Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wenje 'awatosa’ Heche, Mnyika no reforms, no election Kagera

Muktasari:

  • Katika uchaguzi wa ndani wa Chadema uliofanyika Januari 21, 2025, Wenje aliyegombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara) na kushindwa na John Heche alimuunga mkono aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye pia aliangushwa na Tundu Lissu katika nafasi ya uenyekiti.

Bukoba. Amekacha! Huo ndio usemi wa vijana wa kileo unaoweza kutumika kueleza hatua ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Victoria, Ezekhia Wenje kutoonekana katika mikutano ya kampeni ya chama hicho ya "No reforms, No election" inayoendelea kwenye kanda yake.

Tangu jana Mei 8, 2025, viongozi wakuu wa Chadema wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti (Bara), John Heche na Katibu Mkuu, John Mnyika wako mkoani Kagera kwenye mwendelezo wa kampeni ya chama hicho ya kudai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi kabla uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2025.

Akizungumza na Mwananchi leo Mei 9, 2025, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi amesema Wenje alipaswa kuongoza msafara wa Katibu Mkuu, Mnyika katika mikutano ya hadhara kwenye wilaya za Biharamulo na Muleba.

"Tulikubaliana Mwenyekiti (Wenje) aongozane na Katibu Mkuu (Mnyika) katika mikutano ya hadhara ya kampeni ya no reforms, no election kwenye wilaya za Biharamulo na Muleba na mimi niwe na Makamu Mwenyekiti (Heche) katika Wilaya za Misenyi na Karagwe. Lakini hadi leo hajaonekana." amesema Obadi

Amesema tangu jana Alhamisi hadi leo Ijumaa Mei 9,2025 amepiga simu za Mwenyekiti wake huyo kufahamu kilichomzuia kujiunga kwenye kampeni na mkitano inayofanyika kwenye kanda yake, bila mafanikio.

"Hapokei simu zangu tangu jana; sijui jambo gani limemtokea," amesema Obadi

Jitihada za Mwananchi kumpata Wenje kuzungumzia kutoonekana kwenye mikutano ya chama chake yanayoendelea kwenye kanda yake hazijafanikiwa baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa.

Hata ujumbe mfupi wa maneno aliotumiwa pia haukujibiwa kwa njia ya simu pia haukujibiwa.

Akizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika amesema; "Kwa kweli sijui kwanini Wenje hajaonekana hadi leo, labda umpigie simu yeye mwenyewe kujua kilichomsibu,"

Huku akizungumza kwa tahadhari, Mnyika amesema Mei 8, 2925, alizungumza na Wenje kwa njia ya simu na akamjulisha kuwa alichelewa kutoka jijini Dar es Salaam ndio maana hakuweza kuwahi mikutano ya wilayani Biharamulo huku akiahidi kuungana naye kwenye mikutano ya wilayani Muleba leo Ijumaa Mei 9, 2025.

"Hadi tunamaliza mikutano ya Muleba hakutokea. Hata mkutano wa jioni Bukoba mjini pia hajaonekana. Kwa kweli hatuna taarifa ni wapi alipo na nini kimemsibu," amesema Mnyika

Kampeni ya Chadema ya No reforms, No election inaendelea katika Kanda ya Victoria inayoundwa na mikoa ya Kagera, Geita na Mwanza.

Awali, akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kashai mjini Bukoba, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema alirusha kijemba kwa makada wa chama hicho wanaokusudia kujivua uanachama akiwataka kuharakisha ambapo alitaja jina la Wenje bila kufafanua.

"Chadema ni mpango wa Mungu; chama hiki hakiwezi kutetereka kwa sababu wapo watu wamepanga kutoka. Nawasihi wote wenye nia ya kuondoka wafanye hivyo haraka. Hata Wenje, Mwenyekiti wa Kanda ya Victoria akitaka kuondoka afanye hivyo haraka," amesema Lema.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Chadema Januari 21, 2025, Wenje aliyegombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti (Bara) na kuangushwa na Heche amekuwa akionekana kwa nadra kwenye matukio na shughuli za kisiasa za chama hicho.

Katika mchakato wa uchaguzi huo, Wenje alimuunga mkono aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye pia aliangushwa na Tundu Lissu.

Yapo majina ya vigogo wakubwa ndani ya Chadema wamekuwa wakihusishwa kuwepo ndani ya kundi la G55. Baadhi ya wajumbe wa kundi hilo akiwemo msemaji wao, John Mrema wametangaza kujivua uanachama wa Chadema wakitaja sababu kadhaa za kufikia uamuzi huo.

Mbele ya mkutano wa hadhara uliofanyika Mei 7, 2025, Mrema akiwa pamoja na waliokuwa Manaibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu (Zanzibar) na Benson Kigaila (Bara) walitaja chuki dhidi ya waliomuunga mkono Mbowe wakati wa kampeni kuwa miongoni mwa sababu za kujivua uanachama.

Wengine waliojivua uanachama siku hiyo ni waliokuwa wagombea ubunge uchaguzi wa 2020 na wajumbe wa Sekretarieti ya zamani ya Chadema, Julius Mwita na Catherine Ruge.