Askofu Shoo ajitosa sakata la mauaji kada Chadema, CCT yalaani

Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo.
Muktasari:
- Tukio la kuchukuliwa na watu wasiojulikana kwa Mjumbe wa Sekeretarieti ya Chadema, Ally Kibao kisha mwili wake kukutwa umetupwa, limemfanya Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dk Frederick Shoo kuhoji maswali kadhaa juu ya mauaji hayo.
Moshi. Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imekemea vitendo vya utekaji, ukatiili na mauaji yanayofanywa na genge la watu wasiojulikana na kulaani tukio la kuchukuliwa na kuuawa kikatili kwa kada wa Chadema, Ally Kibao.
CCT ni Taasisi inayowakilisha Umoja wa Madhehebu ya Kikristo ya Kiprotestanti pia inaundwa na makanisa mbalimbali wanachama na vyama vya Kikristo au vyenye mwelekeo wa kikanisa kutoka Tanzania Bara na Visiwani.
Tayari Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameeleza kusikitishwa na mauaji hayo na kuagiza vyombo vya uchunguzi kumpelekea haraka taarifa ya kina juu ta tukio hilo na mengine ya aina hiyo.
Kupitia kurasa zake za kijamii, jana Jumapili, Septemba 8, 2024 saa 12:26 jioni, Rais Samia mbali na kutoa pole kwa familia, Chadema, ndugu, jamaa na marafiki, lakini alisema Tanzania ni nchi inayoongozwa kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi.
"Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya mauaji ya kiongozi wa CHADEMA Bwana Mohamed Ali Kibao. Natoa pole kwa viongozi wa chama hicho, familia ya Mzee Kibao, ndugu, jamaa na marafiki."
"Nimeagiza vyombo vya uchunguzi kuniletea taarifa ya kina kuhusu tukio hili baya kabisa na mengine ya namna hii haraka. Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi. Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii," alisema Rais Samia.
Kada huyo wa Chadema alichukuliwa na watu wenye silaha Ijumaa ya Septemba 6, 2024 eneo la Kibo Complex, Tegeta jijini Dar es Salaam akiwa ndani ya basi la Tashrif akitoka Dar es Salaam kuelekea Tanga ambapo watu walimshusha na kuondoka naye hadi mwili wake ulipopatikana umetupwa Ununio jijini hapa.
Mwili huo ulichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala. Unatarajiwa kuzikwa leo Jumatatu, Septemba 9, 2024 saa 7 mchana mkoani Tanga.
Alichokisema Askofu Shoo wa CCT
Katika ujumbe wake kwa Mwananchi jana usiku, Septemba 8, 2024, Mwenyekiti wa CCT, Askofu Fredrick Shoo amesema sasa ifike mwisho kwani inaumiza kila kukicha kusikia taarifa za watu kutekwa, kufanyiwa ukatili na kuuawa na watu wasiojulikana.
“Watanzania tumefika huko? Ndio njia tumeamua kuiendea? Hao wafanyayo hayo sasa wanaonyesha wazi, tena mchana kweupe kuwa hawamwogopi yeyote, chochote, wala hawana hofu ya Mungu tena,” amesema Askofu Shoo na kuongeza.
“CCT tumesikitishwa sana na mauaji na ukatili wanaofanyiwa Watanzania wasio na hatia. Tunakemea vikali utekaji, ukatili na mauaji yanayoendelea nchini kwa sasa.”
“Mnaofanya hayo iwe ni kwa sababu yoyote ile, mjue yupo Mungu, nasi tutamwomba adhihirishe wazi uwezo na mamlaka yake. Mungu hadhihakiwi,” amesema.
"Kama mnayafanya hayo ili kuwajaza watu hofu, jueni Watanzania tunasema kwa haya hatuogopi wala hatutaogopa. Tunayakataa, kuyapinga na kuyakemea wazi,” amesaema Askofu Shoo ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT.
Katika maelezo yake, kiongozi huyo wa kiroho amesema:“Kama lengo lenu ni kumchafua Rais wetu ili mikono yake ijae damu za watu, jueni kuwa mmeshashindwa na mtashindwa vibaya, kwa maana Mungu atatenda jambo."
Mkuu huyo wa KKKT mstaafu amesema:“Tunatoa wito kwa Watanzania wote waombe kwa dhati na kukemea vitendo hivi viovu vinavyotaka kutishia usalama, haki na amani kwa raia wa nchi yetu."
Amesema tukio hilo limerudisha kumbukumbu ya shambulio la Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu.
Lissu ambaye alikuwa Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema hadi aliposhambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana alasiri ya Septemba 7, 2017, Area D jijini Dodoma ambapo kwa uchache risasi 16 kati ya 30 ziliingia mwilini mwake.
Askofu Shoo amesema matukio kama aliyofanyiwa Lissu na sasa mauaji ya kada huyo wa Chadema na utekaji na watu kupotea unaoendelea nchini hauleti picha nzuri, lakini amemshukuru Rais kwa kuagiza kuchunguza mauaji ya Kibao.
DCI aongeza nguvu
Jana Jumapili, Jeshi la Polisi katika mwendelezo wa taarifa zake juu ya tukio la kuuawa kwa Kibao, lilisema timu ya uchunguzi wa matukio makubwa kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), imetumwa kuongeza nguvu ya upelelezi.
“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hili la kusikitisha na timu ya uchunguzi wa matukio makubwa kutoka ofisi ya DCI imetumwa kuiongezea nguvu timu ya awali ili kuhakikisha waliofanya mauaji hayo wanakamatwa,” ilisema.
Taarifa hiyo iliyotolewa usiku wa jana Jumapili Septemba 8,2024 na kusainiwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, imetoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za kweli na za uhakika juu ya mauaji hayo aziwasilishe ili kusaidia uchunguzi wa tukio hilo.
Katika taarifa hiyo, Jeshi hilo limeeleza Kibao aliyekuwa mjumbe wa Sekeretarieti ya Chadema Taifa, alishushwa katika basi la Tashrifu na kuchukuliwa na watu ambao hawakuweza kutambuliwa na uchunguzi ulikuwa umeanza.
Misimu kupitia taarifa hiyo alisema baadae kulipatikana taarifa za kupatikana kwa mwili wa mtu mwanaume ambaye hakuweza kutambuliwa ni wa nani huko Ununio Jijini Dar es Salaam lakini baadaye ndugu waliweza kuutambua kuwa ni wa Kibao.
Kama ilivyo taratibu, mwili huo ulifanyiwa uchunguzi (postmorterm) jana Jumapili Septemba 8,2024 katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko yanatakayofanyika jijini Tanga.
Kauli ya Mbowe, mitandaoni
Baada ya kusambaa kwa taarifa za mwili wa kada huyo kuwapo katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mwananyama, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine walifika hospitalini hapo.
Akizungumza na wanahabari nje ya chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo, Mbowe alitaka uchunguzi wa tukio hilo ufanyike huku akitilia mashaka uchunguzi kufanywa na Polisi.
Ukiacha kauli hiyo ya Mbowe, lakini katika mitandao ya kijamii ya X, Instagram, Facebook na makundi ya Whatsapp, mijadala yenye hisia kali ilikuwa ikiendelea huku baadhi wakiona Serikali ilichelewa kuchukua hatua juu ya utekaji.