Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kova amshinda Nzowa mgogoro wa nyumba ya Serikali

Muktasari:

  • Mahakama ya Rufaa imehitimisha mgogoro wa nyumba ya Serikali kati ya Suleimani Kova na Godfrey Nzowa, ikithibitisha mmiliki halali ni Kova huku ikifuta amri ya Nzowa kulipa fidia ya Dola 200 kwa mwezi.



Arusha. Mahakama ya Rufaa imehitimisha mgogoro wa muda mrefu wa umiliki wa nyumba ya Serikali iliyopo Sekei, Arusha, kati ya waliokuwa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi, Suleimani Kova na Godfrey Nzowa, kwa kuthibitisha kuwa Kova alikuwa na sifa na haki ya kuinunua nyumba hiyo.

Hata hivyo, mahakama hiyo imempa Nzowa ushindi katika hoja moja na kufuta amri ya Mahakama Kuu iliyomtaka amlipe Kova Dola za Marekani 200 kwa mwezi, kama fidia ya mapato aliyodai kuyakosa, ikieleza kuwa madai hayo hayakuthibitishwa kwa ushahidi wa kutosha.

Uamuzi huo ulitolewa Julai 22, 2026 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, Gerald Ndika, Omar Othman Makungu na Mustafa Ismail, katika rufaa iliyokatwa na Nzowa dhidi ya Kova, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Baada ya kupitia hoja 10 za rufaa, Mahakama ilikubaliana na Mahakama Kuu kwamba Kova alikuwa mnufaika halali wa nyumba hiyo, huku ikisema hoja zote za Nzowa hazikuwa na msingi isipokuwa ile iliyohusu malipo ya fidia ya Dola 200 kwa mwezi.


Mzozo ulivyoanza

Mgogoro huo ulihusu nyumba ya Serikali Na. 203 (au 140), iliyopo Kiwanja Na. 40, Kitalu 3, Sekei, Arusha.

Kova na Nzowa walikuwa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi waliobadilishana vituo vya kazi mwaka 2001. Wakati Kova alipohamishiwa Kigoma, Nzowa alihamishiwa Arusha na kukabidhiwa nyumba hiyo Januari 8, 2002, ikiwa ni sehemu ya makabidhiano ya majukumu.

Baadaye Serikali ilipoanza kuuza baadhi ya nyumba zake kwa watumishi wa umma, Nzowa alidai alikuwa na haki ya kwanza kuinunua kwa kuwa ndiye aliyekuwa akiishi humo wakati huo.

Hata hivyo, nyumba hiyo iliuzwa kwa Kova na kusajiliwa kwa jina lake, hatua iliyomfanya Nzowa kufungua kesi kupinga uhalali wa mauzo hayo, shauri lililoenda hadi Mahakama ya Rufani baada ya Mahakama Kuu kumpa haki Kova.

Mahakama ya Rufaa imekataa hoja ya Nzowa kwamba mchakato wa kuwatambua wanunuzi wa nyumba za Serikali ulianza baada ya hotuba ya Rais ya Mei mosi, 2002.

Kwa mujibu wa Mahakama, ushahidi ulionyesha kuwa mchakato huo ulianza mwaka 2001 kufuatia Waraka Na. 7 wa Baraza la Mawaziri, uliotaka kuorodheshwa kwa nyumba zilizopendekezwa kuuzwa pamoja na watumishi waliokuwa wakiishi kwenye nyumba hizo.

Majaji wamesema hotuba ya Rais ilikuwa sehemu ya utekelezaji wa uamuzi uliokwisha kufanywa na Serikali, hivyo haikuwa mwanzo wa mchakato huo.

Kwa msingi huo, Mahakama ya Rufan imekubaliana na Mahakama Kuu kwamba Kova alikuwa na sifa za kununua nyumba hiyo kwa kuwa alikuwa akiishi humo wakati Serikali ilipoanza kuwatambua wanunuzi.

Mahakama pia ilikataa hoja ya Nzowa iliyodai kuwa mkataba wa mauzo kati ya Kova na Serikali ulikuwa batili na kwamba hati ya umiliki ilipaswa kufutwa, ikisema hakuna dosari iliyothibitishwa katika mchakato wa mauzo.

Aidha, ilikataa madai kwamba Kova aliwasilisha taarifa za uongo kuhusu ukaaji wake, ikieleza kuwa alikubali ofa ya Serikali kwa nyumba aliyokuwa akiishi wakati wa mchakato wa utambuzi.


Nzowa alipewa ofa Kigoma

Katika hoja nyingine, Nzowa alidai hakuwahi kupewa ofa rasmi ya kununua nyumba ya Serikali iliyopo Heri Avenue, Kigoma.

Hata hivyo, Mahakama ilibaini kuwa nyaraka zilizowasilishwa mahakamani zilionyesha alipewa nafasi ya kuomba kuinunua Juni 17, 2002, na baadaye akakumbushwa tena Januari 9 na Oktoba 4, 2004, lakini hakuitikia ofa hiyo hadi ilipofutwa.


Aepuka kulipa fidia

Pamoja na uamuzi mwingine, Mahakama ya Rufaa imekubaliana na Nzowa kuhusu hoja ya fidia ya Dola 200 kwa mwezi.

Awali, Kova alidai kuwa kuendelea kwa Nzowa kuishi katika nyumba hiyo kulimnyima mapato ya kodi ya Dola 400 kwa mwezi lakini Mahakama Kuu ilipunguza kiwango hicho hadi Dola 200 kwa mwezi baada ya kuona madai hayakuthibitishwa kikamilifu.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufaa imesema Kova hakuwasilisha ushahidi wa kuthibitisha thamani ya kodi aliyoidai, kama mikataba ya upangishaji, risiti za kodi au nyaraka zinazoonyesha thamani ya soko ya nyumba hiyo.

Kutokana na hilo, majaji hao wamesema mahakama haiwezi kubuni kiwango cha fidia kwa kupunguza tu kiasi kilichodaiwa bila kuwepo ushahidi wa kuthibitisha hasara iliyopatikana.

Kutokana na sababu hiyo, Mahakama ya Rufani  imekubali hoja ya sita ya rufaa na kufuta amri ya Nzowa kumlipa Kova Dola 200 kwa mwezi.

Hata hivyo, Mahakama imesisitiza kuwa ushindi huwa hoja hiyo, haukubadilisha uamuzi kuhusu umiliki wa nyumba hiyo.

"Kwa ujumla, isipokuwa kwa msingi wa sita wa rufaa ambao tunauruhusu, tunaona rufaa iliyobaki haina msingi na tunaikataa," imesema Mahakama ya Rufani katika hukumu yake.

Mahakama ilihitimisha kuwa mauzo ya nyumba hiyo kwa Kova yalikuwa halali na kwamba hakukuwa na dosari katika mchakato wa kuuza nyumba hiyo. Pia imeamuru kila upande kubeba gharama zake za kesi.