunza ujasirimali jinsi unavyoweza kuinua mtu kuwa na kipato kikubwa kwa wauzaji wadogo wa maziwa katika nchi mbalimbali duniani.

Anabainisha kuwa wanaojikita katika ujasiriamali duniani ndiyo wanaokuwa na mafanikio kimaisha.

“Wamekuwa na mafanikio makubwa kwa sababu wanaweza kujiajiri na kujiingizia kipato kikubwa tofauti na kazi za kuajiriwa ambazo zina ukomo,” anasema Pinda.

Kwa sababu hiyo, Pinda anaamini kuwa ujasiriamali wa aina yoyote ni muhimu katika kujenga mazingira mazuri zaidi ya kipato.

Pinda anasema, ameanza ujasiriamali wa kilimo cha kisasa cha embe, kwa lengo la kuwa mfanyabiashara mkubwa katika fani hiyo.

Anasema ameanza kilimo hicho miaka michache iliyopita na tayari amefaidi matunda kwa kuuza embe moja kwa Sh1,000.

Anasema mradi huo ni miongoni mwa ujasiriamali wake ambao anaamini unaweza kumfanya awe na kipato kikubwa miaka ijayo.

Anasema biashara hiyo, inamwingizia faida kubwa ambayo anaona ni nzuri kuliko hata kuajiriwa na kutegemea kulipwa mshahara.

Anasema Watanzania hawana budi kujifunza mbinu za ujasiriamali na wanaweza kujikuta wanaukimbia umaskini na kuwa kwenye ngazi ya matajiri.

Anasema amekuwa akijitahidi kujiingiza kwenye shughuli ndogondogo za kijasiriamali ambazo hata mtu wa kawaida anaweza kuzifanya, kinachotakiwa tu ni kuwa na moyo wa dhati.

“Nina shamba langu Dodoma, kwa sasa nina ng’ombe wa maziwa wanaofikia 30 na kuku 3,000. Nikiuza kila kuku mmoja Sh15,000 nina fedha nyingi. Nimelima embe, ninauza Sh1,000 kila moja. Ukija kwangu utanunua, utakula na hutamaliza,” anatamba Pinda.

Waziri Mkuu anasema kuwa miche yake ya maembe aliyonayo ni ya kisasa na kwamba kwa msimu mmoja kila mwembe huzaa embe 300, hivyo anapata kipato kizuri.

Kwa hesabu za haraka, kila mche mmoja wenye embe 300 humwingizia Sh300,000, wakati kuku 3,000 kwa kila mmoja Sh15,000, anavuna Sh45,000,000.

Waziri Mkuu anaonyesha kuwashangaa vijana na wasomi wanaobaki nyuma katika kujiongezea kipato na kuwashauri kujiingiza kwenye ujasiriamali. “Vijana wetu wasomi, hivi sasa ukimwambia afuge kuku na kukanyaga kinyesi chao, anakutazama vibaya kidogo, jambo ambalo lazima sasa tubadilike,” anasema Pinda.

Hata hivyo, anasema mfumo wa elimu uliopo nchini unaweza pia kuwa ni tatizo, kutokana na kuwaandaa vijana kufanya kazi za kuajiriwa maofisini mabadala ya kupenda kujiajiri.

Mawazo ya Pinda yanashabihi hali halizi ya maisha ya watu wengi katika jamii ambao wameweza kuwa matajiri baada ya kusota maisha ya ujasirimali katika hali ngumu, ya kipato kidogo, nidhamu ya matumizi na mipango mizuri ya biashara.

Mitaani kuna vijana wasomi lakini wanatangatanga hawajui la kufanya kwa sababu wanadai hawana mitaji ya kujiingiza kwenye ujasirimali.

Mkurugenzi wa kampuni ya Excel ambaye pia ni mshauri wa mambo ya biashara, Deogratius kilawe anasema ni mawazo finyu kukaa mitaani ukitafuta ajira au ukilalamika huna mtaji wa kuanzia.

Anema watu wengi huamini kuwa lazima kuwa na fedha ndio uanzishe biashara na ndiyo sababu yao kuu ya kukaa bila kujishughulisha.

Ukweli ni kwamba mtaji ni moja ya kitu muhimu katika kuanzisha biashara, lakini wengi wao huwa na mawazo au mipango ya kuwa na fedha nyingi, ndiyo aingie kwenye biashara.

Anasema mtu hapaswi kukaa bila kazi kwa sababu hana mtaji mkubwa. Hata fedha kidogo anaweza kuanzia na kidogokidogo zinamzalishia na kuwa na biashara kubwa.

Kilawe anasema zipo aina nyingi za biashara na miongoni kuna ambazo hazihitaji mtaji au kama unahitajika ni kidogo lakini baada ya muda unapata mafanikio makubwa.

Anatoa mfano akisema mfanyabiashara anaweza kutoka kwa kishindo sana kwa kuanza ukiwa huna kitu.

Anasema kinachohitajika ni kufanya kazi kwa juhudi na kupata ushauri juu ya mpango bora wa kufanikisha ule ujasiriamali ambao umekusudia kuutekeleza.

Biashara nyingi zisizohitaji mtaji mkubwa, Kilawe anazitaja kuwa ni upande wa kutoa huduma.

“Katika biashara ya huduma, unaweza kufanikiwa kutengeneza faida kubwa na kutokea hapo ukaanza kufikiria kuanza kukodi ofisi yako, kuajiri watu wengine na kadhalika,” anasema Kilawe.

Lakini anaonya: “Ingawa ni rahisi kutoka ukiwa upande wa huduma lakini inahitaji ujuzi au weledi fulani hivi ili uweze kufika kilele cha mafanikio. Hapa simaanishi lazima uwe umesoma chuo kikuu maana ujuzi au utaalamu wa jambo halihusiani na digrii ya chuo kikuu.”

Anasema elimu hiyo anaweza kuipata kwa kuhudhuria semina na warsha mbalimbali au kufundishwa na mtu mwenye ujuzi husika na baada ya kupata ujuzi ambao baadaye ataufanyia kazi katika maisha yako ya kawaida ya kila siku na kuwa bora kwa upande huo.

Bila shaka mtu yeyote ambaye maisha yake yamekuwa ni kuzurura mitaani na kukaa vijiweni kwa maelezo hana ajira, maelezo ya Pinda na Kilawe, yanaweza kuleta mapinduzi kimaisha kwa kupata mwelekeo bora wa kujiajiri.

Wiki ijayo, sehemu ya pili ya makala hii itaelezea kuhusu watu walioanza na biashara ndogondogo lakini kwa sasa ni matajiri. Hapa mtu aweza kujifunza namna ya kuwa tajiri au kufikia maisha bora yenye ustawi, kwa kuanzia na ujasiriamali mdogo.