Prime
Msajili atengua uteuzi wa vigogo Chadema

Muktasari:
- Januari 22, 2025, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu aliteua wajumbe wanane ambao walithibitishwa na Baraza Kuu la chama hicho ambao kada wake, Lembrus Mchome alilipinga akidi haikutimia.
Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imetengua uteuzi wa wajumbe wanane wa sekretarieti na kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliothibitishwa na Baraza Kuu la chama hicho Januari 22, 2025.
Mbali na kutengua, ofisi hiyo imetoa maelekezo kwa chama hicho kikuu cha upinzani nchini yanayopaswa kufanyiwa kazi ili kukidhi matakwa ya sheria ya vyama vya siasa, kanuni na katiba ya Chadema.
Uamuzi huo umefanyika ikiwa ni kujibu malalamiko yaliyowasilishwa kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Lembrus Mchome akipinga akidi ya Baraza kuu iliyowathibitisha.
Mchome alikuwa akilalamikia kwamba akidi haikutimia ya kuwathibitisha viongozi hao ambao walikuwa wameteuliwa na mwenyekiti mpya wa Chadema, Tundu Lissu.
Viongozi waliokuwa wanaolalamikiwa na msajili ameamua kuwaweka kando hadi Baraza kuu jingine liitishwe ni Katibu Mkuu, John Mnyika, Amani Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar).
Pia, aliwataja wajumbe wa kamati kuu walioteuliwa na kuidhinishwa na Baraza Kuu, Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk Rugemeleza Nshala ambaye pia aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa chama hicho.
Barua ya Mchome kwenda kwa msajili ya kwanza aliiandika Februari 18, 2025 akilalamikia uteuzi wa viongozi hao.
Hata hivyo, Machi 25, 2025 akifungua mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) na Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) Kanda ya Kusini, Mnyika alisema kikao cha baraza kuu cha Januari 22, 2025 kilifuata utaratibu unaotakiwa.
Mnyika alisema akidi iliyotumika ni asilimia 50 ya wajumbe, kwa kuwa kikao hicho hakikuwa cha kiuchaguzi wala kupitisha sera au katiba, ambacho uhitaji akidi ya asilimia 75 ya wajumbe.
Kufuatia malalamiko hayo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilisema tayari imepokea barua ya Mchome na imeiandikia tena Chadema kuitaka itoe majibu ndani ya siku tatu kuanzia Aprili 8, 2025.
Machi 31, 2025 Ofisi ya Msajili iliipa Chadema siku saba kujibu malalamiko ya Mchome, hatua ambayo licha ya kutekelezwa na chama hicho, kada huyo hakuridhika akaandika barua ya pili.
Katika barua yake ya pili, Mchome aliitaka Ofisi ya Msajili, kubatilisha viongozi wote waliopitishwa kinyume cha katiba ya chama hicho pamoja na uamuzi uliofanyika Januari 22, 2025.
Leo Jumanne, Machi 13, 2025, taarifa ambazo Mwananchi limezipata kutoka kwa kiongozi mwandamizi ndani ya chama hicho aliyeomba ahifadhiwe jina lake amesema ofisi ya msajili imetoa uamuzi kuhusu malalamiko ya Mchome.
“Aise hizi ni taarifa mbaya sana, msajili ametutwanga barua akikubaliana na malalamiko ya Mchome, amesema kweli akidi haikutimia na ametutaka kuitisha mkutano mwingine wa baraza kuu ukiwa na akidi iliyotimia,” amesema kiongozi huyo.
Katika maelezo yake amesema: “Kwa sasa bado tunasubiri nini cha kufanya kwani viongozi wengi wako mikoani kwenye operesheni yetu ya No reforms, no election. Lakini kwa vyovyote vile lazima baraza liitishwe vinginevyo chama kitakuwa hatarini sana.”
Baada ya taarifa hizo, Mwananchi limemtafuta, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia ambaye amesema taarifa hizo naye amezisikia kwani aliyekuwa ofisini ni Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Golugwa.
“Nimempigia lakini hatukuweza kuwasiliana kwa kuwa taarifa zilizopo amekamatwa na Jeshi la Polisi,” amedai Brenda.
“Bado nazifuatilia hizo taarifa kujua ukweli kwani kama nilivyosema hata mimi nimezisikia tu mtandaoni, nitakapokuwa na uhakika nazo tutaziweka wazi kwa kuwa ni taarifa ambazo jamii inapaswa kuzifahamu,” amesema Brenda.
Pia suala la Golugwa kukamatwa, tunaendelea kulifuatilia.
Aidha, Mwananchi limemtafuta Mchome kujua kama amepokea nakala ya barua hiyo, ambapo hakukubali wala kukataa zaidi amesema kesho Jumatano, Mei 14, 2025 atazungumza na waandishi wa habari.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa wakati wowote Mchome huenda akazungumza na wanahabari kueleza kuelezea majibu aliyopewa na Ofisi ya Msajili kuhusu malalamiko aliyoyapeleka.
Pia, Mwananchi limewatafuta viongozi mbalimbali wa ofisi ya msajili akiwemo Msajili mwenyewe, Jaji Francis Mutungi na au Naibu Msajili, Sisty Nyahoza bila mafanikio.
Jitihada za kuwatafuta bado zinaendelea.