Hashim Lundenga afariki dunia

Mratibu wa zamani Miss Tanzania Hashim Lundenga enzi za uhai wake.
Dar es Salaam. Mratibu wa zamani wa mashindano ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga amefariki dunia leo Jumamosi Apili 19, 2025 katika Hospitali ya Kitengule iliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya kifo chake imethibitishwa na Katibu wa Kamati ya Miss Tanzania, Bosco Majaliwa.
“Ndio Hashimu Lundenga amefariki kama masaa mawili yaliyopita katika Hospitali ya Itengule iliyopo Tegeta hapa. Hashimu ameumwa muda mrefu sana, nafikiri taarifa ya kuumwa kwakwe watu wengi wanayo, alipata ‘stroke’ muda mrefu sana, alilazwa kwenye Hospitali Muhimbili alitolewa, alilazwa Mlongazila akatolewa akawa anaendelea kupata kliniki lakini hali ikazidi kuwa mbaya zaidi,” amesema
Ameongeza kuwa, “Kwa hiyo jana alizidiwa wakamleta hapa kwenye Hospitali ya Itengule lakini bahati mbaya amefariki dunia, msiba upo nyumbani kwake Bunju.”
Amesema baada ya kuuhifadhi mwili mochwari watakaa ili kujadiliana suaka la mazishi.
Lundenga ambaye ameugua kwa muda mrefu, alisimamia mashindano ya urembo Tanzania na kufanya yajulikane na kupata umaarufu. Hata hivyo aliachia kijiti cha kusimamia Miss Tanzania 2018 ambapo alisimamia mashindano hayo tangu mwaka 1994, hivyo akimkabidhi Basila Mwanukuzi.
Mbali na hilo pia Lundenga aliwahi kuhudumu kwenye kamati ndani ya Klabu ya Yanga.