Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hii hapa ratiba kamili ya mchakato wa uchaguzi CCM

Muktasari:

  • Hatua hiyo ya pili inakwenda kutoa nafasi kwa kamati za siasa kuchuja wagombea na kutoa mapendekezo kwa kamati za juu hadi kufikia ngazi ya taifa ambapo baadaye kamati kuu itahitimisha hatua hiyo kwa kurudisha majina ya wagombea.

Dar es Salaam. Baada ya kukamilika kwa mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuomba uteuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika nafasi za ubunge na udiwani, kamati za siasa zinaanza vikao vyake kesho Julai 4, 2025 kuwajadili waliotia nia.

Hatua hiyo ya pili inakwenda kutoa nafasi kwa kamati za siasa kuchuja wagombea na kutoa mapendekezo kwa kamati za juu hadi kufikia ngazi ya taifa ambapo baadaye kamati kuu itahitimisha hatua hiyo kwa kurudisha majina ya wagombea.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CCM, Julai 4, 2025, vikao vya kamati za siasa za kata na wadi vitaanza kuwajadili wagombea udiwani, udiwani wa viti maalumu, kisha kutoa mapendekezo kwa kamati za siasa za jimbo kwa Zanzibar na wilaya kwa Tanzania Bara.

Julai 5, 2025, kamati za siasa za jimbo (Zanzibar) kufanya vikao vyao kuwajadili wagombea wa udiwani, ubunge na uwakilishi na kisha kutoa mapendekezo yao kwa kamati za siasa za wilaya, kwa hatua nyingine.

Siku inayofuata, Julai 6, 2025, vikao vya kamati za siasa za wilaya vitaanza kuwajadili wagombea ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, udiwani wa kata au wadi na udiwani wa viti maalumu, kisha kutoa mapendekezo kwa kamati ya siasa ya mkoa.

Julai 8, 2025, vikao vya kamati za utekelezaji za Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) za mikoa kuwajadili wagombea ubunge na uwakilishi viti maalumu kupitia mkoa na kutoa mapendekezo kwa kamati ya siasa ya mkoa.

Ratiba hiyo inaonyesha kwamba Julai 9 na 10, 2025, vikao vya kamati za siasa za mkoa vitafanyika, huku vikiwa na kazi ya kuteua wagombea udiwani na udiwani wa viti maalumu wasiozidi watatu, watakaopigiwa kura ya maoni na wajumbe.

Pia, kamati za siasa zitawajadili wagombea ubunge na uwakilishi na kutoa mapendekezo kwa kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa Tanzania Bara na kamati maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar, kwa upande wa Zanzibar.

Julai 15, kamati ya utekelezaji ya UWT Taifa itawajadili wagombea ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na makundi Maalumu na kutoa mapendekezo yake kwa kamati kuu ya kwa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar kutoa mapendekezo kwa kamati maalumu.

Kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kitafanyika Julai 17 na 18, 2025 ambapo kitapokea na kuchambua majina ya wagombea ubunge na uwakilishi wa jimbo na viti maalumu kwa ajili ya maandalizi ya vikao vya uteuzi.

Julai 19, 2025, kikao cha kamati kuu ya CCM kitafanyika kufikiria na kuteua majina ya wanaCCM wasiozidi watatu walioomba nafasi ya ubunge na uwakilishi wa jimbo na viti maalumu ili wakapigiwe kura za maoni.

Mikutano mikuu maalumu ya UWT ya wilaya kupiga kura ya maoni Julai 20, 2025 kwa wagombea wa udiwani wa viti maalumu.

Pia, Julai 22, 2025, mikutano mikuu maalumu ya mikoa ya UWT kupiga kura ya maoni kwa wagombea ubunge wa viti maalumu (Tanzania Bara) na wagombea ubunge/uwakilishi wa viti maalumu (Zanzibar).

Julai 24, 2025, mkutano mkuu maalumu wa UVCCM Taifa kupiga kura ya maoni kwa wagombea wa ubunge wa viti maalumu vijana (Tanzania Bara) na ubunge/uwakilishi wa viti maalumu vijana (Zanzibar).

Mkutano mkuu maalumu wa UWT Taifa kupiga kura ya maoni Julai 25, 2025 kwa wagombea wa ubunge wa viti maalumu vya makundi (Tanzania Bara) na ubunge/uwakilishi viti maalumu (Zanzibar).

Wakati mchakato huo ukiendelea, Julai 26, 2025, mkutano mkuu maalumu wa Wazazi Taifa kupiga kura ya maoni kwa wagombea wa ubunge wa viti maalumu Wazazi (Tanzania Bara) na ubunge/uwakilishi viti maalumu (Zanzibar).

Julai 27 hadi Agosti Mosi, 2025, mikutano ya kujitambulisha kwenye kata/wadi kwa wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani. Agosti 2, 2025, mikutano mikuu ya kata/wadi kupiga kura za maoni za wagombea wa ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na udiwani wa kata/wadi.

Hatua hiyo ikikamilika, kuanzia Agosti 3 hadi 26, 2025, kutakuwa na vikao tofauti vya uchujaji baada ya kura ya maoni ambavyo vitahusisha kamati za siasa za kata, jimbo, wilaya, mikoa, vikao vya sekretarieti na halmashauri kuu.

Agosti 21 hadi 25, ni uchukuaji na urejeshaji wa fomu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa wanachama walioteuliwa kugombea nafasi ya ubunge, uwakilishi na udiwani.