Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Huu ndio msimamo wa Rungwe kwa makada Chadema

Muktasari:

  • Mwananchi lilifanya mahojiano maalumu na Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe kuhusu undani wa jambo hilo, ambaye anaeleza kwamba wanachama hao waliojivua uanachama wa Chadema.

Dar es Salaam. Wakati jinamizi likiendelea kukitikisa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mamia ya wanachama wake wametangaza kukihama chama hicho huku wakitajwa kuhamia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Licha ya kwamba wanachama hao hawajaweka bayana chama wanachokwenda kujiunga, duru za ndani zinaeleza kwamba waliokuwa viongozi na wanachama wengine wanakusudia kujiunga na Chaumma kuendeleza siasa zao.

Chaumma, kikiwa moja ya vyama 19 vyenye usajili wa kudumu nchini, kimejipanga kuwapokea wanachama hao endapo watataka kwenda kujiunga nao na kuhusu masuala mengine ya mgawanyo wa madaraka watajadiliana.

Mwananchi lilifanya mahojiano maalumu na Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe kuhusu undani wa jambo hilo, ambaye anaeleza kwamba wanachama hao waliojivua uanachama wa Chadema, bado hawajafika kwake.

Rungwe anasema kwamba mwanachama kuhama chama kimoja kwenda kingine, anatumia uhuru na haki yake aliyopewa kikatiba; kuanzia chama tawala cha CCM na vyama vingine vyote, ikiwemo Chaumma.

“Wana uhuru kujiunga na vyama vingine, kuhusu waliokuwa wanachama wa Chadema kuja kwangu, bado hawajaja. Nami nasikia tu kwenye magazeti na wala hatujafanya mazungumzo yoyote,” anasema Rungwe.

Rungwe, ambaye ni maarufu kama Mzee wa Ubwabwa, anafafanua kwamba iwapo watakwenda kujiunga na chama hicho, atafurahi na milango iko wazi kwao muda wowote, huku akisema huenda bado wanaangalia uwezekano.

“Hapa Chaumma bado hawajafika, nafikiri zamu yetu bado, lakini wakija hapa tutakuambia, kwa sababu hakuna kitu cha kuficha, hawajaja na hicho ndicho nakifahamu hadi sasa,” anasema mwanasiasa huyo.

Rugwe anasisitiza kwamba: “Vyama hivi ni mali ya umma, mtu anaweza kutoka CCM akaja huku, ni sawa, kwani kuna tatizo gani, si Mtanzania, kwa nini tujipe mamlaka hiki chama si changu, ni cha wananchi.”

Rungwe anasema vyama ni mali ya wananchi, wakati wowote wanatoka na kwenda kujiunga na vyama vingine na huo ni utaratibu na si jambo jipya.

“Wakija milango iko wazi, hata sasa hivi kama wanakuja na wakija na sharti la kuhitaji nafasi za uongozi, hilo tutajadiliana na wakubwa wangu wengine na kupata mwafaka, ni jambo la kawaida,” anasema Rungwe.


Mkutano mkuu wakwama

Rungwe anaeleza kwamba mchakato wa kupata wagombea ndani ya chama hicho umeanza, lakini wameahirisha kwa muda kufanya mkutano mkuu kwa sababu ya kukosekana kwa fedha kwa ajili ya maandalizi ya mkutano huo.

“Tumekosa hela kwa ajili ya kuandaa mazingira, ikiwemo ukumbi na kugharimia malazi ya wajumbe wanaotoka mikoani, kwa hiyo tumesogeza mbele kujipa muda tuongezee kiasi ili tufanye mkutano,” anasema.

Awali, chama hicho kilipanga kufanya mkutano mkuu Mei 11 na 12, mwaka huu, hata hivyo kikasogeza mbele, sasa mkutano mkuu utafanyika Juni 27 na 28 ambapo watapitisha jina la mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar.

Rungwe anasema haiwezekani wajumbe wanatoka mikoani kuja Dar es Salaam kwenye mkutano mikononi wasiwe na chochote kitu, vinginevyo hapatakalika, kutakuwa na kelele nyingi za malalamiko.

“Mfano, gharama za kulipia ukumbi kama pale Mlimani City, lazima uwe na Sh10 milioni, wajumbe wanahitaji kula, wanahitaji malazi, vitu vingi vinahitajika ili kufanya shughuli yetu ionekane,” anasema.

Kwa mujibu wa Rungwe, wanatarajia kupokea wajumbe zaidi ya 400 kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini kwa ajili ya mkutano mkuu. Anasema chanzo kikubwa cha mapato wanachotegemea kupata fedha ni michango ya wanachama na misaada ya wadau.

“Chanzo chetu kikubwa cha fedha ni kupitia malipo ya kadi, lakini tukipata wahisani fedha zikipatikana, zinasaidia kuendesha shughuli zetu,” anasema mwenyekiti huyo.

Anasema wanatafuta fedha kujiandaa na uchaguzi huo na kwamba hawawezi kususia au kuingia kwenye mipango ya vyama vingine vinavyodai haviwezi kuingia kwenye uchaguzi hadi mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi.

“Mawazo yao ya kususia uchaguzi ni sawa na wengine wanaoshiriki pia wako sawa. Sisi tutangoja mabadiliko yatakapokuja taratibu na tumekuwa tukilalamikia hizi kanuni lakini haziwezi kututoa kwenye uelekeo wetu,” anasema.

Anasema hawawezi kususia uchaguzi, huku akihoji kwamba kuna sheria nyingi zimebadilishwa nchini lakini kwa taratibu na kuwa baadhi ya vyama, kupitia sheria hizo, vilipata hadi wagombea 70 na 80.

“Sawa sheria ni mbaya, sasa tunafanyaje? Lazima tujue kitu tunachokiambia kina mamlaka na kimepewa na wabunge. Chaumma hatuko hapa kupingana na mamlaka, tutalalamika na kutoa mawazo yetu na uchaguzi tunashiriki,” anasema.

Rungwe anasema siku wakisikia na kuridhia kile wanacholalamikia, watafanya mabadiliko, huku akitolea mfano Zambia, Hakainde Hichilema aliyegombea mara saba, wengi walikuwa hawamjui lakini walishangaa ameshinda.

“Sasa wewe unasema huwezi kushiriki uchaguzi peke yako. Nafikiri wengi wape, angalieni ni wangapi wanasema uchaguzi usifanyike, ni wachache lakini kura inaangukia kwa wengi, inabidi wapewe,” anasema.

“Muda ukifika mtegemee jina la Rungwe kuliona katika nafasi ya urais, ingawa nakutana na upinzani mkali, kuna wanaosema nimekaa sana, nimekaa muda mrefu, vipi mbona Nyerere alikaa mika 25 na hakuna mtu aliyeongea hadi aliamua kuondoka mwenyewe,” anasema.


Muungano wa vyama kukwama

Kwa mujibu wa Rungwe, vyama vya upinzani nchini vinashindwa kuungana kuikabili CCM kwa sababu ya ile dhana iliyojengeka ya kiburi kwa baadhi ya vyama kujiona ni vikubwa kuliko vingine.

“Kama kingine kinajiona kikubwa na mimi nitajiona mkubwa vilevile, ndiyo maana tunashindwa kwenda kuzungumza na fulani, kila mtu ana kiburi chake, huyu anajidai mkubwa, anaowaona wadogo nao wanafanya jeuri zao,” anasema.

Mbali na hilo, Rungwe, ambaye ni wakili, anasema kuna sababu nyingine za kisheria zinakwamisha jambo hilo, ingawa haziwezi kuwa kikwazo cha wao kushindwa kushirikiana na kuelewana, hasa kipindi cha uchaguzi.


Chaumma kinakua

Mwenyekiti Rungwe anasema Chaumma kinakua, licha ya kuwa sasa kimefikisha miaka 18 na kila mwaka kinashiriki uchaguzi.

Anadai kwamba hata Chadema wakati kinaanza kilikuwa cha kawaida kabisa, ingawa kilijivutavuta na kuwa chama kikubwa kilichovuna wabunge wengi.

“Kilianza kupata mbunge mmoja, lakini ilifikia hatua kikawa hadi na wabunge zaidi ya 70. Ukuaji ni taratibu na walichukua zaidi ya miaka 15, Chaumma hatuwezi kuwa na haraka ili mradi tunafanya siasa zinazokubalika na wananchi,” anasema.

Anasema chama hicho kitaendelea kutetea maslahi ya raia na si matusi wala vitisho na hawawezi kuiga vyama vingine kupita kufanya operesheni.

“Kumbukeni tunashindwa kufanya mikutano ya hadhara kwa sababu ya fedha, sasa kama hatuna hiyo rasilimali tutakwenda vipi, hao mnaosema wanaonekana ni baada ya kupata fedha, sasa ni vitu ambavyo viko wazi,” anasema.

Rungwe anasema kuna vyama vina misuli ya fedha wanazozikusanya kupitia ruzuku, huku akisisitiza hakuna chama kidogo wala vya kawaida, isipokuwa kuna vyama ambavyo havina wawakilishi bungeni.


Dhana ya kutumika

Rungwe anapinga kwamba vyama visivyo na uwakilishi vimekuwa vikitumiwa na CCM kwenye ajenda zake, huku akifafanua kwamba kushiriki mialiko wanayopewa na Serikali na wanayokwenda ni haki yao na wasichukuliwe kwamba wanatumika.

“Rais akiniletea barua lazima nitaenda, nikatae ili iwe vipi? Sasa utamtii nani, yule ni kiongozi, lazima tumtii na tusipoenda tutaonekanaje? Tutakuwa watu wa ajabuajabu, ni sawa ukubali baadhi ya mambo lakini nenda ukiitwa, kwanza kule kunakuwa na ubwabwa,” anasema.

Kulingana na Rungwe, anaenda kukiwakilisha chama chake na ni mialiko inayoenda kwa vyama vyote na si sawa kuwachukulia wanaoenda wanatumika.

“Usipoenda ni shauri yako, kwanza si lazima wewe uende, unajua kwenye jambo hili ni yale majivuno niliyokuambia, wana kiburi na wanataka kuwaambukiza wengine, mimi mtu mzima siwezi kuingia kwenye mambo hayo ya kifedhuli, kwani kila unalosema wewe ni haki?” anahoji.


Matukio ya utekaji

Rungwe anasema mambo ya utekaji yanayoendelea nchini hayafai, hususan tukio la hivi karibuni la kada wa Chadema, Mdude Nyagali ambaye hajulikani alipo. Anahoji kwamba inakuwaje matukio hayo yanatokea halafu Jeshi la Polisi limekaa kimya.

“Nilishawahi kutoa maoni, Polisi waliopo madarakani wote waondolewe, tuajiri wengine kwa sababu waliopo hawawezi kazi na nimesema mara kadhaa, wote waondoke kazini, ikiwezekana tuchukue wanajeshi wafanye shughuli hii kwa muda,” anasema.

Mwanasiasa huyo anasema Polisi waliopo sasa wameshindwa kukabiliana na vitendo hivyo na wamekuwa wakilalamikiwa kila uchwao.

“Maoni yangu, hawa Polisi waliopo hawatufai, wanatufanya tuwe na wasiwasi na nimebadili hata mtindo wa kuondoka hapa kazini siku hizi huwa nawahi kundoka kwenda zangu nyumbani, ingawa wanakuja hadi nyumbani na kutolewa kitandani, unapigwa,” anasema.

Rungwe anasema kuna matukio mengi ya kusikitisha, hata lile la Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padri Charles Kitime ni aibu, kwa nini kiongozi huyo wa dini ashambuliwe.

“Hali ya utekaji nchini si nzuri, wananchi wanakuwa na hofu na ushauri wangu polisi hawa waondolewe tuajiri wengine na waliopo warudi mtaani wakafanye shughuli nyingine na tuajiri wengine watakaotufanya tuwe na amani zaidi,” anasema Rungwe.

Chaumma kilisajiliwa rasmi Juni 4, 2013 kikiwa ni miongoni mwa vyama vya siasa 19 vilivyopo nchini. Chama hicho kinaongozwa na mwenyekiti wake, Hashim Rungwe.

Tangu chama hicho kimeanzishwa, hakijawahi kushinda nafasi ya ubunge wala udiwani. Katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka 2024, chama hicho kilifanikiwa kushinda mtaa mmoja uliopo jijini Mbeya.

Katika kusherehekea tukio hilo, chama hicho kilifanya sherehe kwa kupika ubwabwa, kama ishara ya sera ya ubwabwa iliyoasisiwa na Rungwe ambayo aliinadi katika kampeni zake za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Katika uchaguzi wa mwaka 2020, Rungwe alishika nafasi ya saba akipata jumla ya kura 32,878.

Waliomtangulia kwenye uchaguzi huo ni John Magufuli (CCM), Tundu Lissu (Chadema), Bernard Membe (ACT Wazalendo), Leopold Mahona (NRA), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), John Shibuda (Ada-Tadea).