Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema yaishukia Chauma, Hashimu Rungwe akitupia ‘bomu’

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akihutubia mkutano wa hadhara eneo la Igoma jijini Mwanza. Picha na Peter Saramba

Muktasari:

  • Wamewatuhumu baadhi ya makada wake wanaojivua uanachama kwa kupanga kujiunga na Chaumma kwa ahadi ya ubunge na udiwani, wakidai ni njama za kukidhoofisha chama hicho. Mwenyekiti wa Chaumma, Hashimu Rungwe, amesema hana taarifa kuhusu madai hayo.

Sengerema/Mwanza. Viongozi wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), wametegua kitendawili cha chama gani watajiunga nacho wanachama na makada wa chama hicho wanaojivua uanachama.

Kitendawili hicho kimeteguliwa kwa nyakati tofauti leo Mei 12, 2025 wakati wa mikutano ya hadhara ya kampeni ya "No reforms, No election".

Zakaria Obadi, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, ndiye alikuwa wa kwanza kueleza hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Stendi ya zamani mjini Sengerema, akisema makada hao watajiunga na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) baada ya kupata ahadi ya nafasi za ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu ujao.

Akifafanua, Obadi amesema kuna njama zinafanyika kukidhoofisha Chadema kupitia kwa baadhi ya waliokuwa viongozi, wanachama, na makada wa chama hicho ambao wanatangaza kujivua uanachama kuaminisha umma kwamba kuna mgogoro ndani ya chama.

 “Tumepata taarifa kuna kichama kinaitwa Chauma kinaandaliwa kizunguke na chopa na magari nchi nzima kiwe mbadala wa Chadema na kimeshapewa mabilioni ya fedha kwa ajili ya kazi hiyo," amesema.

Hivyo, amewaomba wana Chadema kukilinda na kukihami chama hicho kwa akili na nguvu zao zote.

Hata hivyo, alipoulizwa na Mwananchi kuhusiana na madai hayo ya Chadema na baadhi ya waliokuwa viongozi, wanachama, na makada wa Chadema kuhamia Chaumma, Mwenyekiti wa chama hicho, Hashimu Rungwe, amesema hajui lolote kuhusu hilo, huku akiwarushia mpira wanaosema hivyo kwamba ndio wanajua vizuri na waulizwe wao.

“Waulizwe kwa undani (wanaosema hivyo) inawezekana wanalijua jambo hilo na wanaweza kuwa na majibu sahihi. Lakini kama chama bado hatujapata taarifa yoyote,” amesema Rungwe.

Leo ni mara ya pili kwa Rungwe kujibu fununu hizo. Wiki iliyopita aliliambia Mwananchi kuwa kazi moja wapo ya chama cha siasa ni pamoja na kuandikisha wanachama wapya.

“Japo sina taarifa, ila kama watakuja kuomba kujiunga na chama chetu na kama watakuwa wamekidhi viwango, tutawapokea, ila kwa sasa sina taarifa yoyote,” alisema Rungwe.

Akihutubia mkutano wa hadhara eneo la Igoma jijini Mwanza, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, naye amegusia uwepo wa taarifa za waliokuwa makada wa chama hicho kupanga kuhamia vyama vingine vya siasa.

"Baada ya Chadema kuweka msimamo wa kutoshiriki uchaguzi bila mabadiliko, CCM wanafanya mpango wa kuvitumia vyama vingine kushiriki uchaguzi kuonyesha dunia na jumuiya za kimataifa kwamba Tanzania kuna uchaguzi wa kidemokrasia na wamewaahidi baadhi ya waliokuwa wanachama na makada wa Chadema waende vyama vidogo vya upinzani kuhamia huko kwa ahadi ya nafasi za ubunge na udiwani; dawa ya watu hawa ni kuwapuuza," amesema Mnyika.

Ingawa Mnyika hakutaja jina la chama chochote cha siasa, umati uliokuwa ukimsikiliza ulipaza sauti ukitaja chama cha Chaumma, hali iliyomfanya kiongozi huyo kuutaka umati huo kurudia.

"Kumbe mnajua? Hebu rudieni tena. Mmetaja chama gani?" amesema Mnyika, na umati kujibu kwa kupaza sauti, Chaumma.

Mtendaji Mkuu huyo wa Chadema amesema kuna jitihada zinafanyika za kushambulia taasisi hiyo, juhudi alizosema hazitafanikiwa kwa sababu Chadema ni sawa na imani kwa wanachama wake.

"Wanashambulia taasisi ya Chadema kwa lengo la kukidhoofisha, lakini hawatafanikiwa," amesema.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema, naye amezungumzia suala la waliokuwa makada wa chama hicho kujivua uanachama akiwataka wenye nia hiyo kuharakisha kuondoka ili chama kibaki salama.

"Hatuwezi kuwa na kundi la watu ambao matamanio yao ni vyeo, badala ya maslahi na maisha ya Watanzania," amesema Lema.

Akionyesha msisitizo, Lema amesema: "Tumezika watu wengi kwa sababu ya uchaguzi, wapo wana Chadema wameenda magereza, wapo watoto wamebaki yatima na wanawake wamekuwa wajane kwa waume wao kuuawa kwa sababu ya uchaguzi.”

Amesema ndoto ya Chadema si kupigania ubunge, bali ni mabadiliko na maisha bora ya Watanzania.

"Yeyote asiye katika malengo haya hatufai na siyo mmoja wetu," amesema.

Akizungumzia madai ya kuwepo ahadi ya ubunge na udiwani kwa vyama vya siasa, hasa kwa makada na wanachama wa Chadema wanaojivua uanachama, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila, amehoji kwanini ahadi hiyo inahusu ubunge na udiwani pekee na si nafasi ya urais.

"Kama kweli wana roho nzuri ya kuwagawia ubunge na udiwani watu wanaotoka Chadema, basi wafanye hivyo kwa kuwagawia hadi nafasi ya urais pia," amesema Mahinyila.

Kiongozi huyo wa vijana amewashangaa wanaolaghaiwa kwa ahadi za aina hiyo kwa sababu wapo watu kutoka vyama vya upinzani walipewa ahadi za namna hiyo Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, lakini wakaambulia patupu.