Wanasiasa wamekwamisha ‘kesi’ ya utakatifu wa Nyerere

NyerereBaba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere akizung-umza na Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa John Paul II (sasa Mtakatifu John Paul II) alipotem-belea Tanzania mwaka 1990. Kulia ni mkewe, Mama Maria Nyerere. Picha ya Maktaba
Muktasari:
- comMwalimu Julius Nyerere alizaliwa Aprili 13, 1922 katika Kijiji cha Butiama, Mkoani Mara.Baada ya elimu yake ya juu aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Makerere.
- Uganda na baadaye Edinburgh, Uingereza, alifundisha katika Shule ya Sekondari Pugu kabla ya kuingia katika siasa.
- Alikuwa Rais wa kwanza wa Tanzania hadi alipomwachia Ali Hassan Mwinyi mwaka 1985.Alifariki dunia tarehe ya kama ya leo, Oktoba 14 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, London Uin-gereza alipokuwa amelazwa kwa ugonjwa wa kansa ya damu.
Mchakato kuhusu kumtangaza mtakatifu Julius Nyerere ulizinduliwa na Jimbo Katoliki la Musoma mwaka 2006. Je, umefikia wapi?
Jibu la swali hili nisentensi moja tu kama tutakavyoona.“Mchakato” wa utakatifu ni jambo la kihistoria, hivyo unaeleweka kwa kuieleza historia yake.
Ukristo ni dini iliyochukiwa na serikali ya Roma, hivyo Wakristo waliteswa, waliuawa ili kuuangamiza. Hata hivyo, Wakristo hawakutikiswa na serikali, baadhi ya waliouawa wakatangazwa kwamba ni “watakatifu wafia dini”.
Mwishowe Ukristo uliishinda serikali na ikajikuta ina utangaza kuwa dini rasmi ya Ulaya. Baada ya hapo kukaibuka utakatifu uliopatikana kwa kuishi maisha ya kuitetea imani bila ya kuuawa.
Hadi leo kuna aina hizi mbili za watakatifu, yaani “wafia dini”na walioishi maisha ya kiimani.
Nani hutangaza utakatifu
Utakatifu wa hao watu ulitangazwa na waumini wenzao. hawakuhitaji Papa au askofu wa jimbo awatangazie. Mwaka 604, waumini wa Jimbo la Roma walimtangaza Gregory kuwa mtakatifu saa chache baada ya kifo chake.
Waumini pia walipenda
kuhamisha masalia ya marehemu na kuyapeleka mahali panapofikiwa na wengi. Kwa mfano, masalia ya Klara Bernadeta wa Songea aliyefariki mwaka 1950 yalihamishwa mwaka 2012.
Hata hivyo ilitokea waumini wakaanza kuvuruga utaratibu. Ilipofika hapo akabaki askofu tu ndiye anayetangaza na Papa akawa anatangaza watakatifu kwa jimbo la Roma pekee.
Lakini mataifa hayakuacha desturi ya kuamiani kwamba mtu fulani kwa matendo yake ni mtakatifu. Desturi hii inaitwa “cult” na inapodumu kwa miaka mingi, kanisa huweza kumtangaza mtu husika kuwa mtakatifu.
Papa aanza kuhusishwa
Kabla ya mwaka 993 iliwezekana mtakatifu asikubalike katika jimbo jingine. Hivyo kuanzia mwaka 993 maaskofu waliomba Papa awe anatangaza watakatifu wa kila jimbo ili wajulikane duniani kote.
Mwaka 1588, Papa aliunda “idara ya utakatifu” imsaidie, ikawa inauendesha “mchakato” kama kesi. Hadi leo, kanisa linapoanzisha tunachokiita “mchakato”, linakuwa limefungua kesi inayokaribisha wanaopinga na wanaokubali kwamba marehemu fulani ni mtakatifu.
Nani anaanzisha mchakato
Je, “mchakato” wa utakatifu ukoje na unaanzishwa na nani? Mtu yeyote unaweza kutuma ombi la kuuanzisha. Jimbo litakalouendesha ni lile alilofia marehemu.
Askofu wa Jimbo hilo akilikubali ombi husika anafuata utaratibu utakaohitimishwa kwa kutuma ombi kwenye “idara ya utakatifu” kule Roma.
Idara ikikubali inamruhusu askofu kuanza “mchakato” jimboni mwake. Askofu anaunda timu ya watafiti itakayopokea mashahidi wenye taarifa za marehemu. Hapo marehemu anaanza kuitwa “Mtumishi wa Mungu”.
Timu ya utafiti ikimaliza kazi yake, askofu anaufunga “mchakato” jimboni ili zianze hatua za idara ya kule Roma, kama ambavyo Januari 14, 2013 jimbo la Songea liliufunga “mchakato” wa Klara Bernadeta.
Pale Roma ripoti ya askofu ikionekana ni safi, inaandikwa ripoti nyingine iitwayo “positio” inayoonyesha marehemu alivyouawa au alivyoishi kwa kuitetea imani.
Ripoti hiyo inakaguliwa na maprofesa wa historia. Ikishakubaliwa inakaguliwa na maprofesa wa teolojia ya Ukatoliki.
Kama “mchakato” una muujiza inayomhusisha marehemu inatayarishwa ripoti ya wataalamu wa ugonjwa uliopona kimiujiza.
Ripoti hizi zinapelekwa kwa makardinali na maaskofu wa ile idara. Hawa wakiikubali ndipo kardinali anayeongoza idara anaipeleka kwa Papa.
Papa naye anaikagua na akiikubali ndipo anampa marehemu hadhi iitwayo “Venerable”. Kazi kubwa huishia hapa, kwani mtu akiwa “Venerable” kanisa linaruhusu matendo yake kuigwa.
Mwenyeheri na mtakatifu
Baada ya hatua hiyio, kinachofuata ni kusubiri miujiza. Roma ikithibitisha muujiza wa kwanza unaohusihwa na merehemu, “Venerable” anatangazwa kuwa “Mwenyeheri”. Muujiza wa pili ukitokea unamfanya atangazwe “Mtakatifu”.
Ipo tofauti ndogo kati ya “Mwenyeheri” na “Mtakatifu”. “
Mwenyeheri anatumika sehemu chache duniani wakati “mtakatifu” anatumika duniani kote.
Kwa ufupi kihistoria ndivyo mchakato ulivyo. Lakini hata leo, Papa hazuiwi kumtangaza mtu mtakatifu ndani ya dakika chache baada kifo chake.
Mchakato wa Nyerere
Julius Nyerere alifia katika Jimbo Katoliki la Westminster, Uingereza. Kama ndani ya siku moja Papa John Paul II angemtangaza utakatifu, basi tungekuwa tunamwita “Mtakatifu Julius wa Westminster.
Hivyo, askofu Justin Samba aliomba ruhusa Roma iuhamishe “mchakato” wake kutoka Westminster kwenda Musoma na aliruhusiwa Mei 13, 2005.
Misa iliyozindua “mchakato” ilifanyika Januari 26, 2006 parokiani Butiama jimboni Musoma. Ilipofika Mei 02, 2014 ukahamishiwa Jimbo Kuu la Dar es Salaam uliko hadi leo.
Umefikia wapi
Sasa tujibu lile swali, “mchakato wa utakatifu kwa Julius Nyerere umefikia wapi”? Jibu ni kwamba kwa miaka 12 mchakato huo haujasogea hatua yoyote zaidi ya kuhama kutoka Westminster, Musoma hadi Dar es Salaam, katika hatua ileile ya jimbo.
Wakati “mchakato” wa Klara Bernadeta umetumia siku 303 tu jimboni Songeana sasa uko Roma, ripoti yake inaandaliwa ichunguzwe na wale maprofesa wa historia.
Nini kinakwamisha mchakato wa Nyerere?
Gazeti la Tumaini Letu la Oktoba 14, 2011, kwenye ukurasa wa pili liliandika habari isemayo: “Wanasiasa wanakwamisha Nyerere kuwa mwenyeheri”.
Katika habari hiyo, Askofuku mkuu Polycarp Kardinali Pengo amenukuliwa akisema, “Tunasikia Rais wa Uganda na Rais wa Tanzania wanakutana na kujaribu kujadiliana kuhusu kumtangaza Mwalimu Nyerere kuwa Mwenyeheri, wao inawahusu nini?”
Kwenye ukurasa huohuo Kardinali Pengo amenukuliwa hivi, “kipingamizi kikubwa ambacho kimejitokeza hadi mchakato huo kusuasua licha ya kuwa vipo vigezo ambavyo hayati Mwalimu Nyerere anastahili kuwa Mwenyeheri ni kuingiliwa na wanasiasa na makundi ya watu wanaotaka kujipatia umaarufu”.
Hivyo, kanisa lilishatufahamisha jinsi wanasiasa na vikundi walivyokwamisha “mchakato” huu.
Mwaka uliofuata, Kardinali Pengo alinukuliwa akisema, “Tusianze kusema Mwalimu akiwa Mwenyeheri manake sisi CCM tumetangazwa watakatifu. Hii si shughuli ya kisiasa, wala akitangazwa usiseme sisi familia ya Nyerere tuko kwenye heri. Wapi, nani kakwambia, wote mko kwenye heri? Nayataja mambo haya kwa sababu yanajitokeza sana” {Tanzania Daima: Januari 14, 2012, uk. 01}.
“Mchakato” ulipoanza, kanisa lilielekeza watu wapeleke taarifa za Julius Nyerere kwa askofu wa Musoma. Sasa mwanasiasa anapokwenda majukwaani badala ya Musoma hicho ni kigezo sahihi cha kuukwamisha.
Tatizo jingine ni ugeni wa kutolijua jambo hili. Nimeeleza “mchakato” kwa kifupi sana lakini ni mrefu na mgumu.
Binafsi sijui tafsiri ya kiswahili ya maneno “venerable”, “postulator”, “undersecretary”, “relator”, “promotor fidei”“promotor justitiae” ambayo hutauelewa “mchakato” bila kuyajua.
Hata waliotafsiri maneno “causes of Saints” walikosea kutuletea neno “mchakato” linalosababisha tudhani “mchakato” hukamilika kwa kumtangaza mtu mtakatifu.
Neno sahihi ni “kesi” kwani kila hatua ya tunachokiita “mchakato” ni kesi kama mahakamani. Maadamu ni kesi, inaweza kukamilikia hatua yoyote kwa matokeo kwamba hastahili hata kuvuka hatua aliyofikia.
Kikwazo kingine kwa Julius Nyerere ni ugumu kupata taarifa zake. Julius Nyerere ameishi akilindwa na askari karibu muda wote. Binadamu wa namna hiyo si rahisi kumkaribia na kiuhalisia maisha yake hayajulikani.
Hata wanaoandika vitabu na makala za utakatifu kumhusu, wanarudia matendo na hotuba tunazozijua hadharani, kama tunavyojua matendo ya Mahatma Gandhi na wengine wengi wazuri. Matendo yasiyo ya hadharani mengine yana utata.
Ninacho kitabu kiitwacho “Mtumishi wa Mungu J. K. Nyerere” kilichoandikwa na padri Felician Nkwera akishirikiana na Anna Julius Nyerere. Kwenye ukurasa wa tano (5) ninakinukuu kinasema hivi,
“Ile fimbo ilikuwa ya kawaida wala si ya ushirikina kama walivyodai watu wengine. Inasemekana alipewa fimbo hiyo na Papa Pius XII mwaka 1948. Papa alimuuliza, Ndiwe unayetafuta uhuru wa Watanganyika? Akajibu “Ndiyo Baba.” “Chukua fimbo hii ukatawale watu wangu (wa Mungu). Alivyorudi Tanganyika aliwaomba wachongaji wamchongee fimbo nyingine na kuitia hiyo fimbo ndogo ndani yake”.
Huhitaji mapofesa wa historia wa pale Roma kutilia shaka kauli hii. Huo mwaka 1948 Julius Nyerere alikuwa ni mwalimu pale Tabora, hajaenda Scotland kusoma na hata Tanu haijazaliwa.
Hivyo, habari ya kupewa kifimbo chake na Papa Pius XII mwaka 1948 inasaidia tu kuukwamisha mchakato wake.
Jambo jingine ni kwamba Watanzania tunamheshimu sana Julius Nyerere, tunamwita “Baba wa Taifa”. Mimi ni Mkatoliki, lakini akitangazwa utakatifu watajivuna Watanzania ambao hata imani zao hazitambui utakatifu.
Lakini mwenye taarifa za kuzuia asitangazwe ana haki kwenda kutoa taarifa zake. Kikanisa huyu ni mzuri analiokoa kanisa lisidanganywe kwamba fulani ni mtakatifu wakati siyo. Je, wananchi na wanasiasa wakimgundua huyu aliyekwamisha, tutaishi naye vipi? Je, atapata utulivu au atasumbuliwa?
Kardinali Pengo alinukuliwa hivi: “Licha ya Mwalimu kuwa mcha Mungu, lakini katika uongozi wake kulikuwa na dosari, kwa hiyo ukiangalia katika hilo kwa viongozi hao kutangazwa kuwa watakatifu ni lazima kuwe na maelezo ya kutosha na viambatanisho ambavyo kweli vinaonyesha kuwa anastahili”: {Tumaini Letu: Oktoba 14, 2011, uk. 02, aya ya 7}.
Viongozi katika mchakato
Moja ya nyimbo za Krismas ni ule uitwao “Good King Wenceslaus”. Ulitungwa na kuimbwa na wananchi wa Bohemia wakiamini mfalme wao Wenceslaus alikufa kifo kitakatifu. Hatimaye Mfalme Wenceslaus akatangazwa kuwa mtakatifu. Bohemia siku hizi inaitwa Jamhuri ya Czech.
Watakatifu wengine waliokuwa watawala ni Edmund (England), Edward (England), Margaret (Scotland), David (Scotland ), Henry II (Germany), Louis (France), Ladislaus (Hungary), Casimir Jagiellon (Poland), Stephen (Hungary).
Lakini wote hawa hawakufanyiwa “mchakato” walitoka siku walipofariki wananchi waliamini wameshakuwa watakatifu kwa ile desturi ya “cult”. Hatimaye wakaja kutangazwa moja kwa moja bila “mchakato” huu.
Hivyo, hakuna mfalme, malkia au rais yeyote duniani aliyewahi kufanyiwa “mchakato” wa utakatifu kama anavyofanyiwa Nyerere, tena unaoanzia kwenye jimbo la nchi aliyoitawala.
Wanaopiga kampeni waziwazi ili Nyerere atangazwe mtakatifu walikosea kusubiri hadi “mchakato” ukaanza. Inaonyesha hawana uzoefu kwani wangeanzisha ile desturi ya “cult” kabla kanisa halijaanza “mchakato”.
Ndivyo walivyotangazwa utakatifu watawala wote niliowataja humu na ndicho walichofanya waumini kwa miaka mingi pale Songea kwa Klara Bernadeta.
Mwaka 1587, Malkia Mary wa Scotland aliuawa na mwaka 1887 Wakatoliki na maaskofu wa Scotland waliomba “mchakato” wake usianzie Scotland. Walitaka ushughulikiwe moja kwa moja na Papa pale Roma.
Roma iliwajibu maaskofu wa Scotland kwamba kama kusingekuwa na utata wa sababu ya mauaji yake ingemtangaza Malkia Mary kuwa mtakatifu.
Kimsingi maaskofu wale wa Scotland waliifundisha dunia kwamba haiwezekani rais wa taifa lolote “mchakato” wake ukaanzia kwenye jimbo la nchi aliyoitawala.
Hivyo, “mchakato” wa Julius Nyerere ni bora ubakie hapohapo ulipo ikibidi ipite miaka hata zaidi 500 ndipo mazingira ya sasa yatakuwa yamebadilika. Wakati huo kutakuwa hakuna anayewakumbuka au kuwaogopa wanasiasa wa sasa.
Joseph Magata, ni msomaji wa Mwananchi na mchambuzi wa masuala ya kanisa Katoliki. Anapatikana kwa simu 0754-710684 Email: [email protected]