Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mashambulizi dhidi ya viongozi na hisia za hasira za wananchi

Muktasari:

  • Video ya tukio hilo ilisambaa kwa haraka kwenye mitandao ya kijamii, na ndani ya dakika chache, taifa lilikuwa linazungumzia jambo moja: Rais wa Kenya amevamiwa hadharani.

Katika jua kali la alasiri, Rais wa Kenya, William Ruto alisimama mbele ya umati mkubwa katika Kaunti ya Migori, akizungumza kuhusu gharama ya juu ya maisha na juhudi za Serikali kupunguza bei ya mbolea.

Umati ulikuwa ukimiminika kwenye uwanja wa Kehancha, Migori, wakati Rais Ruto aliposimama jukwaani kuzindua mradi wa nyumba nafuu.

Hotuba yake ilikuwa ikienda vizuri mpaka kiatu kilipopita kwa kasi kuelekea usoni mwake.

Mkono wake wa kushoto ukiwa juu akitoa ishara ya salamu, ghafla na kwa mshangao wa wote kiatu hicho kilirushwa kutoka kwenye umati wa watu kikipita kwa kasi na kupiga mkono wake wa kushoto karibu na bega.

Video ya tukio hilo ilisambaa kwa haraka kwenye mitandao ya kijamii, na ndani ya dakika chache, taifa lilikuwa linazungumzia jambo moja: Rais wa Kenya amevamiwa hadharani.

"Wacha waendelee!" alisema kwa sauti kubwa, akiwaonyesha maofisa usalama wasimchukue mtuhumiwa. Ruto alifanikiwa kukizuia kwa mkono wake wa kushoto, na tukio hilo lilinaswa kwenye video na kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii. Waziri wa Mambo ya Ndani, Kipchumba Murkomen, alithibitisha kuwa watu watatu walikamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Tukio hili limeibua maswali kuhusu usalama wa viongozi wa kitaifa na kuleta kumbukumbu ya matukio mengine ya aina hiyo duniani.

"Hii ni aibu!" alisema Isaac Mwaura, Msemaji wa Serikali, akitaja tukio hilo kuwa "tishio kwa heshima ya urais" na kutaka waliohusika wakamatwe haraka. "Je, nini kitatokea tukiamua kurushiana viatu? Tunawafundisha nini watoto wetu?" alihoji kupitia mtandao wa X.

Rais wa Kenya, William Ruto

Katika video nyingine ya tukio hilo, iliyosambazwa na Ofisa Mwandamizi wa Ikulu, Dennis Itumbi, mtu mmoja anaonekana akinyanyua kiatu kana kwamba ni kamera  “shoe-cam” lakini mwingine akakipiga kwa mkono kwa hasira, akilalamikia kuzuia mtazamo wake. “Bahati mbaya, kikaruka… moja kwa moja hadi kwa rais,” Itumbi aliandika kwenye Facebook.

Polisi walikamatwa watu watatu, ingawa hakuna aliyekiri kufanya kosa. Dennis Itumbi, ofisa wa ofisi ya rais, alijaribu kudhoofisha tukio kwa kusema kuwa ilikuwa kitu cha bahati mbaya, mtu alikuwa akicheza na kiatu, kikapasuka na kurushwa.

Lakini wengi waliona kitu kikubwa zaidi. "Je, kama kiatu hicho kingekuwa risasi?" aliuliza Nelson Koech, akisema kuwa tukio hilo lilidhihirisha hatari ya kipekee kwa usalama wa viongozi.

Migori, eneo lenye historia ya upinzani, ilikuwa mwaka mmoja tu tangu Rais Ruto na Raila Odinga waliposaini mkataba wa amani. Lakini, gharama ya maisha na mzigo wa kodi zilizokwama kwenye koo za Wakenya zilizidi kuchochea hasira. Kiatu hicho kilikuwa si tu kitu kilikuwa sauti ya wale wasio na sauti.

Hili halikuwa tukio la kwanza la aina hiyo kutokea katika eneo la Migori. Miaka 10 nyuma, mwaka 2015, Rais wa zamani, Uhuru Kenyatta, alikumbwa na tukio la kurushiwa viatu katika kaunti hiyo hiyo, jambo ambalo lilisababisha kusitishwa kwa baadhi ya miradi ya maendeleo kwa muda.

Inaonekana Kaunti ya Migori inayojulikana kuwa ngome ya kisiasa ya mpinzani wa Ruto, Raila Odinga, ina historia ya mvutano wa kisiasa wa wazi.

Ingawa Odinga na Ruto walitia saini makubaliano Machi 2025 ya kupunguza mvutano wa kitaifa, tukio hili lilionyesha hisia za wananchi bado zinaweza kuzua misukosuko isiyotabirika.


Matukio kama hilo Afrika Mashariki

Katika historia ya kisasa ya Afrika Mashariki, hili halikuwa tukio la kipekee. Katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka Oktoba 2005, mgombea wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, alikumbana na tukio hatari katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Mtu mmoja alifanikiwa kupenya kwa walinzi na kumvamia jukwaani, akimng’ang’ania mguu. Alidaiwa kuwa ametumwa na mganga wa kienyeji ili apate utajiri kwa kumvamia mtu maarufu mbele ya hadhira kubwa.

Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Kwa kutumia mafunzo yake ya kijeshi, Kikwete alimdhibiti mshambuliaji kabla ya walinzi kuingilia kati.

Miaka mitatu baadaye, Oktoba 16, 2008, akiwa ziarani mkoani Mbeya, msafara wa Rais Kikwete ulirushiwa mawe yaliyolenga magari sita, yakiwamo ya mawaziri na waandishi wa habari.

Kikwete hakudhuriwa, lakini alilazimika kubadili ratiba yake kwa tahadhari zaidi. Huo ni wakati ambao nchi ilikuwa imekumbwa na kashfa ya Richmond, iliyosababisha aliyekuwa Waziri mkuu, hayati Edward Lowassa kujiuzulu na kusababisha mtikisiko mkubwa wa kisiasa.


Alichokumbana nacho Rais Bush, Iraq

Mashambulizi haya ya hadharani si ya Afrika pekee. Desemba 14, 2008, mjini Baghdad, wakati wa mkutano wa pamoja kati ya Rais George W. Bush na Waziri Mkuu wa Iraq Nouri al-Maliki, mwandishi wa habari Muntadhar al-Zaidi aliruka kutoka kwenye kiti chake na kurusha viatu viwili mfululizo kwa Bush.

“Hili ni busu la kwaheri kutoka kwa watu wa Iraq, wewe mbwa!” Mtu huyo alipaza sauti kwa Kiarabu. Rais Bush alikwepa kwa ustadi, lakini taharuki ilitanda ukumbini.

Rais mstaafu wa Marekani, George W. Bush

Al-Zaidi alikamatwa, kushtakiwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu (baadaye kikapunguzwa hadi mwaka mmoja).

Katika mahojiano baada ya kuachiwa, alieleza kuwa aliteswa kwa kupigwa nyaya, kuchomwa kwa kutumia sigara, na kufanyiwa mateso ya umeme kisha kulazimishwa kuandika barua ya msamaha. Baadaye alihamia Uswisi, akasema: “Sijutii. Laiti ningekuwa na viatu zaidi.”

Tukio hilo lilizua hisia kali kote duniani. Kwa wengi katika ulimwengu wa Kiarabu, Al-Zaidi aligeuka kuwa shujaa wa watu.

Alipewa zawadi, nyumba na hata viatu vya dhahabu lakini alibaki kuwa mtu wa kawaida kifedha.

Sarkozy naye yalimkuta Ufaransa

Juni 30, 2011, nchini Ufaransa, Rais Nicolas Sarkozy alikumbana na hali kama hiyo. Akiwa katika mji wa Brax kusalimiana na wananchi, mtu mmoja alinyosha mkono na kumvuta kwa nguvu karibu aanguke.

Hermann Fuster, mshambuliaji huyo alikuwa mfanyakazi wa sekta ya sanaa asiyekuwa na rekodi ya uhalifu.

Alikamatwa papo hapo, na baadaye kuhukumiwa kifungo cha miezi sita lakini baadaye kikasimamishwa.

Pia alilazimika kufanya kazi ya kijamii na kuhudhuria kozi ya uraia. Alidai alitaka tu kumsemesha vibaya rais, na ujumbe aliomtumia mke wake wa zamani kabla ya tukio alieleza kuwa ni mzaha.

Tukio hili liliibua mijadala kuhusu usalama wa viongozi wa kitaifa hata katika nchi zilizo na mifumo imara ya usalama.

Kama ilivyokuwa kwa Silvio Berlusconi wa Italia mwaka 2009, aliporushiwa usoni sanamu ndogo ya ukumbusho, na kupata majeraha ukweli unabaki kuwa hata sekunde chache zinaweza kubadilisha historia ya taifa.

Matukio haya ya kihistoria yanaunganika kupitia mstari mmoja wa dhahabu: hisia za wananchi, usalama wa viongozi, na hatari ya kudharau dalili ndogo za kukata tamaa.

Lakini swali kuu linabaki: Je, tunajifunza nini kutokana na matukio haya? Ikiwa urais ni taasisi ya heshima, basi lazima iwe ya pande zote.

Wananchi wanahitaji kusikika, na viongozi wanapaswa kujifunza kusikiliza kabla ya mawe au viatu kurushwa. Kama alivyosema Bush baada ya kukwepa viatu: "It was a size ten." Alitabasamu, lakini ulimwengu ulihisi uzito wa ujumbe.

Katika enzi ya mitandao ya kijamii na siasa za hisia kali, tukio dogo linaweza kugeuka kuwa historia. Na kwa wale wanaoongoza, hatari haiko tu kwenye kura bali pia kwenye kiatu kinachorushwa ghafla kutoka kwa umati usioridhika.