Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uongozi mabasi ya Tashriff waeleza sababu kutozuia utekaji kada wa Chadema

Picha ya Ali Kibao, ambapo inadaiwa mwili wake upo monchwari ya Mwananyamala

Muktasari:

  • Uongozi wa Kampuni ya mabasi hayo umesema mtu aliyekuwa ndani ya basi hilo na kuambatana na watekaji, mwanzo wa safari aligoma kutoa taarifa zake, lakini alilazimishwa kuzitoa, hivyo tarifa zake tayari wameziwasilisha Polisi.

Dar es Salaam. Uongozi wa Kampuni ya Mabasi ya Tashriff umesema tukio la kutekwa kwa aliyekuwa kada wa Chadema, Ally Kibao ndani ya usafiri wao, liliwashtua na wamedai walishindwa kuzuia kutokana na wahusika kuwa na silaha za moto.

Pia, umedai watu hao waliwatisha wafanyakazi waliokuwa ndani ya basi hilo kwa kutumia silaha za moto, baada ya tukio hilo waliripoti Kituo cha Polisi Magufuli.

Kibao, aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema alichukuliwa ndani ya basi hilo jioni ya Ijumaa Septemba 6, 2024, eneo la Kibo Complex, Tegeta jijini Dar es Salaam, wakati akisafiri kwenda nyumbani kwake, mkoani Tanga.

Tukio hilo lilianza kujadiliwa maeneo mbalimbali Jumamosi ya Septemba 7, 2024, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alizungumza na waandishi wa habari kuzungumzia tukio hilo na kutoa wito kwa vyombo vya usalama kulichunguza.

Katikati ya mijadala hiyo, asubuhi ya jana Jumapili, Septemba 8, 2024, kuliripotiwa mwili wa Kibao uliokuwa umetupwa Ununio, jirani na viwanja vya NSSF na ulichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Dar es Salaam.

Uchunguzi wa kitabibu ulifanyika jana hospitalini hapo na taarifa yake bado haijatoka, ingawa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyekuwapo alidai Kibao kabla ya kufikwa na mauti aliteswa na kumwagiwa tindikali usoni.

Mwili wa Kibao unazikwa mchana wa leo saa 7 mchana mkoani Tanga. Viongozi mbalimbali wamehudhuria akiwemo Mbowe, Mnyika, Naibu katibu wakuu wa Chadema, Salum Mwalimu (Zanzibar), Benson Kigaila (Bara) na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni.

Leo Jumatatu, Mwananchi limezungumza na Msimamizi wa Mabasi ya Tashriff, Dar es Salaam, Shaban Shemweta ambaye amedai tukio la kuuawa kwa mzee huyo limewahuzunisha.

Amedai watu waliosimamisha basi hilo walikuwa na magari mawili yasiyo na namba ya utambuzi na baada ya kulisimamisha basi hilo, mtu mmoja alikwenda mbele ya gari na kumuamuru dereva asiliondoe gari na wengine wenye silaha kupanda ndani na kumchukua kwa nguvu wakiwa wamemfunga pingu.

“Mzee Kibao namfahamu ni mteja wetu wa muda mrefu, tulishangazwa na tukio hilo na limetuuliza. Watu walikuwa na silaha za moto na walitutisha kwenye gari letu ambalo walizuia kwa mbele na nyuma na ndani ya gari kulikuwa na mtu mwingine ambaye aliungana na watu wale,” amedai.

Shemweta amedai mtu ambaye alikuwa kama abiria ndani ya basi lao na kuungana na watekaji, wakati akianza safari kituoni alikataa kutoa taarifa zake wakati wa ukatishaji wa tiketi.

“Alikataa kutoa taarifa zake, lakini alipoona tumemkazania akazitoa ila namba za simu hakuridhia, taarifa zake za tiketi tayari tulizikabidhi polisi,” amedai. 

Baada ya tukio la kutekwa kwa mzee huyo, Shemweta amesema walitoa taarifa kwa ndugu zake na baadaye kituo cha Polisi Magufuli kilichopo Mbezi, Dar es Salaam.

Kutokana na tukio hilo, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alitumia akaunti zake za kijamii kulilaani na kuagiza uchunguzi wa haraka kufanyika.

Rais Samia alisema, “Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya mauaji ya kiongozi wa Chadema, Mohamed Ali Kibao. Natoa pole kwa viongozi wa chama hicho, familia ya Mzee Kibao, ndugu, jamaa na marafiki.

“Nimeagiza vyombo vya uchunguzi kuniletea taarifa ya kina kuhusu tukio hili baya kabisa na mengine ya namna hii haraka. Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana Haki ya kuishi. Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii,” amesema.

Awali, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alitoa taarifa kwa umma akisema:“Jeshi la Polisi, lingependa kutoa taarifa kuwa lilipokea taarifa hiyo na kuanza uchunguzi wa kubaini kilichotokea, chanzo chake na watu waliohusika ni kina nani.”

Misime alisema kwa yoyote mwenye taarifa za kweli na za uhakika aziwasilishe kwa mujibu wa taratibu, ili kusaidia kufanikisha kukamilika mapema kwa uchunguzi wa tukio hilo la kusikitisha.