Golugwa, wenzake wa Chadema waachiwa

Muktasari:
- Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam lilikiri kumshikilia Aman Golugwa kwa uchunguzi wa tuhuma za kusafiri kwa siri kwenda na kurudi nje ya Tanzania.
Dar es Salaam. Wakili Dickson Matata ameliambia Mwananchi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)-bara, Aman Golugwa ameachiwa usiku huu baada ya kushikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu kwa saa kadhaa.
Matata ameeleza hilo leo Mei 13, 2025 kufuatia taarifa ya Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kukiri kumshikilia kwa uchunguzi wa tuhuma za kusafiri kwa siri kwenda na kurudi nje ya Tanzania.
Taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa mchana wa leo imesema Golugwa amekamatwa saa 6:45 usiku Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, akiwa katika maandalizi ya kusafiri kuelekea Brussels nchini Ubelgiji.
Awali, Chadema kupitia ukurasa wake wa kijamii wa X iliweka taarifa ya kukamatwa kwa Golugwa ikisema: “Alikuwa anasafiri leo Mei 13, 2025, kuelekea nchini Ubelgiji kukiwakilisha chama katika mkutano wa International Democracy Union (IDU) unaoanza kesho nchini humo.”
Akizungumzia na Mwananchi usiku huu Matata amesema wamekamilisha taratibu zote na kiongozi huyo ameachiwa.
"Kweli ameachiwa huru muda si mrefu baada ya kukamilisha taratibu za dhamana yake, pamoja na wengine," amesema Matata ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Magharibi.