Chadema bado hali tete, makada wengine 100 wajivua uanachama

Tabora. Jumla ya wanachama 110 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Tabora wamejivua uanachama wa chama hicho.
Miongoni mwa wanachama waliojivua uanachama ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema mkoani humo, James Kabepele.
Wanachama hao wamesema miongoni mwa sababu zilizopelekea kujivua ni pamoja ni kudharauliwa mawazo yao ndani ya chama, hawako tayari kutokushiriki uchaguzi kwani hiyo ni haki yao ya msingi.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora, James Kabepele amesema baadaye watasema rasmi kuwa watajiunga na chama gani kwa sababu siasa ni maisha ni lazima waifanye.
Mapema jana, viongozi Mei 11, 2025 viongozi 58 wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho mkoa, Gervas Mgonja walitangaza kujivua uanachama wa chama kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa chama hicho.
Viongozi wengine waliojivua ni Katibu wa Bawacha Kanda ya Kaskazini, Rachael Sadick, Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Kilimanjaro, Grace Kiwelu, Mjumbe wa kamati ya Tehama Kanda ya Kaskazini, Answary Kimaro na Mwenyekiti wa Chadema mstaafu Mkoa wa Kilimanjaro, Michael Kilawila.
Jana pia kundi la makada 80 wa chama hicho Mkoa wa kichama Temeke jijini Dar es Salaam walijivua uanachama.
Kundi hilo la makada 80, liliongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa kichama Temeke, Helman Kiloloma, wenyekiti wa wilaya ya Temeke, Hamza Kinyema, Mjumbe na Mratibu wa Mkoa wa Temeke, Mjumbe wa Jimbo la Mbagala, Ivon Haule na Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Makangarawe, Josephine Mwenda.
Uamuzi wa wanachama hao pia, unatokana na sababu kama zilizoelezwa na waliohama awali, kwamba ajenda ya kuzuia uchaguzi inayoendeshwa na viongozi wakuu wa chama hicho, inafifisha ndoto zao za kisiasa.