Prime
Chadema yamjibu Msajili sakata la uteuzi

Muktasari:
- Msimamo huo wa Chadema umekuja baada ya jana Jumatatu Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kutengua uteuzi wa wajumbe wanane wa sekretarieti na kamati kuu ya Chadema waliothibitishwa na Baraza Kuu la chama hicho Januari 22, 2025.
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemjibu Msajili wa Vyama vya Siasa, kikisema hakitabadilisha chochote katika maelekezo waliyopewa na ofisi hiyo, kwa maelezo kuwa walishafunga mjadala kuhusu kikao cha Baraza Kuu.
Msimamo huo wa Chadema umekuja baada ya jana Jumatatu Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kutengua uteuzi wa wajumbe wanane wa sekretarieti na kamati kuu ya chama hicho waliothibitishwa na Baraza Kuu Januari 22, 2025.
Baada ya utenguzi huo, ofisi hiyo imetoa maelekezo kwa chama hicho kikuu cha upinzani nchini yanayopaswa kufanyiwa kazi ili kukidhi matakwa ya sheria ya vyama vya siasa, kanuni na katiba ya Chadema.

Uamuzi huo umefanyika ikiwa ni kujibu malalamiko yaliyowasilishwa kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Lembrus Mchome akisema akidi ya baraza kuu lililowathibitisha haikutimia.
Mchome alikuwa akilalamika kwamba akidi haikutimia ya kuwathibitisha viongozi hao ambao walikuwa wameteuliwa na mwenyekiti mpya wa Chadema, Tundu Lissu.
Viongozi waliokuwa wanaolalamikiwa na msajili ameamua kuwaweka kando hadi Baraza kuu jingine liitishwe ni Katibu Mkuu, John Mnyika, Amani Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar).
Pia, aliwataja wajumbe wa kamati kuu walioteuliwa na kuidhinishwa na Baraza Kuu, Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk Rugemeleza Nshala ambaye pia aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa chama hicho.
Barua ya Mchome kwenda kwa msajili ya kwanza aliiandika Februari 18, 2025 akilalamikia uteuzi wa viongozi hao.
Ilichosema Chadema
Leo Jumanne, Mei 13, 2025, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche akihutubia mkutano wa hadhara unaonadi ajenda ya No reforms, no election, Mgumu, wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara amesema chama hicho bado kinamtambua John Mnyika kuwa ni katibu wa chama.

“Wamechukua baadhi ya watu tuliokwa nao wamewapa… eti wajifanye wanajitoa kwenye Chadema, sasa ile Chadema wanaojitoa wananchi ndio hawa hapa. Sasa ya mwisho ndio hii, msajili amesema hamtambui katibu mkuu wa chama chetu, hatambui wajumbe wa kamati kuu wa chama chetu.”
“Namwambia msajili hahitaji kumtambua katibu mkuu wa chama chetu, sisi Chadema tunamtambua katibu mkuu wetu, huna uwezo wa kututeulia nani awe katibu mkuu wa chama chetu. Msimamo wa chama chetu, katibu mkuu wetu atateuliwa na mwenyekiti kama katiba inavyosema na mwenye malalamiko akate rufaa katika mkutano mkuu,” amesema Heche.
Huku akishangiliwa, Heche amesema Chadema hawatabadilisha chochote kati ya yaliyofanyika, kwa maelekezo ya msajili, akisema wameshamaliza na wamefunga mjadala.
“Msajili kama una nguvu ifute Chadema, usitupige mkwara sisi…,” amesema Heche.
Pia, Mwananchi limewatafuta viongozi mbalimbali wa ofisi ya msajili akiwemo Msajili mwenyewe, Jaji Francis Mutungi na au Naibu Msajili, Sisty Nyahoza bila mafanikio.
Walichokisema wachambuzi
Mwananchi limezungumza na wanazuoni juu ya hilo na mengine yanayoendelea ndani ya Chadema ikiwemo wanachama wake kujiuzulu, kesi ya uhaini na ya kuchapisha taarifa za uongo mitandaoni inayomkabili Mwenyekiti wake, Tundu Lissu ambapo wamesema hatua hiyo inakirudisha nyuma.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema Chadema kinapitia katika tanuru la moto, kinazongwa kila kona kuanzia ndani hadi nje.
“Chadema kila kona inazongwa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, anayepaswa kuwa mlezi anawashughulikia, Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini, ukirudi ndani ya chama wanapigwa na lile kundi lililoshindwa uchaguzi. Ule uchaguzi umewavuruga na kukipasua Chadema,” amesema Dk Mbunda.
“Ni chama kinachoshambuliwa kila kona, jinsi watakavyoweza kujinasua katika mazingira haya ndiko kutaonyesha uimara wa chama na viongozi wa sasa waliopo madarakani,” amesema Dk Mbunda.
Wakati Dk Mbunda akieleza hayo, Mhadhiri mwingine wa UDSM, Dk Aviti Mushi amesema kwa yanayoendelea anaiona Chadema ikikosa mwelekeo kutokana na misukosuko inayokipitia chama hicho.
“Chadema inakoelekea inakwenda kukosa nguvu, jambo ambalo si afya katika siasa za Tanzania, kwa sababu sioni chama cha upinzani kitakachotoa upinzani kwa CCM zaidi ya Chadema. Kitendo cha Lissu kuwekwa ndani huku Chadema yenye ikishughulikiwa haileti picha nzuri,” amesema.

“Naiona Chadema ikivunjika nguvu, ndicho ninachokiona kwa sasa, huu mkakati unakwenda kuwapunguza nguvu zao za ushindani, kuanzia vurugu zao za ndani za G55, mara msajili, kule Lissu kuwekwa rumande, wanakwenda kupunguza uwezo wao,” amesema Dk Mushi.
Kwa mujibu wa Dk Mushi, Chadema kilikuwa katika nafasi nzuri ya kuleta ushindani, lakini kwa hali ilivyo na yanayoendelea, haoni kama kitaweza kusimama na kurejea katika ubora wake kama miaka ya nyuma.