Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mapya mvutano wa viongozi, wanachama Chadema

Karagwe/Dar. Wakati baadhi ya makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiendelea kujivua uanachama, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche akiwarushia tuhuma hizo kwamba “wamefika bei”.

Tuhuma hizo ni mwendelezo wa majibizano kati ya viongozi wa Chadema na wanachama wao ambapo kila upande unaukosoa mwingine, hivyo kukosekana kwa maelewano baina ya pande mbili, jambo linalotajwa kuwa sababu ya wengine zaidi kujivua uanachama.

Kundi la makada 55 (G55) lilijitokeza kueleza kutokubaliana na msimamo wa Chadema wa kutaka kuzuia uchaguzi kupitia kaulimbiu ya “No reforms, no election” wakitaka chama hicho kishiriki uchaguzi, ili kuendelea kupigania mageuzi katika mifumo ya uchaguzi, jambo ambalo uongozi haukuliafiki.

Katikati ya malumbano hayo, Mei 7, mwaka huu, viongozi watano waliokuwa wajumbe wa sekretarieti ya Chadema katika uongozi uliomaliza muda wake chini ya aliyekuwa mwenyekiti, Freeman Mbowe, wakatangaza kukihama chama hicho na taarifa za ndani zinaeleza wakati wowote watatua kwenye Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Viongozi hao ni pamoja na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Benson Kigaila na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu ambao walidai uwepo wa ubaguzi, udikiteta na ukiukwaji wa katiba ya chama unaofanywa na uongozi mpya.

Mbali na hao, yumo pia aliyekuwa Katibu wa Bawacha Taifa, Catherine Ruge, aliyekuwa katibu wa sekretarieti, Julius Mwita na aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Uenezi, John Mrema, ambao walisisitiza kwamba kuondoka kwao si mwisho wa mapambano, bali wanatafakari jukwaa lingine la kwenda.


Kauli ya Heche

Akiwa Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera juzi, Heche aliwashukia makada hao waliotangaza kujivua uanachama akidai kwamba wamefika bei.

Akihutubia mikutano ya hadhara ya kampeni ya No reforms, no elections kwa nyakati tofauti katika wilaya za Kyerwa na Karagwe, Heche alisema baadhi ya makada hao wamefika bei baada ya kupokea ahadi ya nafasi za uongozi, fedha na vifaa vya kampeni katika uchaguzi mkuu ujao.

Mbunge huyo wa zamani wa Tarime Vijijini, alitaja sababu nyingine iliyowakimbiza baadhi ya waliokuwa makada hao kuwa ni hasira ya kukosa nafasi za ujumbe kwenye sekretarieti mpya ya Chadema.

“Baadhi ya waliotangaza kujiondoa Chadema wamedumu kwenye sekretarieti kwa miaka kati ya 17 hadi 22; sasa uongozi mpya umewateua wana Chadema wengine kushika nafasi hizo imekuwa nongwa,” alisema Heche.

Aliwataka Watanzania kutokatishwa tamaa na wanaofika bei na kusaliti imani ya kupigania mabadiliko ya kimfumo kwenye uongozi wa nchi kwa sababu viongozi na makada wa Chadema waliosalia wataendeleza mapambano bila kuchoka wala kurudi nyuma.

Alisema tayari wanazo taarifa kuwa viongozi na makada kadhaa wa Chadema wanashawishiwa kujivua uanachama kwa ahadi mbalimbali ikiwemo fedha na vyeo.

“Sisi hatutatetereka wala kurudi nyuma katika mapambano ya kudai haki, usawa kwa wote na ustawi wa Watanzania," alisema Heche.

Alisema milango iko wazi kwa wote wanaosukumwa na tamaa ya nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao waondoke kwa sababu fursa hiyo hawataipata kupitia Chadema, iwapo hakutafanyika mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi unaotoa fursa sawa kwa vyama na wagombea wote.

“Tuna taarifa baadhi ya walioondoka wamepata ahadi ya kusaidiwa kifedha na vifaa, yakiwemo magari na pikipiki ili wagombee ubunge.

“Sasa wajiulize iwapo kweli watashinda baada ya kuhamia vyama vingine kwa sheria na mfumo huuhuu, kama hawakuweza wakiwa ndani ya Chadema inayoungwa mkono na Watanzania wengi,” alisema Heche.

Alisema licha ya mbinu zinazofanyika kuwadhoofisha, viongozi wa Chadema hawatarudi nyumba katika kampeni ya No reforms, No election hadi mabadiliko yatakapofanyika.

"Sisi hatutaki upendeleo, bali tunachohitaji ni haki na usawa katika uwanja wa siasa, kutoa fursa kwa Watanzani si tu kuwachagua viongozi wanaowataka, bali pia nguvu ya kuwawajibisha wasipotimiza wajibu na ahadi zao za uchaguzi,” alisema Heche.


Mrema ajibu mapigo

Akizungumzia madai ya wao kufika bei, msemaji wa kundi la makada waliojivua uanachama wa Chadema maarufu kama G55, John Mrema alisema tuhuma hizo haziwatendei haki kwa sababu wameeleza wazi kilichowatoa Chadema.

“Makamu Mwenyekiti wa Chadema anatukosea sana kusema tumefika bei kusaliti imani yetu katika haki na usawa; ni vema viongozi wa Chadema wakubali matatizo yaliyopo ndani ya chama chao na kuyatafutia majawabu,” alisema Mrema.

Huku akionyesha msisitizo, Mrema alisema: “Sisi tulikuwa tunadai haki ya kuingia kwenye uchaguzi ili tushinde na kuleta mabadiliko kwa sababu hatuwezi kuleta mabadiliko tukiwa nje ya uongozi wa dola. Tumeondoka kwa sababu Chadema imejigeuza kuwa chama cha harakati kisichoshiriki uchaguzi.”

Msemaji huyo wa zamani wa Chadema, ametaja sababu nyingine iliyowafanya wajivue uanachama wa chama hicho kuwa ni chuki na ubaguzi dhidi ya makada waliomuunga mkono Mwenyekiti wa zamani, Freeman Mbowe wakati wa uchaguzi mkuu wa chama Januari 21, 2025.

“Sisi hatujapewa ahadi yoyote kutoka kwa mtu yeyote, tumeondoka Chadema kwa sababu ya chuki na ubaguzi dhidi ya tuliomuunga mkono Mbowe,” alisema Mrema.

Alisema uchaguzi wowote lazima uwe na makundi ya wagombea, hivyo walioshinda walipaswa kuyaunganisha makundi yote kujenga na kurejesha umoja, kazi ambayo anadai uongozi mpya chini ya Tundu Lissu haujafanya.

“Badala ya kukiunganisha chama, hivi sasa yeyote aliyemuunga mkono Mbowe anaonekana adui na msaliti,” aliongeza.

Kuhusu madai ya kuwarubuni makada wengine kuondoka Chadema, Mrema alisema: “Wao (viongozi wa Chadema) wana hofu ya watu kuondoka kutafuta fursa za kugombea katika uchaguzi ujao. Chadema ina madiwani 85 ambao walishinda uchaguzi mwaka 2020; hawa bado wanapendwa na wapigakura wao, watakwenda vyama vingine kutafuta fursa ya kuendelea kuwawakilisha wananchi.”


Wengine wajiengue

Makada wengine watano wa Chadema wakiongozwa na aliyekuwa katibu wa kundi la G55, Edward Kinabo wametangaza kujivua uanachama wa Chadema, hivyo kufanya idadi ya waliojiondoa Chadema kufikia 10.

Wengine walioungana na Kinabo ni aliyekuwa miongoni mwa mameneja wa Mbowe katika uchaguzi wa ndani ya chama hicho na mjumbe wa kamati kuu ya Chadema Wilaya ya Temeke, Eliya Gregory.

Vilevile, yumo Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) Wilaya ya Ilala, Rachel Kitamkadala na wajumbe wa mkutano mkuu Grace Ngola na Salma Sharif.

Akizungumzia uamuzi huo, Kinabo alisema gari la Chadema limechoka, halina “spea mpya”, hivyo wanakwenda kupanda gari lingine.

“Natangaza rasmi kuagana na gari la Chadema, halina matumaini mapya tena, kwa umoja wetu, tunaenda kwenye chama kingine, tunaenda kupanda gari lingine jipya, tutaunganisha nguvu zetu tulizotokana nazo huku na kukifanya kuwa kikubwa,” alisema Kinabo.

Alisema ndani ya chama hicho hakuna heshima tena iliyojengeka kwa muda mrefu, lakini chuki za wenyewe kwa wenyewe zimetamalaki na zimekuwa kubwa kuliko mifumo kandamizi inayofanywa na dola na washindani wao wa kisiasa.

“Vita ya ndani imekuwa kubwa kuliko ya nje na yamekuwa yakifanyika hadharani na raia wamekuwa wakitushangaa kila uchao, chuki na makundi yamekuwa yakiibuka kiasi kwamba hatuwezi kurejesha upendo na heshima ile tuliyoijenga kwa wivu mkubwa,” alisema Kinabo.

Kada wa Chadema, Edward Kinabo na wenzake wakiwa wameshikana mikono ikiwa ni ishara ya umoja, baada ya kutangaza kujivua uanachama wa chama hicho leo Ijumaa Mei 9, 2025 jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Kwa upande wake, Gregory alisema hakuna masika isiyokuwa na mbu, wanaondoka wamechoka kuishi kama yatima na kuendelea kutengwa na uongozi mpya ambao hautaki kuunganisha wanachama.

“Najivua vyeo vyangu vyote ndani ya Chadema, nahama rasmi na nautangazia umma, Chadema si jukwaa sahihi la kidemokrasia, tunaenda kutafuta jukwaa lingine zuri na bora,” alisema Gregory.