Wachungaji KKKT: Msuya atakumbukwa kusimamia kuzaliwa Dayosisi ya Mwanga

Aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Cleopa Msuya enzi za uhai wake.
Muktasari:
- Dayosisi ya Mwanga, ilizaliwa Julai 2016 ikiwa ni safari iliyochukua miaka 18 tangu vuguvugu la kuanzishwa kwake lilipoanza huku mchungaji Chediel Sendoro, akichaguliwa kuwa Askofu wa kwanza wa Dayosisi hiyo.
Moshi. Wachungaji waanzilishi wa Dayosisi ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), wamemwelezea Cleopa David Msuya kama mmoja wa waasisi wa kuzaliwa kwa Dayosisi hiyo akihimiza vuguvugu hilo liwe la amani.
Vuguvugu la uanzishaji wa Dayosisi hiyo lilipitia milima na mabonde huku wachungaji 16, wainjilisti na waumini waliokuwa wakiunga mkono kuanzishwa kwa Dayosisi ya Mwanga kutoka Dayosisi ya Pare wakitengwa na Kanisa.
Licha ya wachungaji kutengwa, lakini mzee Msuya aliendelea kusimama nao kwani hata mkewe, Rhoda Msuya na mwanae, Geofrey Msuya walipofariki kwa nyakati tofauti mwaka 2005, walizikwa na wachungaji wa iliyojiita Dayosisi ya Mwanga.
Mbali na hilo, Mei 27, 2007, watu wasiojulikana waliushambulia kwa mawe msafara wa Askofu wa Dayosisi ya Pare, Stefano Msangi uliokuwa ukitokea Usharika wa Mruma wilayani Mwanga, lakini hakuna aliyejeruhiwa.
Ukiacha matukio hayo, lakini baadhi ya waumini waliokuwa wanaounga vuguvugu la kuzaliwa Dayosisi ya Mwanga walijikuta wakifunguliwa makosa ya jinai huku baadhi ya makanisa yakifungwa muda wa ibada ili ‘waasi’ wasiyatumie kuabudu.
Lakini ni kutokana na busara na hekima za mzee Msuya, maaskofu wa KKKT na uongozi mzima wa KKKT, waliweka mapatano na kurejesha maelewano na wachungaji na waumini waliokuwa wametengwa na Kanisa, wakarejeshwa.
Hatimaye Dayosisi ya Mwanga, ikazaliwa Julai 2016 ikiwa ni safari iliyochukua miaka 18 tangu vuguvugu la kuanzishwa kwake lilipoanza huku mchungaji Chediel Sendoro, akichaguliwa kuwa Askofu wa kwanza wa Dayosisi hiyo.
Hata hivyo, Askofu Sendoro alifariki kwa ajali ya gari Septemba 9, 2024 katika eneo la Kirinjiko ambapo Machi 10, 2025, mkutano mkuu maalumu wa Dayosisi hiyo ukamchagua Mchungaji Daniel Mono kurithi mikoba ya Askofu Sendoro.
Wachungaji hao wametaja waasisi wengine waliotoa mchango wa hali na mali katika vuguvugu hilo na ambao nao wamengulia mbele ya haki kuwa ni pamoja na Peter Kisumo na mfanyabiashara mashuhuri ndani na nje ya nchi, Steven Kangero.
Waasisi wengine ambao walisimama kidete na mzee Msuya katika vuguvugu hilo, ni Philemon Mgaya aliyepata kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), na mzee Timoth Msangi aliyewahi kuwa Meneja Mkuu wa Kampuni ya Sigara Tanzania.
Mzee Msuya aliyewahi kuwa Makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu wa Tanzania, alifariki Jumatano ya Mei 7, 2025 kutokana na matatizo ya moyo na atazikwa Jumanne Mei 13, 2025 kijiji kwake huko Usangi wilayani Mwanga.
Rais Samia Suluhu Hassan ndiye atawaongoza waombolezaji katika mazishi hayo ya kitaifa, ambayo yatatanguliwa na kuaga mwili Mei 11,2025 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, shughuli ambayo pia itaongozwa na Rais Samia.
Walichokisema wachungaji KKKT
Mchungaji Richard Muzze ambaye ni mkuu wa jimbo la Tambarare mstaafu aliyeshiriki mwanzo mwisho katika vuguvugu la kudai kuzaliwa kwa Dayosisi ya Mwanga, alisema Msuya ni miongoni mwa waasisi wa Dayosisi hiyo.
“Sisi tuna huzuni sana kwa kweli. Mzee Msuya alitoa mchango mkubwa wa mawazo, fedha na mali pamoja na kina mzee Kisumo na wenzake kuhakikisha Dayosisi hii inazaliwa. Kiukweli hana deni na waumini wa KKKT Mwanga,”amesema.
“Alisimama na sisi kipindi kigumu sana wakati ule wachungaji na waumini wote wa eneo la Mwanga tulioonekana kudai kuzaliwa kwa Dayosisi tulitengwa lakini alikuwa anakuja kusali na sisi majumbani. Hata mkewe Rhoda tulimzika sisi,” amesimulia.
Kwa upande wake, Mchungaji Abraham Mshana ambaye ni Mkuu wa Jimbo la Magharibu Ugweno mstaafu, alimwelezea mzee Msuya kama injini au dereva aliyewaandesha pamoja na waasisi wengine kupata Dayosisi ya Mwanga.
“Kwa kweli chombo muhimu kwenye gari basi mzee Msuya alikuwa ni Injini. Tunaweza kumfananisha na dereva anayefikisha abiria wake salama. Mzee Msuya alituendesha kwa umakini hadi tukaipata Dayosisi. Mungu amrehemu,”amesema.
“Alikuwa mshauri mzuri. Hata katika ile ibada ya kurudiana baada ya awali kutengwa ambayo na yeye alihudhuria alitoa maneno mazito sana. Alisema angetamani kuona Dayosisi ya Mwanga inazaliwa akiwa hai,”amesema.
“Hata upatikanaji wa Askofu wa kwanza wa Dayosisi yetu (Sendoro) baada ya kutambuliwa na KKKT yeye ana mkono wake. Hata Askofu wetu mpya (Mono) kuna ushauri wake humo. Kwa kweli ameacha pengo kubwa sana,”ameeleza.
Mchungaji David Assery ambaye ni mkuu wa Jimbo mstaafu Jimbo la Mashariki, amesema alimfahamu mzee Msuya wakati yeye (Assery) akiwa darasa la sita wakati huo ndio Wilaya ya Mwanga inazaliwa kutoka wilaya mama ya Same.
“Joto likaendelea la kutaka tuwe na Dayosisi yetu hapa Mwanga ili kusogeza huduma za Injili karibu zaidi. Mzee Msuya alikuwa mstari wa mbele katika vuguvugu la kuanzishwa kwa hii Dayosisi. Alilihangaikia sana hilo jambo,”amesema.
“Alihamasisha upendo na amani wakati wote wa vuguvugu. Yeye na akina mzee Peter Kisumo na wenzake wale kwa kweli wana mchango mkubwa wa kuhakikisha Dayosisi inapatikana kwa amani. Tunawaombea pumziko la amani,”ameeleza.
“Tulipozaliwa tulijikuta Dayosisi ina madeni mengi sana. Nakumbuka siku moja mzee Msuya alituita nyumbani kwake Dar es Salaam akaita marafiki zake akafanya harambee. Mengi (Reginald-marehemu) alikuja na alitupa msaada mkubwa.”
“Kwa hiyo kwetu sisi wana Dayosisi na Wilaya ya Mwanga ni msiba mkubwa sana. Tunamlilia tukikumbuka mema mengi aliyotufanyia. Hakugusa tu kwenye imani, hata katika huduma za kijamii ndio maana anaitwa baba wa Mwanga,”amesema.
Muumini wa Dayosisi hiyo aliyekuwepo wakati wa vuguvugu la kuanza kudai kuzaliwa kwa Dayosisi ya Mwanga, Rodgers Msangi, amesema Mzee Msuya alichangia sana kusimamia upatikanaji wa Dayosisi kwa njia ya amani.
“Hekima zake, busara zake na mchango wake wa mawazo, mali na fedha ndio ulifanikisha kwa sehemu kubwa kuzaliwa kwa Dayosisi yetu. Kwa kifupi ameacha alama inayoishi kwenye mioyo ya wakristu. Apumzike kwa amani,”amesema.
Wosia wa Askofu Mjema
Katika mkutano mkuu maalumu wa kumchagua Sendoro mwaka 2016, Askofu wa Dayosisi ya Pare ambayo ndio iliyozaa Dayosisi ya Mwanga, Charles Mjema, alisema tukio la kuzaliwa kwa Dayosisi hiyo ni la kihistoria na linahitimisha safari ya miaka 18.
“Itakuwa ni hatua ya kuhitimisha safari yetu ya miaka 18 iliyokuwa imejaa changamoto nyingi na kutupa uzoefu wa aina yake katika kuhudumiwa Kanisa la Mungu,”alisema Askofu Mjema alipozungumza katika mkutano huo.
“Hakuna aliyeshinda au kushindwa wala hakuna aliyefanya zaidi ya mwingine kwa vile kila mmoja kwa nafasi yake alifanya kile kilichokuwa wajibu wake,”amesisitiza.
Askofu huyo alinukuliwa akisema japokuwa historia ya wapi safari hiyo ilipoanzia itabakia katika vichwa vya wengi lakini, aliomba historia hiyo isigubike mtazamo wa kuifanya Dayosisi hiyo kusimama imara na kutimiza ndoto za wakristo.