Prime
Mchome azidi kuichoma Chadema kwa msajili

Muktasari:
- Barua hiyo ya Mchome kwenda kwa msajili ya hivi karibuni inakuwa ya pili baada ya kuwasilisha nyingine Februari 18 kwenda ofisi katika hiyo akilalamikia uteuzi wa viongozi wa kamati kuu na sekretarieti, uliofanywa na Baraza Kuu analodai akidi haikukamilika Januari 22, 2025
Dar es Salaam. Sakata la Lembrus Mchome, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Mwanga, limechukua sura mpya baada ya kada huyo kuiandikia tena Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, akitaka uongozi wa juu wa chama hicho kubatilishwa.
Barua ya Mchome kwenda kwa msajili inakuwa ya pili baada ya kuwasilisha barua yake ya kwanza Februari 18, 2025 akilalamikia uteuzi wa viongozi wa kamati kuu na sekretarieti uliofanywa kinyume cha katiba kwa kuwa akidi haikutimia.
Viongozi wanaolalamikiwa ni Katibu Mkuu, John Mnyika, Amani Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar.
Pia, aliwataja wajumbe wa kamati kuu walioteuliwa na kuidhinishwa na Baraza Kuu – Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk Rugemeleza Nshala.
Hata hivyo, Machi 25, 2025 akifungua mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) na Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) Kanda ya Kusini, Mnyika alisema kikao cha baraza kuu cha Januari 22, 2025 kilifuata utaratibu unaotakiwa.
Alisema akidi iliyotumika ni asilimia 50 ya wajumbe, kwa kuwa kikao hicho hakikuwa cha kiuchaguzi wala kupitisha sera au katiba, ambacho uhitaji akidi ya asilimia 75 ya wajumbe.
Kufuatia malalamiko ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesema tayari imepokea barua ya Mchome na imeiandikia tena Chadema kuitaka itoe majibu ndani ya siku tatu kuanzia Aprili 8, 2025.
Machi 31, 2025 Ofisi ya Msajili iliipa Chadema siku saba kujibu malalamiko ya Mchome, hatua ambayo licha ya kutekelezwa na chama hicho, kada huyo hakuridhika akaandika barua ya pili.
Katika barua yake ya sasa, Mchome anaitaka Ofisi ya Msajili, kubatilisha viongozi wote waliopitishwa kinyume cha katiba ya chama hicho pamoja na uamuzi uliofanyika Januari 22 mwaka huu.
Akizungumzia hayo leo Jumanne, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza amesema tayari wameiandikia Chadema barua ikitakiwa kutoa majibu na nakala kupatiwa Mchome.
“Mchome ametuandikia barua analalmikia uongozi kukiuka katiba na ameleta na ushahidi wa video, tumewaandikia Chadema barua wajibu ndani ya siku tatu,” amesema Nyahoza.
Alipoulizwa yaliyomo ndani ya barua hiyo, Nyahoza amesema Mchome ameomba uongozi wa Chadema uliopatikana kinyume cha katiba Februari 2025 ubatilishwe pamoja na uamuzi wao.
Leo Jumanne Aprili 8, 2025, Mchome amewaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa ameomba hatua hiyo ichukuliwe kutokana na uamuzi ya Baraza Kuu la chama hicho kuwa na dosari.
Mchome anadai dosari mojawapo alidai uwepo wa Askofu Emmaus Mwamakula, Mchungaji Maximillian Machumu (Mwanamapinduzi) John Pambalu, Twaha Mwaipaya, Rose Mayemba na wengineo zaidi ya 40 aliodai si wajumbe wa kikao walichoshiriki.
Anasema uwepo wa watu hao ni kinyume na katiba ya chama hicho, akisisitiza hoja zake alizowasilisha Ofisi ya Msajili zina amshiko.
“Nimemwomba Msajili kubatilisha baraza kuu la Januari 22, 2025 pili viongozi wote wanane waliopitishwa siku hiyo watenguliwe,” amesema.
Sakata la Ruge
Katika hatua nyingine, Chadema imetetea utenguzi wa Catherine Ruge kwenye nafasi ya mtaalamu wa Dawati la Jinsia kuwa ulifuata taratibu zote.
Ruge alitenguliwa Aprili 5, 2025 na mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu ambaye yupo ziarani mikoa ya kusini kunadi ajenda ya bila mabadiliko hakuna uchaguzi (No Reforms No Election).
Baada ya uteuzi huo, Ruge andika ujumbe na kusambaza katika mitandao ya kijamii, akieleza kushtushwa na hatua iliyochukuliwa na Lissu kutengeua nafasi yake, akidai katibu ya Chadema imekiukwa.
“Mamlaka ya utenguzi wa nafasi yangu ni Kamati Kuu na sio mwenyekiti wa chama hivyo nilitegemea utaratibu wa kikatiba na kanuni ungefuatwa,” amesema Ruge.
Hata hivyo, katika mazungumzo yake na Mwananchi, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Aman Golugwa amesema mchakato wa kumuondoa Ruge katika nafasi hiyo ulifuatwa taratibu zote.
Amesema Ruge kudai anateuliwa na kamati kuu anajipotosha anateuliwa na mwenyekiti akishauriana na Katibu mkuu na hiyo ndio mamlaka yake ya uteuzi isipokuwa Kamati Kuu inataarifiwa.
“Hawa ni wataalamu watano mwenyekiti kwa mamlaka yake anaweza kushauriana na Katibu Mkuu kwamba ninaona watu, moja mbili, tatu waingie kwenye sekretarieti ili kuleta tija ya utaalamu fulani,”amesema Golugwa.
Wakati Golugwa akieleza hayo, taarifa kwa umma iliyoandikwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia iliyotolewa Machi 12, ilieleza kuwa kikao cha kamati kuu maalumu kimefanya uteuzi wa wakurugenzi kwa mujibu wa ibara 7.7.16(b) ya katiba ya chama hicho, sambamba na watalaamu wa makao makuu kwa mujibu wa ibara ya 7.7.17(e).