Heche: Chadema ikishika dola itawalipa pensheni wazee wote

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche akipeana mkono na wananchi wa Nyehunge waliounga mkono kampeni ya 'Tone Tone' kugharamia shughuli za uendeshaji wa shughuli za chama.
Muktasari:
- Ataja sekta ya madini, kilimo, utalii na bandari kuwa vyanzo vya mapato
Geita/Sengerema. Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche amesema chama hicho ikishika dola italipa pensheni kwa wazee wote nchini wenye umri wa kustaafu.
Akihutubia mikutano wa hadhara katika viwanja vya Kanisa la Wasabato Kijiji cha Nkome Wilaya ya Geita na Nyehunge Wilaya ya Sengerema leo Mei 11, 2025, Heche amesema kila mzee nchini ana mchango wake katika ujenzi wa Taifa bila kujali iwapo waliajiriwa au kujiajiri katika sekta za kilimo, uvuvi na biashara.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Nyehunge, Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema.
"Mfumo wa sasa wa pensheni unawahusu waajiriwa pekee huku wanaojiajiri kwenye shughuli nyingine za uzalishaji kama kilimo, uvuvi, ufugaji na ujasiriamali wakiachwa nje licha ya kuwa na mchango katika ujenzi na maendeleo ya Taifa; Chadema tutarekebisha hilo kwa kuwalipa mafao wazee wote nchini wenye umri wa kustaafu," amesema Heche.
Akifafanua, Makamu Mwenyekiti huyo amesema; "Kila mtu anao mchango katika ujenzi na maendeleo ya Taifa hili, wakulima, wafugaji, wavuvi, wamachinga na wafanyabiashara wanachangia maendeleo ya Taifa; wote wanastahili kulipwa pensheni uzeeni."
Kiongozi huyo amesema Chadema pia itarekebisha mfumo oensheni kwa kuweka uwiano sawa kwa kada zote tafauti na sasa ambapo wanasiasa hulipwa mafao makubwa kulinganisha na watumishi wa umma.
"Mbunge akimaliza muda wake wa miaka mitano analipwa mafao ya zaidi ya Sh300 milioni, wakati mwalimu, askari na watumishi wa kada nyingine wanaostaafu baada ya kutumikia Taifa kwa zaidi ya miaka 30 wanaambulia pensheni kati ya Sh30 milioni hadi Sh200 milioni kutegemeana na cheo chake. Hii siyo sawa na Chadema tutaondoa uonevu huu," amesema Heche.
Amesema Tanzania imejaaliwa wingi wa rasilimali ikiwemo madini ya dhahabu, almasi, chumu, nickel, makaa ya mawe, ureniam, gesi na Tanzanite inayopatikana nchini pekee duniani; rasilimali anayosema ikitumika vema, Serikali iatamudu siyo tu kulipa pensheni kwa wote, bali pia utekelezaji wa miradi ya maendeleo bila kutegemea misaada na mikopo kutoka nje.
Amesema licha ya madini, Tanzania ina bandari zinayoyegemewa na mataifa zaidi ya matano, mbuga na hifadhi ya wanyama, ardhi kubwa yenye rutuba, maziwa, mito na mvua za kutosha ambazo zikitumika vema, Taifa litaingiza kipato cha kuendesha shughuli za Serikali bila kuweka mzigo wa kodi na ushuru kwa wananchi.
Ili kurekebisha hali hiyo, Heche amewaomba Watanzania kuunga mkono kampeni ya kudai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi kuweka sawa uwanja wa siasa kuwezesha wananchi kuondoa CCM madakarani kupitia uchaguzi huru na haki.
"Chedema haina ugomvi binafsi na mtu yeyote, hatuna ugomvi na mtu yeyote kuwa CCM au chama chochote cha siasa; bali ugomvi wetu ni uongozi wa Serikali chini ya CCM kuongoza nchi yetu vibaya," amesema Heche.
Amesema Chadema inawasema viongozi wa CCM kwa sababu ndio wenye dhamana ya kuongoza Serikali kwa niaba ya wananchi kwa miaka zaidi ya 63. Hali iliyopo ni dhahiri viongozi wanaotokana na CCM hawawezi kutatua matatizo ya kiuchumi na kijamii yaliyopo kwa sababu ndio wameyasababisha.

Akihutubia mkutano huo, Askofu Maximillian Machumu maarufu kwa jina la 'Askofu Mwanamapinduzi' ameutaka umma wa Kanda ya Ziwa kuamka kwa kuacha kuwa daraja la CCM kupata wingi wa kura kuingia madarakani na baadaye kusahau eneo hilo lenye asilimia takriban 25 ya Watanzania wote.
"Kanda ya Ziwa inayoundwa na mikoa sita ikiwemo Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu, Mara na Kagera ina mawaziri wawili pekee ambao ni Innocent Bashungwa na Doto Biteko kulinganisha na Kanda ya Pwani yenye mawaziri watano. Kanda ya Ziwa tuamke kudai haki ya nafasi yetu kutambulike kwenye uongozi wa Taifa,” amesema Askofu Machumu.
Ameshangazwa na kitendo cha mawaziri wanaoshughulikia sekta za uvuvi na madini ikiwemo dhahabu na almasi, wote wanatoka nje ya mikoa ya Kanda ya Ziwa yenye wingi wa rasilimali hiyo.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila amesema; "Umaskini wa Watanzania siyo mpango wa Mungu kwa sababu nchi yetu ina wingi wa rasilimali chini na juu ya ardhi. Tatizo la umaskini wetu ni sera mbovu ya Serikali ya CCM,"
Amesema mikoa yote sita ya Kanda ya Ziwa ina madini ya dhahabu, ina Ziwa Victoria, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ardhi na mabonde yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji lakini maisha ya wananchi hayaakisi uwepo wa rasilimali hizo.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche akipeana mkono na wananchi wa Nyehunge waliounga mkono kampeni ya 'Tone Tone' kugharamia shughuli za uendeshaji wa shughuli za chama.
"Chadema ikiingia madarakani itahakikisha Kanda ya Ziwa inanufaika na rasilimali zake kupitia sera ya majimbo. Vijana kwa wingi wetu tuwe chachu ya mabadiliko kwa kuunga mkono kampeni ya kudai mabadiliko ya katika, sheria na mfumo wa uongozi utakaorejesha madaraka kwa wananchi," amesema Mahinyila.