Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Heche apeleka 'No reforms, No election' Chato

Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni ya 'No reforms, No election' katika Kijiji cha Muganza Wilaya ya Chato. Picha na Peter Saramba

Muktasari:

  • Chadema inaendesha kampeni ya 'No reforms, No election' kudai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi.

Chato. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) (Bara), John Heche amefika Wilaya ya Chato kupeleka kampeni ya chama hicho ya No reforms, No election.

Heche anayeongoza timu ya chama hicho katika ziara ya Kanda ya Victoria ameingia Chato leo Mei 10, 2025 kwa kuhutubia mkutano wa kwanza katika Kijiji cha Muganza ambako amewaomba wakazi wa eneo hilo na Watanzania wote kuunga mkono kampeni ya kudai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi unaorejesha mamlaka kwa umma.

Amesema mapambano ya Chadema ya kudai mabadiliko yanalenga kujenga Taifa ambalo mamlaka yote ya nchi yako mikononi mwa wananchi, huku viongozi wakiwajibika kwa umma tofauti na sasa ambapo viongozi wanafanya watakalo bila hofu.

"Hapa Muganza mna Ziwa Victoria, lakini hamnufaiki ipasavyo kutokana na kukosekana kwa sera na mipango ya kuwainua wananchi kiuchumi: wananchi tuungeni mkono kudai mabadiliko tubadilishe mfumo huu," amesema Heche

Akifafanua, kiongozi huyo amesema sheria na mfumo uliopo hauweki sawa uwanja wa ushindani kisiasa kwa sababu mchakato wote wa uchaguzi unasimamiwa na kuendeshwa na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

"Mfano hai ni Tume Huru ya Uchaguzi ambao miongoni mwa wajumbe watano siyo tu kada wa CCM, bali pia alikuwa kiongozi wa juu wa chama hicho," amesema Heche

Mwenyekiti wa Baraza la vijana wa Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Muganza Wilaya ya Chato. Picha na Peter Saramba.

Amesema Chadema inachopigania ni haki na usawa kwa wagombea na vyama vyote vya siasa.

"Chadema hatupiganii mabadiliko ili tupate upendeleo. Hapana! Tunataka ushindani wenye haki na usawa kwa wote na kura za wananchi ziheshimiwe kwa anayepata kura nyingi kutangazwa," amesema makamu mwenyekiti huyo

Mbunge huyo wa zamani wa Tarime Vijijini amesisitiza msimamo wa yeye na viongozi wenzake kuendelea na kampeni ya kudai mabadiliko kupitia kampeni ya 'no reforms, no election' bila kujali  vikwazo wanavyokutana navyo.

"Mwenyekiti Tundu Lisuu yuko mahabusu kwa kesi ya uhaini; lakini  bado tuko imara  tunaendeleza kampeni ya kudai mabadiliko. Hata wakinikamata mimi pia, viongozi wengine wataendeleza kampeni ya no reforms, no election" amesema Heche

Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni ya 'No reforms, No election' katika Kijiji cha Muganza Wilaya ya Chato. Picha na Peter Saramba



Akizungumzia ajira kwa vijana, Heche amesema sera zilizopo za kukabidhi rasilimali na vyanzo vikuu vya mapato ya nchi ikiwemo bandari, viwanja vya ndege na migodi ya madini mikononi mwa wageni haiwezi kutatua tatizo la ajira kwa sababu faida yote inaenda nje ya nchi.

"Chadema ikiingia madarakani itahakikisha inaweka mazingira bora yatakayowawezesha Watanzania kumiliki na kuendesha njia kuu za kiuchumi ikiwemo migodi ya madini. Tunachoomba ni umma kutuunga mkono kudai mabadiliko yatakayorejesha mamlaka kwa wananchi," amesema.

Akihutubia mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila amewasihi vijana kote nchini kuunga mkono madai ya mabadiliko ya mfumo utakaowahakikishia kesho yao.

"Vijana wa Tanzania tuamke kwa kuungana kudai mabadiliko yatakayotuhakikishia maisha bora sasa na baadaye sisi na vizazi vyetu. Vijana ndio chachu ya mabadiliko katika jamii na Taifa," amesema Mahinyila