Waombolezaji wakatisha hotuba ya Waziri Masauni, wamtaka aondoke msibani

Viongozi mbalimbali wakiwa msibani kwa aliyekuwa kada wa Chadema, Ali Kibao nyumbani kwake mkoani Tanga, katika shughuli ya mazishi yake akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni. Picha na Rajabu Athumani
Dar es Salaam. Kelele zimetokea wakati hotuba zikiendelea katika msiba wa aliyekuwa kada wa Chadema, Ali Kibao nyumbani kwake mkoani Tanga, wakati Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni akihutubia wananchi.
Kelele hizo zimeibuka zikimtaka Waziri Masauni kujiuzulu nafasi yake kutokana na matukio ya kutekwa wananchi yanayoendelea nchini.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwatuliza wananchi hao na kuwaomba kumuacha Waziri Masauni kumaliza hotuba yake na alifanikiwa kumaliza hotuba hiyo.
Wamtaka ajiuzulu
Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wa ACT Wazalendo, wamewataka Waziri Masauni na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillius Wambura kukaa kando kutokana na mfululizo wa matukio ya utekaji na kuuawa kwa wananchi.
Viongozi hao wamesema hayo leo Jumatatu Septemba 9, 2024 mkoani Tanga, wakati wa kutoa salama kwenye msiba wa aliyekuwa kada wa Chadema, Ali Kibao anayezikwa leo, saa 7 mchana.
Kibao, aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema alichukuliwa jioni ya Septemba 6, 2024 eneo ya Kibo Complex Tegeta jijini Dar es Salaam na watu wasiojulikana, akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea Tanga na basi la Tashriff na mwili wake kupatikana jana Jumapili Septemba 8, 2024 eneo la Ununio, Dar es Salaam.
Akitoa salamu katika msiba huo, Godbless Lema, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, amesema, “Mheshimiwa Waziri nikuombe sana usiende tena kwenye msiba wa mtu aliyetekwa, nenda kwenye msiba wa mtu ambaye ameuawa. Mnatuumiza, nilitarajia baada ya statement ya Rais jana, wewe leo uwe umejiuzulu, IGP amejiuzulu na viongozi wengine wakae kando.
“Sisemi mambo haya kukuvunjia heshima, lakini wewe ni Waziri wa Mambo ya Ndani tusaidie, najiuliza hata nikiwa na kosa polisi wakija kunikamata natokaje,” amesema.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti (Bara) wa ACT Wazalendo, Isihaka Machinjita amesema: “Tukio lililotukutanisha hapa ni la ndugu yetu (Ali Kibao) ambaye ameuawa, tukio la namna hii linazusha hofu juu ya usalama wetu, tuna swali juu ya usalama wetu, ndugu yetu huyu ameuawa kwa sababu Jeshi la Polisi limeshindwa kulinda usalama wa raia na mimi niunge mkono alichosema Lema.
“Wakati mimi nipokuwa naangalia kwenye mtandao unakuja (Waziri Masauni), nikasema sisi tulishatoa wito kwamba mheshimiwa waziri angechukua hatua za kujiuzuru tangu matukio haya yalipotokea,” amesema.
Endelea kufuatilia Mwananchi.