Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fyatu anaweza kuzuia kutupiwa-tupiwa viatu

Baada ya mafyatu wa kaya jirani kumfyatua fyatu wao mnene, nimeogopa. Si juzi walimfyatua kwa kiatu kiasi cha kumtia aibu na gadhabu! Sijui hakupata shinikizo la moyo kwa namna alivyoaibishwa mchana kweupe. Japo simsikitikii, amenisaidia kuanza kujihami. Maana mafyatu wangu kwa kuigiza, asikwambie fyatu. Hivyo, nina mikakati ya kuepuka aibu hii. Ni aibu kiasi gani kutwangwa kiatu? Nasikia eti kiatu chenyewe kilikuwa kimepakwa manonihino. Sijui kama ni kweli au rongorongo za mafyatu za kumdhalilisha fyatu wao waliyemchoka, kudhalailishaji kwa ubabaishaji na ubadhirifu wake na wenzake. Kwa tunaojua maana ya kutupiwa kiatu, wanaokutupia au kukupiga kwa viatu, wamekuchoka, wanakudharau kwa kukulinganisha na shimo la choo.

Hivyo, ikitokea ukala kiatu, mbali na kuonyesha umelaaniwa na unachukiza, achia ngazi mara moja usingoje kutwangwa kinyesi au mayai viza, marungu na sime. Kitaalamu, hiyo ni kura ya hapana kwako na ulaji wako. Najua mafyatu wengi wananiponda kwa kunipa misifa nisiyostahili ilhali mioyoni wananiponda na kunichukia. Hawafanyi hivyo kwa sababu yoyote, bali kuning’ong’a na kunigeuza zwazwa. Nawatapeli. Nao, wananitapeli, tunatapeliana, na kufyatuana ngoma droo.

Wanadhani sijui kuwa wanajua kuwa ninawadanganya. Wao hawanidanganyi? Wanajua. Tunadanganyana na kufyatuana katika siasa zetu za kichovu na kisanii. Najua wanajua. Ninawatumia badala ya kuwatumikia, nao sasa wanaweza kutumia kiatu kuniaibisha. Ninawadharau, kumbe nao wananidharau! Hivyo, tunadharauliana kinamna au siyo? Unacheza na siasa nini? Kwa wasiojua wala kukumbuka, kwangu, siasa ni usanii sawa na usanii mwingine. Haina tofauti na karata tatu au mchezo wa kanyabwoya. Unaniuzia dhahabu feki, nakulipa kwa fedha feki. Katika nchezo huu, ninavuna nisipopanda na kupanda nisipovuna na mambo yanakwenda.

Ninatoa ahadi hewa na kupewa kura ya kula maraha. Ninakupa T-shirts na vitenge, na upuuzi mwingine, unanipa kura ya kula miaka mitano. Ajabu, nikishakutwisha mkenge, unaanza kulalamika ilhali wewe ndiye ulinipa pawa na ulaji!

Tokana na kadhia iliyotokea kwa mafyatu jirani, ifuatayo ndiyo mikakati yangu ya kuepuka nakama na zahama:

Kwanza, watakaokuja kwenye mikutano yangu ya hadhara watapaswa kuja pekupeku. Mfano, bangili, fimbo, kalamu, karatasi, mikanda, saa, simu, na nguo nzito ni mwiko kuja navyo. Hapa, waandishi wa umbea watapaswa watafute namna ya kuripoti mikutano yangu. Kuzuia aibu hata madhara, nitaamuru wote watakaohudhuria mikutano yangu kuvaa misuli tu ili kujihakikishia salama.

Pili, kuanzia sasa, nitahakikisha nanunua gari lenye vioo pande zote ili kunilinda na mafyatu waliofyatuka na kupanga kunifyatua iwe ni kwa viatu hata kunitemea makohozi.

Tatu, nitaamuru wote watakaohudhuria mikutano yangu wafungwe mikono ili wasitokee wa kunikata vibao au kunirushia mingumi. Je, nitafanyaje kuhusiana na miguu ili wasinipige mateke, makarate, na makung fu? Sijui niamuru wafunge pingu miguuni au walale kifudifudi ili niwe salama. Hili bado nalisukuti. Naamini nitapata jibu mujarabu.

Nne, nitahakikisha kila anayekaribia nilipo, anasachiwa ile mbaya ili wasinifanyie kitu mbaya kama yule jamaa wa kaya jirani.

Tano, nitapunguza mikutano ya hadhara. Hii itasaidia mafyatu kunimiss na kutaka kuniona bila kunidhuru. Nanajua wanajua ninavyowadhulumu.

Sita, kuepusha aibu, maumivu, na shari, kuanzia sasa nahubiri amani na mshikamano.

Saba, nitaamuru bunge la wapenda ubunge la mafyatu kutunga sheria inayotoa adhabu ya kifo kwa yoyote atakayenitupia kiatu au kitu chochote.

Nane, mabango yenye kubeba picha zangu lazima yawekewe ulinzi saa 24 wasijemalizia hasira zao kwangu.

Tisa, nitapiga marufuku ulaji na unywaji wa kitu chochote mahali popote nitakapokuwa. Nani anajua? Wanaweza kufyatua na kunipopoa na chupa hata mirija. Kinachoumiza siyo kuumia tu, bali aibu ya kutupiwa kitu chochote hata iwe kalamu, karatasi, au pini.

Kumi, kuanzia sasa, hakuna runinga itakayorusha live mikutano yangu. Who knows? Linaweza kunitokea zali nikaaibika bure.

Hivyo, kuepusha uwezekano wowote wa kutokea lolote, lazima nipige marufuku kuonyesha picha za mikutano yangu live.

Kumi na moja, kuanzia sasa nitakuwa nalindwa na jamaa zangu. Nitamteua mwanangu au mkwe wangu kuwa mkuu wa kikosi changu maalumu cha ulinzi kama alivyowahi kufanya Braza M7 kule UG. Kwa vile sina kitegemezi au mkwe mjeshi, lazima nimpe vyeo vya kigeshi vya upendeleo haraka sana ili kupambana na kadhia hii.

Kumi na mbili, ikishindikana, nitakodisha mamluki toka ughaibuni kama fyatu mnene wa kule Afrika ya Katikati ambaye siku zote huwekwa kati na mamluki toka kwa Putting. Pia, nitatoa njuluku kwa makampuni ya robot waone kama wanaweza kutengeza robot za kulinda wanene bila kujali zitagharimu njuluku kiasi gani.

Heshima na usalama wangu ni vya muhimu kuliko kaya. Isitoshe, njuluku za kumwaga kunipa raha na usalama zipo. Kwa nini kuishi kwa hofu wakati nina nyenzo? Si inapendeza?

 Hivi niko wapi? Ulevi huu! Hata viatu sina!