Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Padri Felician Nkwera afariki dunia

Padri Felician Nkwera enzi za uhai wake

Muktasari:

  • Waamini wakusanyika Kituo cha Maombezi cha Mama Bikira Maria (Marian Faith Healing) kuomboleza.

Dar es Salaam. Muasisi wa Kituo cha Maombezi cha Mama Bikira Maria (Marian Faith Healing), Padri Felician Nkwera (89) amefariki dunia.

Waamini wamekusanyika katika kituo hicho kilichopo Ubungo Riverside, Dar es Salaam leo Mei 9, 2025 kuomboleza.

Amefariki dunia saa mbili usiku wa jana Mei 8, 2025 katika Hospitali ya TMJ alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya presha kushuka.

Mwenyekiti wa Huduma ya Maombezi kituoni hapo, Deogratias Karulama akizungumza na Mwananchi leo Mei 9, 2025 amesema Padri Nkwera alianza kujihisi vibaya jana Mei 8, asubuhi akiwa kituoni hapo ambako pia ni nyumbani kwake.

Amesema alipopelekwa hospitalini madaktari walipompima walisema presha yake ipo chini, lakini jioni hali ilibadilika wakampeleka hospitali iliyopo Kinondoni walikoelezwa presha ilikuwa sawa hivyo waaanza safari kurejea nyumbani lakini njiani hali ilibadilika ndipo wakampeleka Hospitali ya TMJ alikofikwa na umauti.

Padri Nkwera aliwahi kuhudumu Kanisa Katoliki kabla ya kutengwa na uongozi wa kanisa hilo.

Katika kituo hicho waamini wamekusanyika kufanya ibada, baadhi wakilia.

Kabla ya ibada kuanza, Karulama alitoa taarifa kuhusu kifo cha Padri Nkwera.

"Baba alitudanganya sana kwenye macho, kila tulivyomuambia kula alisema tusubiri kwanza Papa apatikane. Kwa bahati nzuri alipotangazwa kupatikana ndipo naye alipozima pumzi zake," amesema.

Amesema: "Jana wakati tunatoa taarifa wengi walikuwa wanalia kwamba kwa nini hatukuwataarifu. Ukweli ni kwamba mwenyewe alituaga lakini hatukujua na kama mnakumbuka kauli yake ya mwisho alikuwa akituambia mkitenda dhambi mtakufa.

"Na kauli yake ya kujirudia kila wakati alikuwa akisema alipokwenda ni pazuri na haya tunayoishi tumekopeshwa tu, hivyo cha msingi na kikubwa ni kushika yale aliyokuwa anatuelekeza,” amesema.

Amesema katika siku za hivi karibuni alisisitiza kuliombea Taifa.

"Hivyo kwa ajili ya kumuenzi yale yote alipanga kufanya, tufanye. Aliwahi kusema jaribuni kusikia kwa ninayoeleza msije mkasema sikuwaambia, liombeeni Taifa hasa tunapokwenda kwenye uchaguzi mwaka huu," amesema. Amesema ratiba ya mazishi inasubiri ndugu za marehemu ambao wengine wapo nje ya nchi.


Anavyokumbukwa

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Aladin Mutembei amesema wengi wa wataalamu wa lugha ya Kiswahili wamepita katika mikono ya Padri Nkwera.

Amesema ametunga vitabu zaidi ya saba vya kufundishia lugha hiyo na kilichokuwa maarafu ni kile cha Lugha ya Kiswahili kwa Wanafunzi wa Sekondari na Vyuo.

Amesema vitabu hivyo vilisaidia kuwapika walimu wengi wa vyuo pia wanaofundisha somo hilo.

"Sifa nyingine aliyojaliwa Padri Nkwera alijua vizuri lugha hiyo upande wa fasihi na kwa hiyo tuliweza kupata madini yote kwake," amesema Profesa Mutembei.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Musa Hans  amesema Padri Nkwera ni kati ya wanafasihi waliotaka lugha hiyo ivuke mipaka.

"Hata leo ninavyozungumza hapa ana mchango mkubwa wa lugha hii kuzungumzwa katika mataifa mbalimbali duniani, hivyo tuliobaki tumuenzi kwa kuhakikisha lugha hiyo inaendelea kufika mbali," amesema.