Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KONA YA MSTAAFU: Mikopo ya benki inavyotubamiza wastaafu!

Tokea hawa tunaolazimika kuamini kuwa ni miungu wadogo wa dunia walipofanya jambo jema la kupitisha pensheni ya mstaafu kwenye akaunti yake ya benki, japo akaunti yenyewe ilikuwa imeishanyauka, wastaafu sasa hawatalazimika kukanyagana kule Posta ili kupokea vijipensheni vyao, baadhi ya benki za dot.com zikajiongeza fasta.

Tukumbuke kwamba miaka michache tu nyuma, benki hizo za dot.com zilijiwekea zuio kwa mstaafu yeyote kupewa mkopo kwenye benki zao kwa maelezo hafifu kuwa wastaafu, baada ya kustaafu kisheria na kufikisha miaka 60, basi hata utafutaji wao wa hela 'ulistaafu', kwa hiyo hata ulipaji wao wa mikopo ungekuwa 'shughuli' kubwa!

Hizi benki za dot.com zikaona kuwa mstaafu akisha kanyagana na wastaafu wenzake kule Posta ili kupata kijipensheni chake, kule njiani, wakati akirudi nyumbani, akapitia kilo moja ya nyama na kilo moja ya mchele ili kujipongeza, na kupitia pharmacy kununua dawa kwa ajili ya magonjwa yake ya uzee, mpaka alipofika nyumbani, kijipensheni chake alichochukua tayari kilikuwa historia siku ile ile!

Benki za dot.com zikaona isiwe tabu. Zilikuwa na mambo mengi muhimu ya kufanya badala ya kufukuzana na wastaafu ambao hata utafutaji wao wa pesa 'uliishastaafu'! Zikaweka zuio la kutokopesha wastaafu. Benki nyingi zikawa 'don't come' (Kisambaa, kwa msisitizo!), zikiwaambia wastaafu wasije benki kukopa maana wameishazeeka na watasumbuana bure kwenye marejesho ya mkopo watakaopewa!

Ikawa hivyo. Ndipo hapo kibubu cha akiba ya wastaafu kikafanya jambo jema la kuamua kupitisha pensheni za wastaafu kwenye akaunti zao za benki zilizokuwa zimeanza kunyauka, maana kiinua mgongo chao njiwa hakikufuata kanuni ya kustahili kupata japo asilimia 50 tu ya waliowaachia madaraka. Tukiaminishwa kuwa ile ilikuwa kanuni kwa ajili ya waheshimiwa tu, sio kwa kila kajam... kumradhi... sio kwa kila kima cha chini wa nchi! Likatushuka shuu.

Haya, pensheni yetu njiwa ya shilingi elfu hamsini sasa ikawa inapitia kwenye akaunti zetu, na benki nazo, zilipoona pensheni yetu ya mwezi sasa inapitia kwenye akaunti zetu za benki, nazo zikajiongeza.

Badala ya kuendelea kuwa za 'don't come' zisizotaka mstaafu akope kwao, sasa zikajiongeza na zikawa kweli benki za dot.com, maana zilikuwa na uhakika wa kupata marejesho ya mikopo yao bila kufukuzana na mtu!

Naam, wastaafu sasa tukapata mikopo tuliyoaminishwa na benki hizi kwamba ni ya kuboresha maisha yetu, pamoja na kwamba hali zetu, sisi wastaafu, zingeboreka zaidi kama siri-kali au kibubu chetu vingeamua tu kuwapa wastaafu wa kima cha chini pensheni ya shilingi laki tano kwa mwezi. Maisha ya wastaafu yangeboreka maradufu, lakini nani anawasikiliza wastaafu wala kujali kilio chao?

Unaambiwa 'utamu' wa mikopo ya wastaafu umekuwa mkubwa kiasi kwamba benki hizi za dot.com, majuzi zilikuwa zikituambia sisi wastaafu 'don't come', tusiende kukopa kwenye benki zao maana tu wazee sana. Sasa zimekuwa dot.com hasa, maana mkopo ukifika nusu wanawasiliana na wewe fasta ili uje kuongeza mkopo mwingine!

Wana wasiwasi gani? Pensheni yako inapitia kwao, na wanakata fasta kirahisi kinachotakiwa kukatwa, ndipo wanakuingizia mabaki ya pensheni yako.

Kuanzia mwaka 2023, mimi ninapata pensheni ya Shilingi elfu 46 kutoka shilingi laki moja na elfu tano nilizokuwa nikipata kabla shida zangu zisizoisha zilipofanya nikope... ili niboreshe maisha!

Usiyaboreshe ukiwa kwenye ajira kwa miaka 40, uyaboreshe kwa mkopo wa benki zetu za 'don't come' (rudia, Kisambaa kwa msisitizo!), pamoja na kutuaminisha kuwa sasa ni benki za dot.com?

Mikopo ya wastaafu sasa imenoga kweli. Toka mwezi wa kumi mwaka jana tulipopandishiwa pensheni kuwa shilingi laki mbili na nusu, benki nazo zimecharuka kuleta vivutio ili tukajibamize tena humo.

Benki zetu sasa zina kazi ya kututumia ujumbe asubuhi na jioni kuwa sasa mkopo tutakaochukua tunaweza kuulipa hata kwa miaka kumi. Miaka kumi?

Hawasemi kuwa wanapunguza riba kwa wastaafu, bali wanakazania tu kusema sasa unaweza kulipa mkopo uliokopa kwa miaka kumi. Riba iko pale pale, lakini makato yamepungua kutokana na urefu wa miaka ya kulipa mkopo huo. Yaani ukope mkopo mwaka 2025 ukiwa na miaka 66, uulipe mpaka mwaka 2035 ukiwa na miaka 76. Huko ni kuboresha maisha ya mstaafu ama ni kuyanyong'onyeza zaidi maisha yake?

Tunadhani kibubu kinaweza kufanya jambo jema zaidi la kuboresha maisha ya mstaafu. Kila kwenye ofisi ya kibubu kuwe na dawati ama ofisi itakayotoa mikopo midogo midogo yenye riba nafuu kwa wastaafu itakayoboresha kweli maisha yao. Hela zao ziko huko kibubuni, na kibubu hakitakuwa na haja ya kufukuzana na mstaafu ili kupata marejesho ya mkopo waliomkopesha. Si hela zake wanazo kibubuni?