Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanaume wenye tabia hizi tatu ndio chanzo cha talaka

Wanaume wenye tabia hizi tatu ndio chanzo cha talaka

Muktasari:

  • Wakati sakata la kuongezeka kwa talaka nchini likiibuliwa bungeni jana, imeelezwa makundi matatu ya wanaume ni miongoni mwa sababu za ndoa nyingi kuvunjika.

Dar es Salaam. Wakati sakata la kuongezeka kwa talaka nchini likiibuliwa bungeni jana, imeelezwa makundi matatu ya wanaume ni miongoni mwa sababu za ndoa nyingi kuvunjika.

Hivi karibuni Mwananchi iliripoti habari iliyohusu wingi wa talaka nchini na takwimu kutoka kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) za mwaka 2020 zilionyesha kuwa talaka 511 zilisajiliwa Tanzania nzima na kati ya hizo 221 kutoka Dar es Salaam pekee.

Idadi hiyo ni ongezeko la talaka 69 ikilinganishwa na 442 zilizosajiliwa mwaka 2019 huku Msajili wa ndoa na talaka wa Rita, Jane Barongo akisema Dar es Salaam inaoongoza kwa talaka zinazowasilishwa na wanandoa wenyewe.

Hali ikiwa hivyo, suala hilo jana lilitinga bungeni, ikielezwa suala hilo sasa ni janga la taifa ikishauriwa utafutwe mkakati wa kulikabili.

Baadhi ya watalaamu na wanaharakati waliozungumza na Mwananchi, walirusha lawama za kuvunjika kwa ndoa nyingi kwa wanaume wanaoshindwa kutimiza wajibu wao wa kuhudumia familia kuwa ndio chanzo huku wengine wakisema baadhi ya wanawake wanaingia kwenye ndoa wakiwa na matarajio makubwa kuliko uhalisia.


Makundi matatu

Mmoja wa waliozungumzia suala hilo, Deogratius Sukambi anayejitambulisha kama mshauri wa mahusiano, anasema wanaume wanaoangukia katika kundi la kuchangia ndoa kuvunjika wako katika makundi matatu.

Katika kundi la kwanza, anasema ni wale ambao hawataki kujishughulisha hivyo kutaka kulelewa na wanawake kwa kugharamia kimaisha na kifamilia, maarufu mitaani kwa jina la `Marioo’.

Sukambi analitaja kundi la pili la wananume kuwa ni wale ambao wanafahamu na kutambua majukumu yao, lakini hawana uwezo wa kiuchumi.

Kundi la tatu analotaja Sukambi ni la wanaume wanaoacha kwa makusudi kuhudumia familia pindi wanapoona mwanamke anabeba majukumu hayo.

“Kundi hili la tatu ni hatari zaidi na kukabiliana nalo ni muhimu mwanamke kutambua mwisho wa majukumu yake na kumuacha mwenza wake atimize ya kwake, kinyume na hapo, mwanaume huona amedharaulika.

“Si kitu cha kawaida mwanaume kutegemea kuhudumiwa na mwanamke au kuacha majukumu yake yafanywe na mkewe. Inapofika hatua hii si dalili njema,” alionya.

Lakini Joackim Sekela, mwanandoa yeye analitazama tofauti, anasema siku hizi baadhi ya wanawake wanaingia kwenye ndoa wakiwa na matarajio makubwa lakini wanakuta mambo tofauti, na hapo ndio visa vinaanza.

“Hilo linachangia wanaume kuamua kujiweka kando na kila mmoja kuendelea na ustaarabu wake. Ni muhimu wanawake kutambua uwezo wa wenza wao,” alisema Sekela.

Pamoja na mawazo hayo tofauti, Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake (Tawla), Tike Mwambipile anasema kulingana na sheria ya ndoa mwanaume ndiye mwenye jukumu la kulea familia isipokuwa pale kunapotokea changamoto kama za ugonjwa au nyingine zinazomfanywa ashindwe kufanya kazi.

“Hilo lipo wazi kwenye sheria anayekiuka anakwenda kinyume na sheria na tumekuwa tukizipata kesi hizi mara kwa mara. Wanaofika tunazungumza, yanayoshindikana yanakwenda ustawi wa jamii hadi mahakamani,” alisema Tike.

Kwa upande wake, Rose Reuben, mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, anasema kukosekana kwa mawasiliano baina ya wenza kunachangia kwa kiasi kikubwa hali hiyo ambayo inashika kasi.

“Kesi za aina hii huwa zinakuja na zimegawanyika katika makundi mawili, kuna wanaume ambao uwezo wao ni mdogo kuliko mahitaji wanayotaka wanawake na wapo pia ambao ni kweli wametelekeza majukumu kwa wenza wao kwa sababu wanaweza kujitafutia.

“Kutatua hili tunakaa na wenza wote wawili na kuzungumza nao,” alisema Rose.

Lakini Ofisa wa ustawi wa jamii, Vicky John alisema mwenendo wa wanaume huchangia kwa kiasi kikubwa ndoa kuvunjika kutokana na baadhi ya wanawake kuchoka kuendesha familia.

“Unakuta mwanamke amekuja anakwambia nataka taratibu za kupata talaka maana mume hana msaada wowote kwake, sasa anaona bora waachane,” aliongeza.


Majukwaa ya wanaume

Wakati wengi wa waliozungumzia suala hilo wanaeleza chanzo cha tatizo, Sayuni Mero, aliyeko pia katika ndoa anashauri ya kuondokana na tatizo kwa kuwakutanisha wanaume kuzungumzia masuala ya familia ikiwamo kuwakumbusha majukumu yao.

Anasema kuna majukwaa mengi ya wanawake ambayo yanawafunza na kuwakumbusha majukumu yao na namna ya kuhudumia familia, lakini wanaume wanakosa mafunzo kama hayo, na hivyo kujisahau.

“Vitabu vya dini vimeandika mwanaume atakuwa kichwa cha familia, lakini mambo yamebadilika, mke akionekana ana kipato basi anaachiwa majukumu. Kama kuna kodi ya nyumba atalipa, ada za watoto atatoa na bado mahitaji ya kila siku ya nyumbani yanamsubiri.

“Binafsi naweza kukusamehe hata nikikufumania kila siku, lakini majukumu yako ya nyumbani uyatimize. Sio nyumbani hueleweki, watoto hujui wanasomaje halafu bado nivumilie kila siku kukukuta na michepuko, hiyo haiwezi kuwa ndoa,” alisema Sayuni, ambaye ni mfanyabiashara.

Suala la majukwaa pia linazungumziwa na Edna Mihayo, ambaye pia ameolewa, akisema kama wanawake wanavyokumbushwa majukumu yao ni muhimu pia kukawa na majukwaa ambayo yatawakutanisha wanaume kuhusu nafasi zao kwenye familia.

“Wanaume mikusanyiko yao ni kwenye pombe, kungekuwepo na `forums’ (majukwaa) ambayo zinawakutanisha kwa ajili ya kuzungumza mambo ya familia, majukumu yao na mambo yanayowahusu, ingesaidia kunusuru ndoa nyingi. Kwa wanawake tunaona kuna matukio mengi yanayowakutanisha pamoja na kujadili namna ya kujikwamua kiuchumi,” alisema Edna.


‘Kuku wa kizungu’

Suluhisho la muda mrefu linatolewa na Sukambi akisema lianze kwa kubadili mtazamo wa watoto na hivyo wazazi kuacha kuanzia sasa kuwalea kama ‘kuku wa kizungu’.

“Yaani kila anachokitaka mtoto anakipata kwa wakati anaotaka. Hii haimsaidii mtoto, anakuwa akiamini kwamba anastahili kupewa kila anachohitaji. Hili ni bomu lingine linalokuja miaka 20 ijayo kutokana na wazazi wengi tunavyolea watoto,” alionya Sukambi.

Anashauri watoto walelewe katika mazingira yatakayowajengea kuchangamsha ubongo na si kuwa na uhakika wa kila anachokiamini.

“Mtoto anapaswa kuelewa si kila anachotaka atapata kwa wakati anaotaka, yaani siku hizi utasikia mtoto anaamua shule hii haitaki anataka ile, ni muhimu wazazi tuwafundishe kwamba kwenye ulimwengu huu si kila unachotaka utakipata kwa urahisi.

“Pia tuache kuwafuatilia na kuwalinda kupita kiasi. Hii haimsaidii mtoto, wakati mwingine muache uone namna anavyoweza kutanua mawazo yake na kushughulisha ubongo. Mpe mtoto nafasi ya kutoa mawazo na afahamu kuwa si kila mawazo yake yatakubaliwa na ikitokea hayajakubaliwa mpe sababu,” alishauri Sukambi.


Tatizo latinga bungeni

Suala la talaka ni mjadala nje na hata ndani ya Bunge baada ya jana kuibuliwa na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Najma Giga aliyesema ni janga la taifa.

Akichangia hotuba ya Rais John Magufuli wakati akizindua Bunge la 12 Novemba 13, 2020, Giga alisema matatizo ya talaka yamekuwa mengi nchini na yakiachwa bila kuundiwa mkakati huenda yakazidi kuwa mengi zaidi.

Giga alizitaka mamlaka husika kufanya uchunguzi wa mambo hayo na kutafuta njia ya kufanya, vinginevyo huenda likawa kubwa zaidi. “Mimi nitashirikiana na wenzangu katika kipindi hiki cha miaka mitano kuhakikisha tunapata suluhu ya jambo hilo, lazima tutazame kuwa ni janga kwa sasa, alisema Giga ambaye ni mwanasheria.

sababu za talaka

1. Kukosekana uaminifu

2. Kutelekeza familia

3. Matarajio kuliko uhalisia

4. Uchumba wa mwendokasi

5. Usiri katika ndoa