Malaika na Hip Hop ya Fid Q ni samaki na maji

Muktasari:
- Hadi anakuwa kimya kimuziki alikuwa bado hajatoa albamu wala EP ila ngoma zake chache alizotoa zinatosha kumtambulisha yeye ni nani na uwezo wake ni upi kimuziki. Huyu ndiye Malaika
Dar es Salaam. Ni wazi Malaika ni miongoni mwa waimbaji wa kike waliojitokeza kwenye Bongofleva na kufanya vizuri kwa kiasi fulani, ana heshima na historia yake aliyojitengenezea kwenye muziki huo ingawa ni kwa kipindi kifupi.
Hadi anakuwa kimya kimuziki alikuwa bado hajatoa albamu wala EP ila ngoma zake chache alizotoa zinatosha kumtambulisha yeye ni nani na uwezo wake ni upi kimuziki. Huyu ndiye Malaika;.
1. Jina alilopewa na wazazi wake ni Diana, kwenye muziki anajiita Malaika, jina alilopewa na Bibi yake upande wa mama, akiwa mdogo Bibi yake alipenda kumuita jina hilo ndipo akalizoea hadi kuja kuanza kulitumia kwenye muziki.
Hiyo ni sawa na Shilole ambaye naye alipatiwa jina hilo na Bibi yake, maana ya jina hilo ni Kioo kwa Kinyamwezi, hiyo ni kutokana alipokuwa mdogo wakati akilia Bibi yake alikuwa akimpatia kioo, na pindi alipojiangalia alinyamaza.

2. Baada ya kushirikishwa na Chege katika ngoma, Uswazi Take Away (2014) ndipo Malaika alivuma kimuziki, wawili hao walikutana kwa Director Adam Juma ambapo Malaika alikuwa akifanya kazi kama mpambaji (makeup artist) kwa wakati huo.
3. Kabla ya muziki, Malaika alicheza filamu, moja ya filamu alizocheza inaitwa 'Mrembo Kikojozi' ambayo ilikuwa na maudhui ya kuchekesha, huku mastaa kama Aunty Ezekiel na wengineo wakishiriki.
4. Malaika ndiye msanii wa kwanza wa kike Tanzania kutoka kwenye Bongofleva kufanya muziki aina ya Mchiriku, ni baada ya kutoa wimbo wake, Mwantumu (2014) ambao aliwashirikisha Chande na Tin White.
Na huo ndio ulikuwa wimbo wake wa kwanza baada ya kufanya vizuri katika wimbo, Uswazi Take Away uliotengenezwa na Prodyuza Tuddy Thomas.
5. Wimbo wa Malaika, Rarua Rarua (2016) vesi ya mwisho ameandikiwa na Rich Mavoko na sehemu iliyobaiki ameandika mwenyewe, ni Mavoko huyu ambaye ndiye pia ameandika wimbo wa Lulu Diva, Ona (2018) ambao wameshirikiana.
6. Malaika ndiye alipaswa kusikika katika wimbo wa Timbulo, Ngomani (2016) na tayari alikuwa amesharekodi ila sauti yake ilikuja kufutwa na nafasi hiyo kuchukuliwa na Nay Lee, mshindi wa Super Nyota.
Hii ni kutokana na Malaika kutokubali kushiriki kwenye video ya wimbo huo, kitu kama hicho kilitokea kwa Heri Muziki ambaye sauti yake ilifutwa katika wimbo 'Waambie' alioshirikisha na Mtangazaji Diva, huku chanzo kikiwa ugomvi wa kimapenzi.
7. Chege alikubali kushirikiana na Malaika kutokana alikuwa anahitaji msanii wa kike ambaye bado hajatoka kimuziki ili asikike katika ngoma yake hiyo na mashabiki kumfahamu.
Ukiachana na Malaika, hadi sasa Chege ameshirikiana na wasanii wa kike Bongo kama Vanessa Mdee (Manjegeka), Nandy (Kilele cha Chura), Ray C (Najiuliza), Saida Karoli (Kaitaba), Phina (Sinsima), Rosa Ree (Boss) n.k.
8. Mesen Selekta ndiye alimfuata Malaika na kumuomba warekodi pamoja wimbo, Sare Sare (2015) ambao ulifanya vizuri na Mesen ndiye Prodyuza wa wimbo huo.
Baada ya hapo ndipo Malaika akaenda kwa Aby Dady na kutoa wimbo wake, Zogo (2015), moja ya nyimbo zake zilizofanya vizuri kwa wakati huo.
9. Kabla ya kuwa kimya kimuziki ndoto kubwa ya Malaika kimuziki ilikuwa kufanya kazi Staa wa Nigeria, Davido na Justin Bieber kutokea nchini Canada, tayari alishakuwa na mipango ya kuhakikisha anawapata wasanii hao.
10. Msanii wa Hip Hop Bongo ambaye Malaika anamkubali sana ni Fid Q na ngoma ya Rapa huyo ambayo anaikubali ni 'Walk It Of' (2016) aliyomshirikisha Taz kutokea nchini Zimbabwe.

Hiyo ni sawa na Hamisa Mobetto ambaye ni shabiki mkubwa wa Mwana FA na wimbo aliyoanza kuupenda kutoka kwa FA ni 'Kama Zamani' (2013) akiwashirikisha Kilimanjaro Banda (Njenje), Mandojo na Domo Kaya. Kwa sasa Mwana FA (Hamisi Mwinjuma) ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.