Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema bado bundi kaweka kambi, wengine 80 wajitoa

Muktasari:

  • Makada wengine 80 wa Chadema wamekipa mkono wa kwa heri chama hicho, huku wakitangaziwa kujiandaa kwani Mei 18 ni siku rasmi watakayokutana na kuamua rasmi wanaenda kujiunga na jukwaa gani la kisiasa.

Dar es Salaam. Safari ya wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kufungasha virago ndani ya chama hicho na kusaka majukwaa mengine ya kufanya siasa zao, imeungwa mkono na kundi lingine la makada 80 wa Mkoa wa kichama wa Temeke jijini Dar es Salaam.

Idadi hiyo ya waliotangaza kukihama chama hicho, inafanya jumla ya waliotimka kutoka Chadema ifikie 101 ukijumuisha na makundi yaliyohama tangu siku tano zilizopita, wakiwemo waliokuwa wajumbe wa sekretarieti ya Chadema kwa miaka kadhaa.

Kundi hilo la makada 80, linaongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa kichama Temeke, Helman Kiloloma, wenyekiti wa wilaya ya Temeke, Hamza Kinyema, Mjumbe na Mratibu wa Mkoa wa Temeke na Mjumbe wa Jimbo la Mbagala, Ivon Haule na Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Makangarawe, Josephine Mwenda.

Uamuzi wa wanachama hao pia, unatokana na sababu kama zilizoelezwa na waliohama awali, kwamba ajenda ya kuzuia uchaguzi kiliyonayo chama hicho, inafifisha ndoto za kisiasa za wanachama.

Wakati makada hao wakiendelea kutoa mkono wa kwa heri kwa chama hicho, Julius Mwita aliyekwishakihama chama hicho tangu awali, leo Jumapili, Mei 11, 2025 katika hafla hiyo ametaka makundi hayo yaliyohama yajiandae Mei 18, 2025 ni siku ambayo watakayokutana na kuamua rasmi wanajiunga na jukwaa lipi.

"Tujiandae kikamilifu kwa sasa viongozi wenu tunaandaa ukumbi wa kukutana hiyo Mei 18, 2025 tukipata tutawaambia siku hiyo tutavaa na fulana za rangi ya hicho chama tutakachoelekea, tunataka kuwaonyesha kwamba hatujaondoka kwa sababu ya kusaka vyeo," amesema Mwita.

Akizungumza uamuzi huo katika mkutano uliofanyika Buza, Temeke, Kiloloma amesema amekaa na kutafakari kwa kina hawezi kuendelea kukaa kwenye chama ambacho tayari kimeshapoteza dira na uelekeo wa kisiasa.

"Nikiwa na masikitiko makubwa napenda kuutangazia umma mimi Kiloloma nikiwa na wanacha wenzangu na viongozi natangaza rasmi kujivua uanachama wangu na vyeo vyangu kuanzia sasa si mwanaChadema tena.

"Nimekuwa mwanachama wa Chadema tangu mwaka 2006, nikiwa bado kijana mdogo na nimekitumikia kwa nafasi mbalimbali kwa weledi mkubwa na uaminifu, lakini tulipo na tunakoenda hakuna uelekeo wowote najiondoa naunga mkono wenzangu waliohama," amesema. 

Katika maelezo yake, Kiloloma ametaja sababu za kujiondoa ni kujiona hawako salama kwani tangu kupatikana uongozi mpya wamekuwa wakibaguliwa kwa kigezo kwamba walikuwa kambi ya mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Freeman Mbowe.

"Ubaguzi huo umeendelea kuanzia siku hiyo si kwa mimi tu na kuna wenzangu waliofukuzwa uanachama kwa sababu tu hawaungi mkono falsafa za uongozi mpya," amesema Kiloloma.
Amesema jambo la pili la kujiondoa ni chama hicho kushindwa kushiriki uchaguzi mkuu wa 2025, kupitia slogani yao waliyoanzisha ya 'No reforms, no election, (mila mabadiliko hakuna uchaguzi).

"Tulitoa ushauri hatukusikilizwa matokeo yake tunatishiwa kufutwa vyeo na  uanachama tumeamua kujiondoa kuungana na wenzetu waliochukua uamuzi kama huu," amesema Kiloloma.
Mbali na sababu hizo ametaja nyingine ni ubaguzi na kuwatenga viongozi waliokipigania chama kwa muda mrefu katika uongozi mpya na kuwakweka watu wengine wapiga dili.

"Hapa wapo wanachama 80 wanaondoka Chadema, lakini kuondoka kwetu si kwamba wameisha bado wapo wengine watatufuata na hizi ni salamu tu na waliobakia tunawaheshimu na wanapaswa kutuheshimu kulingana na uamuzi wetu," amesema.

Amesema wameondoka kwenye chama hicho kwa moyo mmoja na wala hawajalambishwa asali isipokuwa Chadema imepoteza dira na mwelekeo wa kisiasa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Temeke, Hamza Kinyema amesema uongozi uliopo sasa una visa na visasi, hivyo si tegemeo katika ukombozi wa umma tena.

"Tumejiuliza maswali mengi hatuwezi kuungana na wenye visasi tumeamua kuondoka na ukizingatia kwenye magrupu ya WhatsApp hakuna mipango ya kujenga chama ni mwendo wa matusi muda wote na imefikia hatua sifungui simu yangu," amesema.

Amesema wanakihama chama hicho na nguvu zao zinaelekezwa kwenye chama kipya ambacho watakitangaza baadaye.
Naye, Mjumbe Mratibu wa Mkoa wa Temeke, na Mjumbe wa Jimbo la Mbagala Ivon Haule amesema licha ya kwamba moyo wake unauma lakini ameamua kujivua uanachama.

"Naondoka Chadema kwa hiari yangu na najivua vyeo vyangu vyote na nyuma yangu hasa kutoka kata yangu nao watanifuata," amesema. 

Mbali na hao mapema leo, baadhi ya viongozi wa chama hicho  Mkoa wa Kilimanjaro akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Gervas Mgonjwa, wametangaza kujivua uanachama wa chama hicho kuanzia leo Jumapili, Mei 11, 2025.

Wengine waliojivua uanachama ni Katibu wa Bawacha Kanda ya Kaskazini, Rachael Sadick, Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Kilimanjaro, Grace Kiwelu, Mjumbe wa Kamati ya Tehama Kanda ya Kaskazini, Answary Kimaro na Mwenyekiti Mstaafu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Michael Kilawila

Makada hao ambao wengine wamepata kuwa wabunge, wametangaza uamuzi huo leo mjini Moshi, wakati wakizungumza na waandishi wa habari.

Miongoni mwa sababu walizozitaja kujiondoa Chadema ni madai ya kutokusikilizwa, viongozi kushindwa kukemea matusi yanayotolewa na baadhi ya wajumbe wa chama hicho.